Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Thursday, February 23, 2012

Upendo ni Dawa Ya Maisha


Dunia haiwezi kwenda bila upendo, maisha hayawezi kuwepo bila upendo. Upendo ni dawa ya maisha , maisha bila upendo hayana maana. Upendo ukitoweka mara nyingi hata sababu ya kuishi hufifia, wengi tunaishi sasa kwasababu ya upendo . Kila binadamu ana utofauti na upekee wake, na kiungo kikubwa kinachoweza kumuunganisha binadamu kwa binadamu mwingine ni upendo. Sisi sote ni zao la upendo,tumezaliwa kutokana na upendo na tunaishi kutokana na upendo na maisha yetu sisi sote yanaunganishwa na upendo.

Upendo una maana sana, na ni zaidi ya yale mambo tuliyoyazowea kuwa ndio upendo.
Neno upendo limezoweleka sana, kiasi kwamba linakosa maana na kutafsiriwa visivyo; ni mara ngapi umesikia wengi wakisema ‘Nakupenda’ lakini kwenye macho yao haionyeshi hivyo kabisa?

Upendo ni ukweli wa ndani ya moyo. Upendo ni msukumo wa ndani na si nje. Maana ya upendo huanza ndani ya mtu na kila mtu anao uzuri wa ndani uliobeba upendo ; hata kama mtu huyo anafanya mabaya kiasi gani, au hata kama anaonekana mbaya kimatendo – mimi naamini kabisa kuwa kila mmoja wetu anayo mazuri ndani mwake, mazuri yaliyobeba upendo.
Upendo ni hali ya mmoja kujitoa kwa faida ya ampendaye bila kudai fidia au malipo. Kwangu mimi: Upendo huvumilia, upendo hufadhili; upendo hauna wivu au majivuno.Upendo hauna kiburi na haukosi kuwa na adabu. Upendo hautafuti kujipendeza nafsi; haukasiriki upesi, hauweki orodha ya mabaya.Upendo haufurahii mabaya, bali hufurahia kweli.Upendo huvumilia yote, huamini yote, hutumaini yote, hustahimili yote.Upendo hauna mwisho.
Rafiki yangu, upendo ni zaidi ya zawadi ya maua au kuvaa nguo nyekundu katika siku ya wapendanao Upendo si kutafuta kujifurahisha na kujifaidisha tu, bali kumfaidisha na kumfurahisha umpendaye au uwapendao katika siku za maisha yako duniani. Upendo ni zaidi ya zawadi ya tendo la ndoa , Upendo ni muunganiko wa kutoka rohoni. Upendo si mkataba ili kutafuta kufaidika wewe na pindi usipopendwa au kufaidika au ukipunjwa kutokana na mkataba unavunjika . Upendo ni uhai wa maisha ya kila siku. Upendo ni muujiza wa ndani. Upendo ni mbegu ya furaha ya ndani.Upendo ni mwanga wa ndani unaoweza kuongoza hata katika giza totoro kiusahihi kwa kuangalia mazuri tu ya binadamu mwingine umpendaye. Upendo hutibu,huponya na husamehe. Upendo ni nguvu kubwa kuliko zote duniani. Upendo si kujisikia bali ni ukarimu, shukrani na tabasamu.Upendo ni furaha ya maisha. Upendo haupimwi bali hubakia katika moyo,imani,tarajio au hisia isiyoweza kuhesabika,kuzungumzika na hata kukisiwa.

Na safari ya upendo huanza ndani, kwa kujikubali mwenyewe,kujipenda na kupenda wengine bila sababu. Upendo ama mapenzi si maneno matamu ama ya kimahaba peke yake , bali Upendo ni vitendo kwa kujali,kuhudumia,kuwa muungwana na kustahimili. Kupenda si kutaka tu kuridhishwa peke yake hasa kwa wapenzi bali kutafuta njia za kumridhisha mwenzi wako bila kuchoka hata kama hukuridhishwi mpaka siku atakapojifunza, na hata asipojifunza bado yakupaa kuendelea kumridhisha. Upendo wa kweli haulipi kisasi kwa mabaya bali kwa wema pale tunapotendewa ubaya, na haukimbii kuwajibika bali hukubali makosa pindi tunapokosea pasipo kujali jinsia.

Nahitimisha kwa kusema: Kuishi duniani ni kutamu kama tukijua maana ya kupenda bila sababu au madai. Binadamu anayeamua kupenda kiukweli mara nyingi upendo humrudia.Na pia upendo hautolewi ama kupokelewa kwa siku moja tu; siku ya wapendanao(Valentine day) - bali maisha yetu ya kila siku yapaswa kuongozwa na upendo. Na ikumbukwe kuwa maisha yasiyounganishwa na moyo wa upendo, mara nyingi hukosa maana na. Uhai wa maisha ni upendo kwani upendo ni dawa ya maisha.

Tuamue leo basi kupandana kiukweli – tupendane sisi kwa sisi, tupendane mume kwa mke, tupendane wapenzi, tupendane familia, tupendane wandugu na tuamue leo kuipenda nchi yetu – ili tuone maajabu na malipo ya kupenda yatakavyoturudia hapa duniani. Asanteni sana. Na nawapenda sana.

Na Geophrey A. Tenganamba.
Mshauri wa maisha,mahusiano,mafanikio,biashara,masomo na ndoto za maisha.
Wasiliana nami kwa 0714477218
source:http://www.treasurehousewithinyou.blogspot.com/

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.