Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Monday, February 27, 2012

Wanachama 136 wajiengua CUF                                                Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed
 
Mzimu wa kufukuzwa uanachama kwa Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed, na wenzake 10, umezidi kukiandama Chama cha Wananchi (CUF), baada ya wanachama wake 136, mkoani Tanga, akiwamo aliyegombea ubunge Jimbo la Korogwe Vijijini katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 na 2010, Mohammed Salim Siu, kujitoa katika chama hicho.
Habari zilizolifikia NIPASHE jijini Dar es Salaam kutoka Tanga zinaeleza kuwa Siu na wenzake walifikia uamuzi huo baada ya kurejesha kadi za CUF katika mkutano na waandishi wa habari, uliofanyika katika jengo la Makorora Community Centre, mjini humo jana.
Uamuzi huo ulifikiwa na Siu na wenzake kwa sababu mbalimbali, ikiwamo kile walichodai kuwa ni kuchoshwa na migogoro ndani ya chama isiyokuwa na ufumbuzi wa busara kiasi cha kusababisha wanachama kukikimbia chama kutokana na maamuzi yasiyoheshimu mawazo ya wanachama.
Sababu nyingine zimetajwa kuwa ni vitendo vya kufukuzana katika chama kwa shinikizo la Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad, bila sababu za msingi pamoja na ukimya wa Mwenyekiti Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba, juu ya mgogoro mkubwa uliopo ambao haujawahi kutokea katika chama.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Siu alisema sababu nyingine iliyowafanya wafikie uamuzi huo, ni kushuka kwa kiasi kikubwa kwa utendaji na mvuto wa shughuli za chama.
Alisema sababu nyingine ni kutokuwapo kwa haiba ya chama, kukithiri uzembe kwa viongozi, ubabe na matusi kwa wanachama na kuwavunjia heshima waasisi wa chama.
Sababu nyingine alisema ni matumizi mabaya ya fedha za chama, kutowekwa wazi mapato ya chama, wanachama kutoambiwa kiasi cha fedha kilichomo kwenye akaunti za fedha za kigeni na nje ya nchi .“Anayejua ni Katibu Mkuu peke yake,” alisema Siu.
Alisema sababu nyingine ni ubadhirifu wa mali za chama na upendeleo wa wazi kati ya Tanzania Bara na Zanzibar katika mgawo wa fedha.
Siu alisema sababu nyingine iliyowafanya kuihama CUF inatokana na kiapo cha Maalim Seif kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
Alisema katika kiapo hicho, Maalim Seif aliapa kwamba, atailinda Katiba ya Zanzibar, kutokutoa siri za SMZ, kumtii Raisi wa Zanzibar.
Siu alisema kwa viapo hivyo, ni dhahiri kuwa Maalim Seif kamwe hawezi kufanya kazi ya CUF yenye dhana ya kutetea demokrasia na haki kwa Watanzania.
“Ndio maana akaambiwa wasipeleke mgombea ubunge Arumeru Mashariki ili CCM ishinde kirahisi na kuambiwa wasiunge mkono chama chochote cha upinzani,” alisema Siu.
Aliongeza: “Hizi ni dalili kuwa CUF haipo tena katika ushindani wa vyama vyenye nia ya kuwakomboa Watanzania na kwa mantiki hiyo ni wazi CUF ni kibaraka wa CCM na ndio maana wameisaidia CCM ishinde katika Jimbo la Uzini Zanzibar.”
“Nimetafakari kwa kina sana juu ya mwenendo wa chama chetu cha CUF na hatma yake hasa baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. Chama chetu chini ya Mwenyekiti na Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad wameshindwa kutoa dira ya chama, tumetoka wapi, tuko wapi na tunakwenda wapi,” alisema Siu.
Alisema mbali na hilo, chama kimeshindwa hata kutoa mkono wa pole kwa wagombea wake wa nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo wa 2010 na kwamba hali hiyo imewakatisha tamaa wagombea na imeonyesha CUF haijali wagombea wake japo walifanya kampeni kama wagombea binafsi.
“Hii inaonyesha kuwa chama kimekosa malengo na muelekeo,” alisema Siu na kuitaja sababu nyingine iliyowafanya kufikia uamuzi wa kujitoa CUF, ni ubaguzi wa Maalim Seif miongoni mwa wanachama wa Tanzania Bara na Zanzibar.
Alidai wengi walioajiriwa katika CUF ni Wazanzibari, huku Ofisi Kuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam, ikiwa ina wanachama kutoka makabila mengine. Siu alidai makao makuu ya chama Zanzibar hakuna ofisi ya mwenyekiti wakati Tanzania Bara kuna ofisi ya Katibu Mkuu na ya Makamu Mwenyekiti.
Aliongeza: “Kwa sababu hizo hapo juu, kuanzia sasa mimi si mwanachama wa CUF kwa sababu ya kauli mbiu ya 'CUF ni kwa ajili ya Seif Sharif Hamad' na sio kwa ajili ya Watanzania.”
Alinukuuu kauli ya Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Ismail Jussa Ladhu, aliyokaririwa na kituo kimoja cha televisheni nchini kwamba, kushindwa kwa CUF katika uchaguzi mdogo wa uwakilishi katika Jimbo la Uzini, hivi karibuni, kulitokana na Wabara na Wakristo wanaoishi jimboni humo.
“Kauli hiyo hakuna kiongozi wa CUF aliyeikanusha. Hivyo, maneno hayo ya Jussa ni ya CUF. Nawaomba Watanzania wazinduke na kujitoa CUF sababu ni chama cha kibaguzi,” alisema Siu.
Naye Abdallah Salim (Daiyadaiya) aliyejitambulisha kuwa ni muasisi wa CUF Tanga, akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu kutoka Tanga jana, alidai Maalim Seif alitumia Sh. milioni 500 alipogombea urais Zanzibar wakati Profesa Lipumba aliyewania kiti hicho katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alipewa Sh. miloni 70 tu kuzunguka nchi nzima.
Alisema CUF imekosa mwelekeo kwa sasa na ndiyo maana hata uchaguzi mdogo wa mwakilishi Jimbo la Uzini imeshindwa kushika nafasi ya pili na kuzidiwa na Chadema.
Hata hivyo, wanachama hao ambao hawakueleza wanakusudia kujiunga na chama gani, badala yake walisisitiza kuwa kuondoka kwao CUF ni mwanzo wa kukiua chama hicho mkoani humo kwani tayari kuna wanachama wengine kutoka matawi mbalimbali wameahidi kuwafuata.
Katibu wa CUF Wilaya ya Tanga, Mohammed Haniu, alipotafutwa na NIPASHE kuzunfumzia uamuzi huo wa wanachama wa chama chake, hakupatikana na hadi tunakwenda mitamboni, simu yake ya mkononi ilikuwa imezimwa.
Hata hivyo, Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Wanawake wa CUF Taifa, ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi wa CUF Taifa, Nuru Bafadhili, alisema tuhumza nyingi zilizotolewa na wanachama hao hazina ukweli bali zina lengo la kumpaka matope Maalim Seif.
Alisema si kweli kwamba kwenye kampeni ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 Profesa Lipumba alipewa Sh. milioni 70 tu na kusema kiasi hicho cha fedha kilichotajwa hakijafikia hata fedha zilizotumika kwa kuweka mafuta magari mawili tu ya kampeni kwa aliyekuwa mgombea urais na mgombea mwenza na kukanusha madai kuwa Maalim Seif anaendesha CUF kisultani.
Alisema shughuli nyingi za CUF hufanywa na watendaji walio chini yake ambao kwa sasa wametawanywa nchi nzima kukiimarisha chama.
“Tuna taarifa zote kuwa Hamad Rashid ametuma watu wake hapa Tanga ili kupata watakaokidhamini chama chake mara muda utakapofika. Kama anafanya hivyo afanye kwa salama, lakini si kuwapaka matope wengine kwani tunayajua mengi ya kwake,” alisema Bafadhili.
Alisema wengi waliojinadi kwamba ni waasisi wa CUF si kweli kwani hawamo kwenye orodha ya waliokiasisi na akatolea mfano wa Daiyadaiya kwamba alishatangaza kujiondoa CUF jijini Dar es Salaam kipindi kirefu, hivyo anashangaa kusikia akitangaza tena kufanya hivyo.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.