Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Sunday, February 26, 2012

Slaa amuonya Kikwete

•  Asema akipuuza nchi haitatawalika

na Charles Misango

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amemtaka Rais Jakaya Kikwete kuwa makini na kuchukua hatua za haraka kurejesha amani kabla Watanzania hawajaishiwa uvumilivu na utawala wa serikali yake.
Dk. Slaa amesema kuongezeka kwa matukio ya matumizi ya nguvu ya dola katika kulinda uhalali wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kiasi cha kufikia hatua ya kuua watu wasiokuwa na hatia, yanadhihirisha kuwa muda si mrefu ujao nchi itakuwa haitawaliki tena ikiwa Kikwete ataendelea kufumbia macho mauaji hayo.
Akifungua Ofisi ya Baraza la Vijana wa chama hicho (Bavicha) Mtaa wa Togo, Dar es Salaam jana, Dk. Slaa alisema kuwa mauaji yanayofanywa na vyombo vya dola chini ya serikali ya CCM kupitia kwa viongozi wake hususan Jeshi la Polisi, hayawezi kuvumilika tena na yanawasukuma wananchi kufikia mwisho wa uvumilivu.
Alisema sasa kuna dalili zote za wazi zinazotishia amani na mustakabali wa nchi na watu wake, zikiifanya nchi isitawalike, na wala serikali haiwezi tena kukwepa lawama za kuhusika na mauaji ya wananchi, na kutolea mfano wa tukio la kutwangwa risasi kwa watu wanne wasiokuwa na hatia waliokuwa wakiandamana kudai haki ya kulindwa na serikali yao mkoani Ruvuma mapema wiki hii.
Dk. Slaa akizungumza kwa uchungu alisema mauaji ya Songea yalitokana na uzembe wa hali ya juu wa viongozi wa serikali na vyombo vya dola ngazi ya wilaya na Mkoa wa Ruvuma.
“Napenda kutoa kauli juu ya mauaji dhidi ya raia yaliyofanywa na Jeshi la Polisi huko Songea. Kwa taarifa nilizonazo, mauaji yale yametokea kwa sababu ya uzembe wa hali ya juu na ufinyu tu wa akili ya viongozi, akiwamo mkuu wa Mkoa na polisi wale. Hivi unawaambiaje raia wenye uchungu na vifo vya wananchi wenzao, waliojikusanya na kuamua kuandamana kudai haki, eti wachague kiongozi wa kuonana na mkuu wa mkoa,” alisema.
Aliitaka serikali kuunda tume huru ya kuchunguza mauaji hayo ya Songea na kudai kuwa hakuna uhalali wowote wa viongozi wa serikali wa mkoa ambao ni watuhumiwa wa mauaji hayo kuunda chombo cha kuchunguza.
“Tunawapongeza wananchi na hasa vijana wa Songea kwa kuandamana kudai haki. Tunataka ufanyike uchunguzi huru juu ya mauaji hayo, yatakayoihusisha mahakama (Korona) na mkuu wa mkoa na polisi hawana uhalali wa kuunda tume za kuchunguza kwani wao pia ni watuhumiwa katika tukio hilo,” alisema.
Katibu mkuu huyo wa CHADEMA alilaani tukio la juzi usiku, ambapo polisi katika mji wa Tunduma wanadaiwa kushusha bendera za chama hicho katika maeneo mbalimbali ya mji huo.
Alisema kitendo hicho ni uchokozi tosha kwa CHADEMA na kimelenga kuleta fujo nyingine zinazoweza kuleta uvunjifu wa amani.
“Niliwasiliana na Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, pia mkuu wa mkoa, niliwaambia mimi sipendi kugombana nao kwa masuala ya hovyo kama hayo, tupo kwa mujibu wa sheria, bendera zetu zinatokana na kodi za Watanzania, wakasema eti zingine ziko sokoni, nikawauliza za CCM huwa zinawekwa wapi?
“Watu hawana maji, hawana zahanati, elimu inashuka, mkuu wa wilaya hajawahi kuamuka usiku, lakini kwenye kushusha bendera za CHADEMA wanaamka usiku wa manane,” alisema.
Alitumia wasaa huo kuwataka vijana wa CHADEMA wasimamie haki na kupinga dhuluma na uonevu popote pale wanapofanyiwa Watanzania na wahakikishe wanajua kinachoendelea katika maeneo ya Songea na Tunduma ili chama hicho kijue hatua za kuchukua.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bavicha, John Heche, mbali ya kumshukuru Dk. Slaa na makao makuu ya chama hicho kwa kuwawezesha kuwa na ofisi yao, alisema kuwa watakuwa mstari wa mbele kusimamia malengo ya chama hicho hasa katika kutetea haki za Watanzania, kudai uwajibikaji wa viongozi na serikali kwa wananchi, pia kulinda rasilimali za taifa.
Alisema kuwa vijana watakuwa mstari wa mbele katika vuguvugu la mageuzi yanayoendelea nchini, akisema kuwa ofisi hiyo itakuwa sehemu sahihi ya kuendeshea mipango ya ukombozi wa taifa ambalo pamoja na utajiri wa rasilimali za kila aina, bado wananchi wake wanaishi katika umaskini wa kupindukia.


                Tanzania daima

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.