Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Saturday, February 25, 2012

RAY AMSHAURI KANUMBA

Na Mwandishi Wetu
STAA anayemiliki mkwanja mrefu katika tasnia ya filamu za Kibongo, Vincent Kigosi ‘Ray’, amemvaa ngwiji mwenzake Steven Charles  Kanumba na kumchana kwa kitendo cha kumlipua baba yake mzazi, mzee Charles Kusekwa, katika vyombo vya habari, Risasi Jumamosi lina mkanda mzima.
Akizungumza na gazeti hili, Ray ambaye inadaiwa ana bifu baridi na Kanumba, alisema kitendo alichokifanya mshkaji wake si cha kiungwana kwa kuwa aliyekuwa anamzungumzia ni baba yake mzazi.

HABARI KAMILI
Ray alisema, hata kama baba yake angekuwa amefanya kosa kubwa kiasi gani, kumuanika kwenye vyombo vya habari ni kumkosea adabu.
“Kiukweli pale Kanumba alikosea sana, huwezi kumsema mzazi wako. Baba ni Mungu wa duniani. Anatakiwa kuheshimiwa kwa namna yoyote,” alisema na kuongeza:
“Kwanza mzazi huwa hakosei...tunatumia uungwana kusema, anasahau! Hata kama alimkosea, tutasema alijisahau...halafu unapomsema mzazi wako kwenye vyombo vya habari unatarajia nini? Adharaulike au? Hakufanya sawa hata kidogo.”
NI LAANA
Akiendelea kutambaa na mistari, Ray alisema kitendo alichokifanya Kanumba ni sawa na kutafuta laana.
“Hata kama hatamlaani, lakini moja kwa moja ni laana. Huwezi kumkosesha amani mzazi wako kiasi kile. Nina uhakika Kanumba      hakuomba ushauri kabla ya kwenda kwenye runinga.
“Alikurupuka. Kama angezungumza na sisi wasanii wenzake, naamini hakuna ambaye angemkubalia. Tungemshauri vizuri tu. Hili ni kosa kubwa. Ni sawa na kumvua nguo mzazi wako,” alisema.
Akaongeza: “Mbaya zaidi, baba yake amejibu tuhuma zake kwenye gazeti, na yeye tena akamjibu. Inaonesha ni kwa namna gani anapenda mashindano na mzazi wake. Si kitu kizuri hata kidogo. Hapo Kanumba alichemka, lazima aelewe huo ukweli.
“Unajua kuna mambo mengine hayapaswi kujulikana na watu. Yeye kama msanii mkubwa, mwenye heshima, leo hii anaanika maisha yake ya utotoni? Eti baba alimtesa? Ili iweje? Amepata nini kwa kusema hayo kama siyo kumdhalilisha tu mzazi wake? Haikuwa sawa.
“Haya mambo wangeyajadili kifamilia ingekuwa na maana zaidi kuliko kuyaanika hadharani.”
AMTAKA AOMBE RADHI
Ray alisema, Kanumba akitaka aendelee kupaa katika anga la filamu, anatakiwa kumuomba lazi baba yake.
“Kitu pekee kilichobaki ni kumuomba baba yake msamaha. Amemkosea sana, amuombe amsamehe ili asibaki na kinyongo. Hiyo ndiyo njia pekee ya kumsafisha,” alisema na kuongeza:
“Nina imani atamsamehe na watafungua ukurasa mpya. Huu ni ushauri wangu. Ana uhuru wa kuufuata au kuuacha. Mzazi siku zote ana huruma na mwanaye, bila shaka atamsamehe.”
NI MWENDELEZO WA BIFU?
Alipoulizwa kuwa sababu ya kusema yote kwa Kanumba ni kwa kuwa ana bifu naye, Ray aliruka kimanga, akaeleza kuwa, amefanya hivyo kama msanii mwenzake na ni kwa nia njema.
“Sizungumzii mambo ya bifu hapa, naongelea usahihi wa alichokifanya. Naamini hata jamii haiwezi kuona eti kumshauri mtu ni bifu. Ni mawazo yangu, kama nilivyosema awali,” alisema.

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.