Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Wednesday, February 29, 2012

Siri Ya Waraka Wa Mwakyembe Yafichuka

• Kisa ni kifo cha ghafla cha mhudumu ofisini kwake


na Mwandishi wetu
WARAKA wa siri ulioandikwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe, umezidi kuibua mambo mapya.

Waraka huo ulioripotiwa mara ya kwanza wiki iliyopita na gazeti hili na kueleza mbinu, mahala ambapo waziri huyo anaamini aliwekewa sumu kupitia sabuni na taulo vilivyowekwa ofisini kwake kwenye chumba cha kuoshea mikono, safari hii waraka huo unaendelea kwa kumtaja mhudumu aliyetumika kuweka vitu hivyo.

Kupitia waraka huo alioutoa kwa ndugu na rafiki zake wa karibu, Dk. Mwakyembe anasema mhudumu aliyetumika bila kujijua ni wa kike kutoka katika kijiji cha Ipinda, wilayani Kyela, mkoani Mbeya, ambaye alihamishiwa ofisini kwake.

Inaelezwa kuwa mhudumu huyo aliletwa katika ofisi hiyo siku chache kabla ya siku ya kuweka sabuni na taulo jipya ofisini kwa waziri huyo.

“Nilipoona kuwa najikuna mfululizo mara baada ya kunawia sabuni hiyo, siku ya tatu nilikuwa na wazo la kupeleka vitu hivyo kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, lakini nilipofika ofisini, vilikuwa vimeshatolewa,” anasema Dk. Mwakyembe kupitia waraka huo.

Dk. Mwakyembe ambaye yuko nchini India kwa awamu ya pili ya matibabu, anasema alianza kumuuliza maswali ya kina mhudumu huyo ili kujua kwa nini vifaa hivyo viliondolewa ghafla wakati alivitumia siku moja, hakufanikiwa kupata majibu ya kina.

Naibu waziri huyo ambaye pia ni Mbunge wa Kyela, anadai katika mazingira ya kutatanisha, tena ndani ya muda mfupi tangu alipoanza kuathirika baada ya kunawia sabuni na kujifutia taulo hilo, mhudumu huyo wa kike alifariki na kuzikwa kijijini kwao Ipinda.

Tukio la kufariki ghafla kwa mhudumu huyo bila kuugua, limeacha maswali mengi sio tu kwa Dk. Mwakyembe, bali pia hata kwa rafiki zake wa karibu ambao wanaamini kwamba aliwekewa sumu.

Hata hivyo uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kuhusiana na taarifa kwamba kuna mhudumu mmoja wa kike wa Dk. Mwakyembe alifariki zilithibitisha kuwa ni kweli.

Mmoja maafisa wa juu wa wizara hiyo, aliliambia Tanzania Daima Jumatano kwa sharti la kutotaja jina lake kuwa ni kweli mhudumu huyo aliyemtaja kwa jina moja la Sara Richard ambaye alikuwa akimsadia Naibu Waziri huyo alifariki Septemba 29, mwaka jana, na kuzikwa kijijini kwao Ipinda.

“Ni kweli kuna mhudumu mmoja ofisini kwa Dk. Mwakyembe alifariki mwaka jana. Ila sijui aliugua ghafla au vipi hilo sijui; isipokuwa ni kweli kwamba mwaka jana tulimpoteza mtumishi mmoja na tulimsafirisha hadi kwao Mbeya,” kilisema chanzo chetu cha habari.

Akihojiwa na gazeti hili kuzungumzia waraka huo na tukio hilo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha, alisema hajauona na kusisitiza kuwa Jeshi la Polisi linafanya uchunguzi wa kina kubaini ukweli wa jambo hili.

Hadi sasa wingu zito limetanda kuhusu afya ya Dk. Mwakyembe.

Wakati taarifa zisizo rasmi zikisema amepewa sumu, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Nchini (DCI), Robert Manumba, amesema hajalishwa sumu...
 

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.