Pendo pendo mwashibana, lenu la jambo muhali,
Mwanoga mwaambiana, mwingine hatobadili,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.
Mapenzi yake matamu, wanogewa na mumeo,
Kamwe haiishi hamu, ana upya kila leo,
Penzi lashika hatamu, huwajali visemeo,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.
Mumeo umemkuta, anao na ndugu zake,
Binti unafurukuta, hutaki kwako wafike,
Wataka mume kufyata, lako tu nd’o alishike,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.
Siyo vema mwanakwetu, si tabia yenye sudi,
Nao waoneshe utu, upendo kwao si budi,
Mabezo si malikitu, siwoneshe ukaidi,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.
Kwa mumeo umekuta, tayari alishazaa,
Kabla hajakupata, akupe wake wasaa,
Mtoto wamkorota, zaidi wamkataa,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.
Nawe umepata mke, tayari ana mtoto,
Simfanye ateseke, kuiweka nyumba joto,
Haki yake apendeke, siyo kuleta fukuto,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.
Usipende nusu nusu, nani tena wamwachia,
Yake yote yakuhusu, nayo uyapende pia,
Sisite kumruhusu, nduguze kutembelea,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.
Mapenzi huleta raha, kwa dhati mkipendana,
Tena huipata siha, kama mwasikilizana,
Siyafanyie mzaha, mkaja kuumizana,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.
Cha mwenziyo kyone chako, halafu ukithamini,
Kipende moyoni mwako, sikitenge asilani,
Sikifanyie vituko, kamwe kamwe abadani,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.
Ya kusema nimesema, ni vema kuyasikia,
Yatunze yaliyo mema, kazi ukayafanyia,
Pendo lijae hekima, nyote kulifurahia,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.
source: http://fadhilimshairi.blogspot.com/
No comments:
Post a Comment
Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.