Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Wednesday, February 29, 2012

JK: Hatutaki Rais mzee 2015


na Nasra Abdallah
WAKATI makundi ya urais yakijipanga kuwania kiti hicho mwaka 2015, bila kuyajali, Rais Jakaya Kikwete amesema wanaota urais wakiwa na umri kama wake, wasahau, Tanzania Daima Jumatano limedokezwa.
Kikwete alitoa kauli hiyo wakati wa kikao cha Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kilichokutana juzi, pamoja na mambo mengine, kupitisha jina la mgombea ubunge katika jimbo la Arumeru Mashariki.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zilisema kuwa Rais Kikwete alitoa kauli hiyo wakati akifungua kikao hicho.
Kwa mujibu wa habari hizo, Rais Kikwete alisema kuwa kinachotokea Arumeru Mashariki ni makundi yanayotaka urais na kusisitiza kuwa kama kuna mtu mwenye umri kama wake na anataka urais mwaka 2015, asahau kupata kiti hicho.
Alisisitiza kuwa wanaotajwa kutaka urais wakiwa na umri kama wake na hata kuzidi, huu si wakati wao bali wa vijana.
Mtoa habari wetu kutoka ndani ya kikao hicho, alisema kauli hiyo ya Rais Kikwete iliwanyong’onyeza baadhi ya makada wanaotajwa kutaka nafasi hiyo wakiwa tayari na umri mkubwa.
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Bombuli, Januari Makamba (CCM), amependekeza kuwa umri wa kugombea urais, ushushwe kutoka miaka 40 ya sasa hadi 35.
Ushauri huo uliungwa mkono pia na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, ambaye alihoji kuwa kama Uganda wameweza kwa nini Tanzania mabadiliko hayo hayawezekani.
Makamba alitoa kauli hiyo jana katika kongamano la Femina HIP la vijana walio nje ya shule, lilioandaliwa na Jukwaa la Femina, huku likiwa limebeba mada kuu ya ushiriki wa vijana katika uundwaji wa Katiba mpya na kufanyika katika Ukumbi wa British Council, jijini Dar es Salaam.
Wabunge hao wawili pia walitaka umri wa mtu kuruhusiwa kupiga kura uwe miaka 16 badala ya 18 kama ilivyo sasa.
Akifafanua pendekezo hilo, Makamba alisema Tanzania inapaswa kuiga mfano wa nchi jirani kama Uganda, Burundi na Rwanda ambao tayari wanafuata mfumo huo.
Alisema asilimia kubwa ya wananchi wa taifa hili ni vijana hivyo haoni ni kwa nini hawapewi fursa kugombea nafasi hiyo kwa kisingizio cha umri.
Kuhusu kupiga kura, mbunge huyo alisema anaamini kwamba umri wa miaka 16 alionao kijana wa karne hii ana uwezo wa kuchambua mambo na kumchagua kiongozi anayeona anafaa.
Kwa upande wake Zitto alisema hata yeye anaunga mkono hoja hiyo na kudai kwamba linawezekana kabisa huku akitolea mfano kwamba kipindi cha nyuma wanawake walikuwa hawashiriki katika kupiga kura.
Kama vile haitoshi alisema miaka ya kupiga kura ilikuwa ni kuanzia 21 lakini kadri muda ulivyozidi kwenda na kuonekana kwamba kuna haja ya sheria hiyo kufanyiwa marekebisho, ndipo ikafika miaka 18 hivyo ni wakati sasa muafaka kwa vijana kudai haki hiyo ya kupiga kura wakiwa na miaka 16.
Hata hivyo Zitto aliwataka vijana katika mchakato huu wa Katiba kutokubali mjadala huo utawaliwe na wanasiasa kwa kuwa wengi wanajadili kwa maslahi yao.
Kwa mujibu wa Zitto tayari ameshaona wanasiasa hao wameanza kuutumia mjadala huo kwa manufaa yao huku wakilenga katika kugawana madaraka na kuacha kujadili mambo muhimu kama ajira kwa vijana na namna gani wataweza kulipwa kutokana na kazi wanazozifanya.
Pia mbunge huyo aliwaonya vijana wasije wakafikiri Katiba mpya ndiyo itakuwa suluhu ya matatizo yanayowakabili na badala yake kuwataka wafanye kazi kwa bidii.
“Msidhani kwamba eti Katiba mpya ikiwepo ndipo matatizo ya ajira yatakwisha au uibwaji wa rasilimali za nchi utaisha la hasha kwani matatizo haya yanaweza kuendelea kuwepo; kinachotakiwa ni kuchapa kazi na kujenga hoja pale mambo wanapoyaona yanaenda sivyo,” alisema.
Hata hivyo wabunge hao walipoulizwa swali na mmoja wa washiriki wa kongamano hilo, Humphrey Polepole, kama wangependa kuwa kwenye Bunge Maalum la Katiba, walisema ndiyo kwa madai kwamba wanaamini watakuwa na mchango mkubwa kuwepo kwao katika tume hiyo.
Kwa pamoja wabunge hao walisema kwamba wanataka kuonyesha siasa za tofauti katika kuondoa matatizo ya vijana na wananchi kwa jumla bila kujali vyama wanavyotoka.
Katika kongamano hilo la siku mbili ambapo mgeni rasmi alikuwa Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa, linalenga kupata maoni ya vijana wa Tanzania kuhusu Katiba mpya kwani takwimu zinaonyesha kwamba Tanzania ina watu milioni 44 na kati ya hao asilimia 65 ni watu walio chini ya umri wa miaka 25.


Source: Tanzania Daima. 29/Feb/2012

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.