Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Tuesday, February 28, 2012

Kifo ndiyo tiba pekee kwa CCM

Na Joster Mwangulumbi 


WIKI iliyopita nilihitimisha makala yangu kwa kugusia kidogo juu ya sherehe za miaka 35 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Maadhmisho ya miaka 35 kwa vyovyote vile si haba, ni umri mrefu. Wengi tunaoifahamu CCM tangu kuzaliwa kwake Februari 5, 1977  ilizoeleka kuona shehere zake zikiwa na msisimko wa halaiki, gwaride la chipukizi, shamrashamra zilizopangwa na kupangika.
Nilisema wiki iliyopita kuwa vijana walioshiriki gwaride hasa chipukizi, walionekana kuwa wachovu mno, hawana matumaini, nyuso zao zilionyesha wazi, uchovu wa mwili na hata wa nia, kuchangamka hakukuwako hasa katika ule mtiririko na mambo ya kiitifaki ya magwaride.
Kilichoonekana ni juhudi za kutaka kucheza muziki wa kigeni, wa Afrika Kusini (Kwaito), lakini nao haukuwa na maanadalizi ya maana. Kimingi maandalizi yake hayakuakisi kiwango cha sherehe za kitaifa za chama kikongwe kama CCM.
Baadhi ya watu wanaweza kuamini kwamba mambo haya hayana maana kwa uhai wa chama cha siasa. Ikumbukwe CCM ilitumia mamilioni ya fedha kwa ajili ya kupika chakula cha wote waliohudhuria sherehe zile, ng’ombe wengi walichinjwa, ulaji ulikuwa mkubwa mno. Vyakula vingi.
Hakuna ubishi kwamba kwa mwafrika yeyote sherehe inakuwa na maana, kama inakuwa na vyakula, kwa hiyo si jambo la ajabu kwa CCM kutumia mamilioni kuandaa vyakula, inaeleweka.
Lakini wakati CCM ikiadhimisha miaka 35 ya uhai wake inakabiliwa na changamoto nyingi, kubwa kuliko zote ni kugeuka kutoka kuwa chama cha kuwakilisha wananchi wote hadi kuwa jumuiko la makundi yanayoahasimiana.
Kwa miaka takribani 15 sasa, CCM imekuwa chimbuko la makundi, chama cha makundi tena makundi yenye uhasama mbaya kiasi cha kuleta hofu ya kudhuriana kama vile matumizi ya sumu. Yapo na yamesemwa kwamba sumu sasa imekuwa utaratibu mpya ndani ya siasa za chama hiki.
Kwa sasa CCM ina kazi  kubwa mbili ambazo ilianzisha na zikashindikana kukamilika; hizi ni kujivua gamba na kutenganisha siasa na biashara. Kazi zote hizi mbili badala ya kukijenga chama hiki zimezidi kukichimbia shimo.
Ni katika utaratibu huo hata mapendekezo ambayo yanatolewa kwa ajili ya kufanya mageuzi ndani ya chama hicho yanaangaliwa tu katika sura hiyo, ni kundi lipi linalengwa. Kila kitu kinatazamwa katika sura ya makundi.
Kwa sasa chama kimetangaza mabadiliko ya kupatikana kwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), wabunge na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wameenguliwa kwa kuwa kinachotakiwa sasa ni kupata wajumbe ambao watafanya kazi hiyo kwa muda wote.
Kwamba nafasi hizo zinaongezwa kutoa wajumbe wa mikoa wa sasa kuwa wa wilaya. Kila wilaya itatoa mjumbe wa NEC, lakini wabunge na wawakilishi hawataruhusiwa kuwania. Maamuzi hayo yanalenga kuwaweka kufuli wabunge kwa kuwa sasa hawatakuwa na ubavu wa kutikisa ndani ya chama.
Kiutaratibu wabunge walikuwa wanaruhusiwa kuwania nafasi hizo, lakini si hilo tu hata wabunge wa CCM wana nafasi ya U-NEC inayotokana nao kama kundi la wabunge wa CCM. Hatua hizi mpya hata kwa ufafanuzi gani hazionyeshi ni kwa jinsi gani zinaimarisha chama, ila inazidisha nyufa miongoni mwao.
Inajulikana wazi, wajumbe wa NEC hawana mishahara, wanaishi tu kwa kuendesha shughuli zao, lakini uamuzi wa sasa wa kutaka wawe ni wa kufanya kazi wakati wote ni sawa na kusema sasa ajira mpya ndani ya chama imeibuliwa.
Hali hii inatokea wakati hata wenyeviti wa ngazi zote kuanzia tawi, kata, jimbo wilaya hadi mkoa hawana mshahara;  wanaishi tu kwa kutegemea vikao na miradi ya chama.
Wajumbe wapya wa NEC wa wilaya kwa vyovyote vile wanaongeza mzigo kwa chama ngazi ya wilaya. Wilayani maisha ya chama ni hoi, wanaotegemea chama ngazi hii wako hoi, vyanzo vya mapato ya maana ya chama katika ngazi hii ni matatizo.
Hata kwa wale wanaolipwa mashahara kama makatibu, kiukweli wanaishi kwa kubangaiza tu kwa kuwa ujira wao ni sawa na mzaha. Kwa hiyo chama kinafungua mlango mwingine wa kubeba mzigo ambao hakina mbavu nao.
Hata hivyo, wakati wabunge wakipigwa pingu hizo, mwenyekiti wa taifa ameachwa aogelee kwenye bahari ya madaraka makubwa akiyachanganya na yale ya urais. Hakuna pendekezo lolote la kutenganisha kofia ya mwenyekiti na urais kwa nia kama hiyo hiyo ya kuwaengua wabunge ili kupata fursa pana ya kutumikia na kujenga chama.
Kwa hiyo zengwe hili linasukwa ili kuwakata makali wabunge, lakini wakati huo huo likimjengea madaraka makubwa zaidi mwenyekiti.
Harakati za kujengea mwenyekiti madaraka halionekani kwenye nafasi za U-NEC tu kwa wabunge, bali hata kwa viongozi wastaafu. Wenyeviti wastaafu na makamu wao sasa nao wanaundiwa Baraza la Ushauri.
Kwa maneno mengine wameenguliwa katika vikao muhimu vya maamuzi kwani baraza hilo la ushauri halina nguvu ya kulazimisha ushauri wao uzingatiwe.
Hoja inayojengwa hapa ni kuwapunguzia wastaafu hawa kazi za kuhudhuria vikao vya kikatiba vya lazima vya chama; inawezekana nia ikaonekana haraka haraka kuwa ni hiyo, lakini ukweli ni mkakati wa kujiimarisha madarakani kwa mwenyekiti kwa sababu viongozi hao wakuu ndio watu pekee wanaothubutu kumwambia ukweli pale inapolazimu.
Nilianza kusema kuwa chipukizi walioonekana kule Mwanza walikuwa wamechoka, hawakuwa na uchangamfu wowote unaofanana na umri wao, hii ni kwa sababu, kwa miaka mingi idara ya chipukizi chini ya umoja wa vijana wa CCM imekufa – kifo hiki si cha bahati mbaya ni matokeo ya kupotea njia kwa chama katika mambo mengi.
Mojawapo ni hili la kushindwa kuandaa vitalu vyake.
Kazi kubwa kwa miaka 15 ndani ya chama hiki imekuwa mnyukano, na hata sasa inaendelea. Hali hii ndiyo inasababisha ushiriki na uchangamfu wa chipuki ndani ya chama hiki kuwa tatizo kubwa kama ilivyodhihirika Mwanza.
Kwa hiyo, tunapoiangalia CCM leo na kesho, si uchimvi kukibatiza chama hiki jina jipya la “chama cha makundi,” tena makundi ambayo yamekivuruga kwa kipindi kirefu kiasi kila jambo jipya linalopenyezwa ndani yake hakika haliangalii chama kama taasisi, bali linalenga kundi moja dhidi ya jingine. Mwenendo huo ndio unakipeka chama hiki katika hitimisho la uhai wake.
Wapo makada wa chama hiki kikongwe ambao tambo zao ni kwamba kitadumu madarakani kwa karne nyingi zijazo, lakini wamekosa ujasiri wa kuona kuwa kila hatua inayopigwa katika kujipanga upya inakuwa afadhali ya ilivyokuwa hapo kabla, mwendo ni kukimbilia kwenye kuangamia, hawasikii na wala hawaoni.
Na hata wale waungwana waliopewa vyeo ndani ya sekretariati nao pia hawalioni hili, hawajijui katika hali hii nini zaidi kitarajiwe kama si kuandaa matanga huko tuendako?

Mwanahalisi

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.