Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Mohammed Gharib Bilal,akisalimia wananchi alipowasili kwenye Soko la Tunduma juzi, kwa ajili ya kuzindua soko hilo lililoteketea kwa moto baada ya kukarabatiwa.

Stephano Simbeye na Godfrey Kahango,

Tunduma

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Mohamed Gharib Bilal jana alianza vibaya ziara yake mkoani Mbeya baada ya kupokelewa kwa zomeazomea za kulaani ufisadi, huku wananchi wakinyoosha vidole viwili juu, kuonyesha alama inayotumiwa na chama kikuu cha upinzani cha Chadema.

Wananchi hao ambao waliokuwa wazomea walimshangilia kwa nguvu mbunge wa Jimbo la Mbozi Mashariki (Chadema), David Silinde aliposimama kwa kuimba wakismea; “Rais...rais....rais...”

Hali hiyo ilisababisha zoezi la kutambulisha wageni mbalimbali waliojifika kumpokea Dk Bilal ambaye alifika eneo hilo kufungua soko la Tunduma, kukwama kutokana na wananchi hao kuzidisha kuzomea huku wa kimba; “Fisadi..., fisadi...!”

Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Gabriel Kimolo alijikuta katika wakati mgumu kutokana na kuzomea huko aliposimama kusoma ratiba ya ugeni huo.

Naye Mwenyekiti wa Soko la Tunduma alisimama kusoma taarifa ya soko hilo, lakini kelele hizo za wananchi hao ziliwafanya washindwe kusikika vizuri.

Huku hali ikiwa bado haijatulia, DC Kimolo alilazimika kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro ili amkaribishe Makamu wa Rais, aweze kufungua Soko la Tunduma ambalo liliteketea kwa moto Novemba 28, mwaka jana lakini alipata wakati mgumu kutokana na kelele za wananchi hao.

Kandoro alijitahidi bila mafanikio kuwatuliza wananchi hao kwa kuwasihi kuacha kuzomea na kupiga kelele.

Hata hivyo alimkaribisha Dk Bilal azungumze nao, wakati bado kukiwa na hali ya zomeazomea.

Hali yawa tete zaidi

Dk Bilal alipopanda jukwaani kuzungumza, wananchi hao ambao wengi walikuwa vijana, waliendelea kupiga kelele huku wakinyosha vidole viwili juu pamoja na vitambaa vyenye rangi za bendera ya Chadema.

“Nawaomba tusikilizane, nchi yetu imeweka utaratibu wa kusikilizana na kufikia muafaka, pia zipo mamlaka zilizowekwa kwa ajili ya kusimamia masikilizano ili kufikia muafaka wa matatizo yetu kwa mazungumzo,” alisema Makamu wa Rais huku akiwa hasikiki vizuri kutokana na kelele kutawala umati huo.

“Nimekuja kuwapeni pole ya kuunguliwa moto soko lenu na pia kuwapongezeni kwa kutafuta riziki zenu kwa uhalali,” alisema Dk Bilal.

Pamoja na kuzungumza kwa upole na kuwataka wananchi hao kutulia, alipingwa vikali na umati huo huku ukimtaka, ampishe Mbunge Silinde ili azungumze nao, ombi ambalo lilikubaliwa na Dk Bilal.

Silinde aliwaomba wananchi hao wawe watulivu ili wamsikilize Makamu wa Rais ambaye amefika hapo kama kiongozi wa Serikali na kwamba ni mgeni wa wananchi wote bila kujali chama.

“Nawaomba mtulie kama nilivyowaomba awali na pia naomba muwaruhusu watani zetu CCM ili nao wasikilize mkutano wa Makamu wa Rais,” aliongeza Silinde na kufanikiwa kutuliza umati huo.

Katika hotuba yake, Silinde alimwambia Dk Bilal kuwa wananchi wa Tunduma wana utaratibu wa kuhoji masuala mbalimbali yanayofanywa na viongozi wa Serikali na sio kwamba wanafanya fujo.

Alitoa mfano kuwa, hivi karibuni wananchi hao walihoji kitendo cha Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha kuhudhuria Sherehe za Miaka 35 ya CCM mkoani hapa huku akitumia magari ya Serikali.

Alisema hoja hiyo sio fujo bali ni kutaka kufahamu utaratibu mzima wa matumizi ya magari ya Serikali katika shughuli za kichama.

Alisema kuwa tukio lililowaudhi wananchi hao hadi kufikia hatua ya kupiga kelele katika ufunguzi wa soko hilo, ni kuondolewa kwa bendera ya Chadema saa chache kabla ya Dk Bila hajafika eneo hilo.

Mbunge huyo baada ya kumaliza kuzungumza, alimwomba Dk Bilal amruhusu Diwani wa Kata ya Tunduma, Frank Mwakajoka (Chadema) naye awasalimie wananchi, ombi ambalo lilikubaliwa na Dk Bilal.

Hali yawa shwari

Baada ya Silinde na Mwakajoka kuzungumza wananchi hao, walionekana kuridhika na kutulia na kumfanya Makamu wa Rais kuendelea na hotuba yake ambapo alianza kwa kuwataka kuheshimu utaifa wao, ikiwa ni pamoja na kumaliza matatizo yao kwa njia ya mazungumzo na si vinginevyo.

“Tutashirikiana na wote walio tayari kuonyesha ushirikiano na kuheshimiana na tukikuza uhusiano wetu kwa kusikilizana, tutaonyesha Utanzania wetu,” Alisema kwa kifupi na kumaliza hotuba yake.

Kabla ya Dk Bila kuwasili

Hali ya kuwapo vurugu katika mji huo, ilijionesha tangu asubuhi ambapo ilidaiwa kuwa chanzo chake ni kitendo cha Jeshi la Polisi kushusha bendera za vyama vya siasa katika eneo ambalo lilitarajiwa kufanyika mkutano huo.

Mmoja wa aliyeonja chungu ya ghasia hizo ni Katibu wa CCM Wilaya ya Mbozi, Lucy Mfupe ambaye licha ya gari alilokuwa akisafiria aina ya Toyota Prado kupigwa mawe, alivamiwa na vijana waliokuwepo eneo hilo kabla ya kuokolewa na walinzi wa CCM.

Mwingine ni Mwenyekiti wa CCM Tunduma, Danny Mwashiuya na Katibu wake ambao gari walilokuwa wamepanda, lilipigwa mawe na kuharibiwa vibaya.

Hilo ni tukio la tatu kwa viongozi wa kitaifa kufanyiwa fujo katika eneo hilo.

Hali kama hiyo ilishawahi kuwakuta Rais Jakaya Kikwete na mke wake Mama Salma pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani Nahodha.

Pia mwaka 2009 Mwenge wa Uhuru ulilazimika kubadili njia kutokana na wananchi wa eneo hilo kupanga kupopoa mawe msafara wake.


WAFUASI WA CHADEMA MJINI TUNDUMA MKOANI MBEYA WAKISHANGILIA HOTUBA YA MAKAMU WA RAIS KWA KUONESHA ALAMA YA VIDOLE