Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Tuesday, February 28, 2012

Kwa elimu ile ile, kwa nini mishahara tofauti?

NIMEONA hakuna sehemu nyingine yoyote ambayo naweza kufikisha mawazo na hisia zangu zaidi ya kupitia kwa magazeti yanayoandika kwa uwazi bila kuficha uozo unaofanywa na viongozi wa nchi hii.
Naandika makala hii muda muafaka kabisa ilihali nikiwa na mshangao na kujiuliza maswali mengi yasiyokuwa na ufumbuzi katika halmashauri ya kichwa changu.
Nikiwa kama mtumishi wa umma katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, naamini sana hasa pale tunapokuwa tunawachagua viongozi wetu wa kiserikali tunataraji mambo mengi sana kutimiziwa na viongozi tunaowachagua.
Hii ni pamoja na kuhakikisha maisha ya Watanzania yanakuwa bora kama ilani ya chama tawala inavyojinadi. Ninaposema maisha bora namaanisha maisha mazuri kwa wakulima waliopo vijijini na mijini, wafanyakazi na wale wote walio tegemezi.
Kwa upande wa wakulima uhakika wa dhana/pembejeo bora za kilimo zinazopatikana kwa uhakika na kwa bei nafuu. Kwa upande wa wafanyakazi kuhakikisha maslahi ya wafanyakazi yanaboreshwa kwa kiwango stahiki.
Nitajikita zaidi katika upande wa wafanyakazi wa umma. Maswali ambayo yanakuwa yananisibu ni kitu gani hasa kinaifanya Serikali kuwa na kigugumizi  katika kuboresha mishahara ya watumishi wa serikali ilihali fedha zipo?
Nikivuta kumbukumbu zangu mapema mwaka 2010 Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) kilitishia kuitisha mgomo nchi nzima kuishinikiza Serikali kupandisha mishahara ya watumishi wa serikali lakini kutokana na vitisho visivyokuwa na msingi wowote kwa kutishiwa na kubatizwa majina ya kudhalilisha watumishi wa umma, chama cha hicho kilisitisha mgomo huo mpaka sasa ikiwa imetimia takribani mwaka mmoja bila hatua yoyote madhubuti kuchukuliwa kwa pande zote mbili.
Upande wa Serikali umeshindwa kutekeleza madai ya wafanyakazi na kwa upande wa chama cha wafanyakazi kutochukua hatua zaidi madhubuti ya kuishinikiza Serikali kuongeza mishahara ya wafanyakazi.
Binafsi nashangazwa sana na ngazi ya mshahara anayelipwa mtumishi aliye na elimu ya shahada  TGS D-455,100 ambapo baada ya makato anatoka na Tsh. 370,902.  Kumbuka mtumishi huyu ana wategemezi wengi sana ikiwa ni pamoja na wazazi au walezi waliomsomesha, wadogo zake pia ana familia yake ambao ni mke na watoto.
Wote hao wanaamini mtumishi huyu ameajiriwa na wanamtazama kwa macho yote mawili wakitaraji kupata usaidizi wa kifedha. Mtumishi huyu amediriki kupoteza miaka mitatu na pengine mine kujikita zaidi katka fani (profession), leo hii unamlipa mshahara hovyo kabisa.
Mshahara kama huu ukiuchanganua kiundani zaidi hata ingekuwa anautumia peke yake hautoshi kulipa kodi ya nyumba matumizi ya chakula, usafiri na matumizi mengine ya dharura ingawa kuna kada zingine kama jeshi la polisi na JWTZ na magereza hupendelewa kulipwa  malipo ya ziada kulipia kodi za nyuma, usafiri na resheni katikati ya mwezi.
Kutotosha kwa mshahara pia kunatokana na mfumuko wa bei wa vitu mbalimbali uliopo hapa nchini kwetu, mfumuko huu umeshindwa kudhibitiwa kutokana kutokuwepo kwa mikakati kabambe na sera madhubuti huzuia mfumuko huu.
Hazijapita siku nyingi sana tumesikia kilio cha wabunge wetu ambao ni wabinafsi sijapata kuona wakijipigania ipasavyo wakishinikiza kupandishiwa mishahara yao na posho kwa siku (sitting allowance) wengine kwa kusinzia kwenye kiti kutoka 70,000/= hadi kufikia 200,000/=
Taarifa zinathibitisha wazi kuwa posho hizi mpya zimekwisha sainiwa na zimekwishaanza kulipwa ingawa kuna mikanganyiko wa kauli zinazokinzana kutoka kwa viongozi mbalimbali ikiwa ni pamoja na taarifa za Ikulu, Katibu wa Bunge na kwa Spika wa Bunge.
Katika hili je fedha zinazotumika kuongeza posho za wabunge  zinatoka wapi ilihali za kuwaongezea watumishi mishahara yao inakosekana na wakati mwingine kucheleweshwa kwa mishahara ya watumishi  mfano mzuri ni ya watendaji wa balozi mbalimbali za Tanzania kama taarifa ya kamati ya Bunge ilivyobaini ikiongozwa na Mwenyekiti wake John M. Cheyo. Binafsi sijawahi kusikia kauli za wabunge wakishikia kidedea kutetea kuongezwa kwa mishahara ya watumishi badala yake wanaona ni bora kutetea matumbo yao tu. Hivi hawa wabunge huwa wanamuwakilisha nani bungeni kama hawatetei  maslahi ya watu waliowachagua?
Mbaya zaidi mfumo unaotumiwa na watawala wa nchi hii ni ule ambao kwa lugha ya kiingereza wanaouita “Divide and Rule” Leo hii ukiangalia mishahara wanaolipwa watumishi wa umma wenye elimu na kada sawa katika sekta mbalimbali inatofautiana kwa kiasi kikubwa  sana. 
Kuna mashirika ya umma (parastatal organizations) kama vile Benki kuu (BOT), BRELA, Shirika la Uwekezaji  la Taifa, TRA, NIC, mifuko ya jamii  NSSF, PPF, LAPF, n.k  Kwa wanaobahatika kupata kazi katika maeneo nyeti kama haya ipo wazi kuwa mishahara yao inakuwa ni mikubwa zaidi.
Hapa huwa najiuliza hawa wanaofanya kazi katika maeneo haya elimu zao zina tofauti gani na yule anayefanya Serikali za Mitaa au Serikali uu? Kwa nini walipwe mishahara minono zaidi wakati elimu zao ni sawa na za wale wa Serikali za Mitaa?
Hivi Serikali imesinzia katika hili au imegawanyika vipande vipande? Kwa nini mishahara ya watumishi wote wa umma isingekuwa sawa (uniform)?
Nilibahatika kusoma somo la uchumi nikiwa kidato cha tano na sita, kwa bahati nzuri nilibahatika kufundishwa sababu zinazopelekea kutofautiana kwa mishahara  baina ya waajiriwa yaani salary differentiation.
Hiyo ni pamoja na ugumu wa kozi anayoisomea mtu, ugumu  wa kazi na miaka anayotumia kupata elimu yake mfano udaktari, injinia  wanatumia miaka zaidi ya mitatu lakini sikufundishwa kuwa ukibahatika kupata kazi TRA, NSSF, BRELA, Benki Kuu au kuwa mwanasiasa kama mbunge mshahara wako utakuwa mnono kama nyama ya nundu.
Pia sikufundishwa kuwa ukifanya kazi Serikali za Mitaa utakuwa na mshahara mdogo, la hasha.
Kwa upande mwingine madai ya madaktari ambayo imetikisa nchi hii kwa siku kadhaa na kuchukua kurasa za magazeti na vyombo mbalimbali vya habari, yalikuwa ya msingi kabisa ukiachilia mbali madhara yaliyojitokeza kutokana na mgomo huo.
Siamini kama kuna kada muhimu zaidi ya nyingine. Kila kada ina umuhimu wake na zinategemeana kama mlishano wa “ecosystem” Katika mgomo wa madaktari sikusikia kauli yoyote chafu ya kuwakashifu madaktari kama ile iliyotolewa dhidi ya chama cha wafanyakazi TUCTA mwaka 2010 pale walipotaka kugoma.
Leo hii daktari anasikilizwa kuliko wengine kwa vile madhara yake yanajitokeza papo kwa papo. Ikumbukwe kuwa kuna madhara mengine hujitokeza baadaye mfano waalimu wakigoma na pia watumishi wengine wa Serikali kama wahasibu wachumi, maafisa ugani n.k.
Serikali hii kiziwi imekuwa ni ya kibaguzi na imekuwa na tabia ya kuwasikiliza waalimu na watumishi wa Afya zaidi kuliko watumishi wengine, daktari au mwalimu akikohoa tu Serikali inahaha kutafuta suluhu.
Ukiangalia mshahara wa nesi aliyekomea kidato cha nne na mwenye elimu ya cheti analipwa mshahara mkubwa zaidi ukilinganisha na mtumishi mwenye elimu ya chuo kikuu yaani digrii.
Hii ni fedheha, kebehi na dharau kwa kada zingine na katika hili Serikali imefanya maamuzi ambayo siyo sahihi hata kidogo.
Nakumbuka katika safari yangu ya kimasomo sikuwahi kufeli mitihani ya kitaifa tangu darasa la saba, kidato cha nne, kidato cha sita na kupata divisheni one hadi namaliza shahada yangu ya chuo kikuu.
Nikiangalia mshahara wangu hauendani na jitihada nilizokuwa nazo wakati nasoma. Lakini kwa waliofeli kwa kupata divisheni four na kukimbilia ualimu na unesi wana mishahara minono kuzidi mimi mwenye shahada hadi natamani kama ningefeli ili nikasome unesi nilipwe mshahara mzuri.
Wako wapi wanaojiita wapanga mipango na sera, wanapanga mipango ipi na sera zipi zisizokuwa na tija na maslahi kwa Watanzania? Ni nani anayepanga mishahara ya watumishi wa Serikali?

Raia mwema

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.