Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Monday, February 27, 2012

CUF Chazidi kumeguka


Aziza Masoud
CHAMA cha Wananchi (CUF) kimezidi kubomoka baada ya aliyekuwa Meneja wa Kampeni wa mgombea urais wa chama hicho Profesa Ibrahim Lipumba kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2010,  Said Miraji kutangaza kujitoa kwenye chama hicho huku akisema yeye na wenzake leo wanatangaza kuanzisha chama kipya.

Upepo wa kisiasa umekuwa ukivuma vibaya ndani CUF tangu kupitishwa kwa uamuzi wa Baraza Kuu wa kumfuza uanachama Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed na makada wenzake wa tatu ambao ni wajumbe wa chombo hicho cha juu cha uamuzi.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Miraji ambaye pia aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Usalama wa CUF,  alisema alishawahi kumwandikia barua Profesa Lipumba miaka sita iliyopita akimtaka awashauri viongozi wa juu warekebishe mwenendo wao wa kuendesha chama kabla watu hawajaanza kukihama.

“Leo, katika maisha yangu naandika historia kwa kujiondoa uanachama katika chama ambacho niliweka rehani roho yangu kwa ajili ya kutetea wanyonge. Chama ambacho niliamini kwamba kinasimamia haki za wananchi,” alisema Miraji akiwa na aliyekuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Temeke mwaka 2010, Badau  Limbu ambaye naye amejitoa CUF.

Miraji alisema kutokana na kufa kwa chama hicho, wamejipanga kusajili chama kipya ambacho maombi ya kuanzishwa kwake  yatawasilishwa leo kwenye Ofisi ya Msajili wa Vyama Siasa.
Alisema mambo yanayotokea ndani ya CUF hayatokei kwa bahati mbaya bali, yamepangwa na viongozi kwa nia ya kukidhoofisha chama hicho upande wa bara.

“Mimi niliona mwelekeo chama hiki tangu awali ndiyo maana nilijiweka pembeni kwa muda na kuamua kuwa mjasiriamali kwani sikutaka kuiona CUF ikibomoka mbele yangu lakini leo malengo ya viongozi kukibomoa chama yametimia kwa kuanza kuwafukuza watu uanachama,” alisema Miraji.

Alisema Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad akiwa mwanzilishi wa chama hicho, ndiye anayeongoza kukibomoa akidai kinaendeshwa bila kanuni za uendeshaji na badala yake kina kanuni za uchaguzi tu.
Alidai kuwa mwingine aliyeingia katika chama hicho kwa ajili ya kukibomoa ni Naibu Katibu Mkuu Bara, Julius Mtatiro: “Mkataba aliouingia Mtatiro wa kukibomoa chama umefanikiwa lakini, kafanikiwa kwa kuwa wenye CUF hawakuwepo kama tungekuwepo sisi kwenye uongozi asingekaa. Njama zake zitaishia kukiua chama, lakini hawezi kuwaua watu kisiasa.”

Akizungumzia kauli iliyotolewa na chama hicho ya kujitoa katika uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki, Miraji alisema kushika namba tatu katika uchaguzi uliopita si kigezo cha kutomsimamisha mgombea katika jimbo hilo.
“Hivi kama Arumeru Mashariki kwa kuwa tulishika nafasi ya tatu ndiyo tusisimamishe mgombea kwa kuhofia kupoteza pesa? Mbona katika kiti cha urais mwaka 2010 Profesa Lipumba naye alishika nafasi ya tatu je, uchaguzi wa  mwaka 2015 nao hatagombea urais kwa kuogopa gharama?”

Kwa upande wake, Limbu alisema ameamua kujiondoa katika chama hicho kwa kuwa kimepoteza mwelekeo wa kisiasa... “Nilijiunga CUF mwaka 2007 kwa kuwa kilikuwa chama makini na chenye msimamo kwa kipindi hicho lakini kwa sasa kimepoteza mwelekeo na hakipo kwenye msingi wa awali. Siasa siyo kabila kwamba huwezi kubadilisha.”
Alidai kuwa CUF kimejaa ubaguzi wa Ubara na Uzanzibari na kwamba uchaguzi mdogo wa Igunga ulikuwa ishara tosha kuwa chama chicho kimekufa kisiasa.

Alisema  kama viongozi watataka kuwashawishi wanachama waliojiondoa warudi tena, watapaswa watoke wao kwanza ili chama kiwe safi.

Jinamizi CUF
Januari 4, mwaka huu Kikao cha Uongozi cha Baraza Kuu la CUF kilichofanyika Zanzibar, kiliwafukuza uanachama Hamad na wenzake Doyo Hassan Doyo, Shoka Hamis Juma na Juma Saanani kwa madai ya kwenda kinyume na taratibu za chama hicho.

Awali, kabla ya uamuzi huo kulikuwa na mvutano uliotokana  Hamad Rashid kufanya mikutano ya ndani katika matawi mbalimbali iliyokuwa na nia ya kukiimarisha.
Lakini mikutano hiyo iligubikwa na vurugu hasa katika ule uliofanyika Tawi la Chechnya, Manzese Dar es Salaam ambako  wanachama  wanaomuunga mkono Hamad Rashid walipigana na walinzi wa Blue Guard waliotaka kuvunja mkutano huo.

Baada ya vuta nikuvute katika matawi na siasa za majibizano, ndipo kikao hicho cha Baraza Kuu kilipoamua kuwafukuza uanachama.

Msimamo wa CUF
Akijibu madai hayo ya Miraji, Mtatiro alisema: “Said Miraji ni mfuasi wa Hamad Rashid kwa muda mrefu sana. Amekuwa akikihujumu chama yeye na Hamad kuondoka kwake siyo tishio kwa CUF.”

“Nafahamu anakwenda kukabidhiwa chama cha Hamad Rashid kama kaimu mwenyekiti hadi Hamad atakappmaliza ubunge wake, tunamtakia kila la heri katika kujitoa CUF. CUF iko imara sana.”

Mtatiro alisema kama CCM ilishindwa kuiua CUF, Hamad Rashid na wenzake wachache hawataweza kamwe.

“Acha waunde chama chao halafu CCM wakishakata ufadhili wao ndiyo watajua kuwa siasa za kutumiwa zina hatari kubwa. Mimi niko mikoani, hali ya chama ni nzuri sana na namba ya watu watakaomfuata Hamad Rashid ni ndogo na kwa baadhi ya wilaya tu.”

Alisema Hamad na wenzake wataunda chama lakini kitakufa hivi karibuni... “Tunawakaribisha katika ulingo wa siasa.”

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.