Mwanzo wa mwaka huja na mwamko mpya, mategemeo mapya, matumaini mapya, mipango na malengo mapya. Wengi wetu huanza kwa nguvu nyingi sana mwanzo wa mwaka, kwa sababu , mwanzo una mwamko wake. Lakini wote yatupasa kufahamu ukwelu kwamba; katika maisha, haijalishi umeanzaje au umetoka wapi bali umemalizaje.
1. Jifunze kutoka jana: Ingawa mambo ya jana yamepita lakini ni muhimu wewe kujifunza makosa yote uliyoyafanya jana,mfumo upi uliokufelisha jana na nini ufanye kuyarekebisha hayo sasa. Usilie kwa yaliyopita jana, bali weka mkazo kwa yale yatakayokuja sasa. Yaliyopita yamepita na huwezi kuyabadili ila ni faida kwako kwani waweza kujifunza kupitia hayo. Jana bado ipo kwa maisha yako ili upate faida ya kujifunza.Sema asante jana.
2. Jifunze kufurahia na kuishi leo: Maisha yako halisi yanaendelea leo, hivyo basi ishi leo, furahi leo, cheka leo, tafuta leo, jikubali leo. Hata kama unadhani mazingira yako ya leo hayajakaa poa, jifunze kuishi leo kwa ulichonacho leo huku macho yako yakiangalia na kujipanga kwa ajili ya kesho.
3 Jifunze kuangalia na kujipanga kwa ajili ya kesho: Katika maisha haijalishi upo katika hali gani au mazingira gani bali kule unakokwenda. Hata kama una hali ya aina gani, jifunze kuangalia mbele, kuwa na matumaini ya kesho. Kesho yako itaonekana tu ukiamua kuitengeneza katika akili na imani yako , na hata zaidi , kimatendo. Kumbuka kuwa macho yaliwekwa mbele ili kuangalia na kwenda mbele, jifunze kuangalia mbele, jifunze kuangalia kesho kwa matumaini na shauku kubwa zaidi kuanzia leo.
4. Amua kubadilika wewe kwanza: Badilika ili kufanya vizuri zaidi kile unachokifanya au kingine unachotaka kukijua, badilika ili utoe matokeo mazuri mwisho wa mwaka, amua kujiendeleza kwa kusoma vitabu vinavyoweza kukuendeleza na si kukupumbaza akili. Na ukumbuke kuwa ukitaka mabadiliko yoyote maishani badilika wewe kwanza.
5. Fanya malengo yako kuwa sehemu ya maisha yako ya kila siku: Kumbuka kuwa dunia hii imechanganyikiwa. Ni rahisi sana kubebwa kama takataka na pepo na ukaishia kuishi maisha ya wengine. Ni rahisi kupoteza ukweli wetu kuhusu sisi. Yapo mambo mengi yanayotufanya tupoteze muda wetu duniani na zaidi yanayoweza kutufanya tusiongee na mioyo yetu. Usipong’ang’ania kuishi malengo yako , usipousikiliza moyo wako dunia itakupoteza, kwani haina huruma kama usipoamua kujisimamia. Watu wengi wenye mafanikio kila siku, usiku na mchana wanahangaika kuyafikia malengo yao zaidi. Wanautumia muda wao wote kuyafikia malengo yao na hawachoki. Jifunze kila siku kufanya yale yatakayokufikisha katika malengo yako.
6. Usikate tamaa: Maisha yanachanganya, na mara nyingi huonekana kuwa magumu lakini inawezekana kabisa kufanikiwa; haswa ukijidhatiti kuyafikia unayoyataka. Fahamu kuwa, kuishi kwako duniani ni kwa muda tu,na ndoto yako na malengo yako ni kama sababu ya kuwepo kwako. NI UHAI WAKO. Hakuna kitu chochote kizuri duniani kinachopatikana bila kujitoa. Ukitaka cha kwako kifanikiwe na kutambulika, amua kujitoa mpAka kukipata na usikate tamaa njiani mpaka kipatikane. Tafadhali usikate tamaa, usikate tamaa.
No comments:
Post a Comment
Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.