Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Monday, February 27, 2012

CCM yataka kumtosa mtoto wa Sumari Arumeru

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye



Gazeti la Mwananchi 
 NI MAPENDEKEZO YA SEKRETARIETI YAKE, HATIMA YAKE NI LEO KWA KAMATI KUU, BUNDI AINYEMELEA CHADEMA
Fredy Azzah,     Moses Mashala, Arusha
MCHAKATO wa kumpata mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM katika uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki umefikia katika wakati mgumu baada ya Sekretarieti ya chama hicho taifa kupendekeza mshindi wa kura za jimbo, Sioi Sumari atoswe kwa madai kwamba uraia wake una utata.

Sekretarieti ya CCM ilikutana Dar es Salaam jana na mapendekezo yake yamewasilishwa kwa Kamati Kuu (CC) ya chama hicho inayoketi leo kutoa uamuzi wa mwisho kuhusu nani atapewa jukumu la kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Aprili Mosi.

Taarifa kutoka ndani ya kikao  hicho cha sekretarieti, zilisema uamuzi huo ulikuwa na sababu kuu mbili, utata wa uraia wa Sioi na kutoungwa kwake mkono na wagombea wenzake aliowashinda katika kura za jimbo... “Wanasema kwamba, Sioi ana elimu nzuri lakini uraia wake una utata.”

Mkutano Mkuu wa jimbo hilo uliofanyika Februari 20 ulimchagua Sioi, mtoto wa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo marehemu Jeremiah Sumari kwa kura 361, akifuatiwa na William Sarakikya aliyepata kura 259, Elishilia Kaaya (176), Elirehema Kaaya (205), Anthony Musari (22) na Moses Urio (11).
Ilidaiwa kwamba Sioi alizaliwa Kenya, hivyo kama akisimamishwa anaweza kukifanya chama kikawekewa pingamizi mbele ya safari.

“Kwa hiyo, hoja ni kwamba kama alizaliwa Kenya je, uraia wake ni wa kujiandikisha au kuzaliwa? Ndiyo maana, hata katika fomu ya uchaguzi ambayo ilikuwa na maswali mawili kama ni raia wa kuzaliwa au kujiandikisha, hakujaza hata moja,” kilisema chanzo hicho.

Imedaiwa pia kwamba Sioi amekuwa mjanja kukataa kujaza vipengele hivyo viwili kwani labda kama kungekuwa na cha tatu ambacho ni uraia wa kurithi.

Kutokana na sababu hiyo na ile ya kutoungwa mkono na wagombea wenzake aliowabwaga, chanzo hicho kilisema Sekretarieti imempendekeza Sarakikya ambaye alikuwa mshindi wa pili apeperushe bendera ya chama katika uchaguzi huo kwani anaungwa mkono na wagombea wengine.
Imeelezwa kwamba Sioi ameitwa mbele ya CC leo  ili kuwasilisha vielelezo vyake kuhusu uraia wake kabla ya kamati hiyo kufanya uamuzi.

Nape anena
Alipoulizwa juu ya taarifa hizo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema uamuzi wa mwisho kuhusu nani atagombea kwa tiketi ya chama hicho utatolewa leo na CC.
“Hata kama imetoa (Sekretarieti) mapendekezo kwa utendaji kazi wangu siwezi kulizungumzia. Kama nitazungumzia pendekezo maana yake nitakuwa nimezungumzia uamuzi. Mimi nazungumzia uamuzi wa chama ambao utatolewa na CC leo,” alisema.

Alisema anajua kuwa wapo wanaoeneza taarifa hizo wakidhani kuwa wanaweza kukifanya chama kikaacha kufanya uamuzi wake.

“Kamati Kuu itakaa kesho (leo) hapa Dar es Salaam kuanzia saa 4:00 asubuhi, ndiyo itapitisha jina la mgombea wetu na kupanga mikakati mingine ya ushindi,” alisema Nape.

Bundi Chadema
Kwa upande wake, mgogoro mkubwa unakinyemelea Chadema wilayani Arumeru baada ya baadhi ya wanachama na wagombea waliochukua fomu za kuomba nafasi ya kupeperusha bendera ya chama hicho, kupinga kitendo cha mgombea mwenzao, Joshua Nassari kuitisha harambee na kuchangisha fedha kwa ajili uchaguzi huo wakati chama bado hakijapitisha jina la mgombea.

Hivi karibuni, Nassari aliitisha harambee ya kuchangisha fedha mjini Arusha ikielezwa kwamba alifanikiwa kuchangiwa takriban Sh10 milioni na magari manane ili kumsaidia katika harakati za kuwania ubunge wa jimbo hilo. Zaidi ya makada 50 walishiriki katika harambee hiyo iliyohudhuriwa na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.

Hadi sasa wafuasi wa Chadema waliochukua fomu mbali ya Nassari ni Goodlove Temba, Yohane Kimuto, Rebbeca Mugwisha, Samwel Shami Sanjari na Anna Mgwilla.

Mchakato wa kuchukua fomu za kuwania ubunge ndani ya chama hicho umefungwa juzi na jina la mgombea atayapeperusha bendera ya chama hicho linatarajiwa kujulikana Machi 3, mwaka huu baada ya kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwa masharti ya kutotajwa majina, baadhi ya wagombea hao walisema wanasikitishwa na kitendo kilichofanywa na mgombea mwenzao kuitisha harambee ya kuchagisha fedha za kuwania jimbo hilo wakati bado hajapitishwa na chama. 

Walipinga kitendo hicho na kusema kimekiuka taratibu za chama hicho kwa kuwa hadi sasa uongozi haujapitisha jina la mgombea yeyote.

Nasari hakupatikna jana kuzunguamzia malalamiko hayo ya wagombea wenzake lakini Katibu wa Chadema Wilaya ya Arumeru, Totinan Ndonde alisema uongozi ulipata taarifa juu ya tukio hilo lakini, bado haujapokea malalamiko yoyote.

Alisema awali chama chao kiliwaita wagombea wote na kuwakumbusha juu ya taratibu na kanuni wanazopaswa kuzifuata lakini alisisitiza kwamba si kosa kwa mgombea kukutana na marafiki zake kuchangisha fedha katika harambee kwa kuwa ni suala la mtu binafsi.

       

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.