Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Tuesday, February 28, 2012

WARAKA MAALUM KWA DR. MWAKYEMBE

NAKUTUMIA salamu zangu za pole popote ulipo Dk. Mwakyembe. Wakati
wengine wamezoea kusema ugua pole, mimi nikimbilie kutumia lugha ya
Kiingereza kidogo ili niweze kueleweka ninaposema ‘Get well soon.’

 Nimeanza kukupa pole Mwakyembe, kwa sababu najua historia ya ugonjwa
wako ilianza tangu Oktoba 9, mwaka jana ulipougua na baadaye kuonekana
haja ya kupelekwa nchini India kwa matibabu zaidi.

 Mara kadhaa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta,
amekuwa akijitokeza hadharani kukusemea, akidai kwamba ugonjwa wako
unatokana na sumu.

 Hata hivyo, Februari 17, mwaka huu, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa
ya Jinai (DCI), Robert Manumba, alisema kwa mujibu wa taarifa zilizopo
Polisi ambazo wamezipata kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii
zinaonesha kuwa hukulishwa sumu.

 Manumba alisema kuwa waliwasiliana na Wizara ya Afya ili kubaini
chanzo cha ugonjwa wako, na taarifa ikawa hiyo, kwamba hujalishwa
sumu.

 Kamishna Manumba alisema hata kabla ya madai ya Sitta, Jeshi la
Polisi lilikuwa linafanya uchunguzi kuhusu madai yako ya kupokea
ujumbe wa kutishiwa maisha na kwamba lilikuwa linaendelea na jukumu
hilo ambalo nadhani bado halijakamilika.

 Hata hivyo siku moja baada ya kauli hiyo ya DCI Manumba, Dk.
Mwakyembe; kiongozi wangu, ulieleza kukerwa na kile ulichokiita
taarifa za uongo kwa wananchi, ikiwa ni pamoja na kuingilia utaratibu
wa matibabu yako bila idhini yako.

 Katika taarifa yako, ulifafanua kuwa si lazima mtu anyweshwe sumu ili
imdhuru, bali inaweza kumdhuru hata kwa kugusishwa, tamko ambalo kwa
hakika linapingana na la Sitta, anayetia bidii kukusemea, anayedai na
kusisitiza kwamba umelishwa sumu.

 Mwakyembe, kimsingi hapa nimechanganyikiwa na naomba uniweke sawa,
maana utolewaji wa haraka wa taarifa yako, umekuja wakati ambao
haukutarajiwa, kwa sababu kwa jinsi taarifa zinavyovumishwa ni kwamba
hupo hoi, ndiyo sababu nashindwa kuamini hiyo haraka ya kujibu na
nadhani ulikuwa umeiandaa taarifa na kuiweka kabatini ikisubiri tukio?

 Nasema hivyo nikiamini alichokisema DCI Manumba kuhusu afya yako
hakikuwa tamko rasmi la Polisi, bali ni jibu alilotoa kwa ufupi, baada
ya kuulizwa swali la ghafla na mwandishi wa habari ambapo alitaka
kujua hatua iliyochukuliwa kuhusu madai kwamba ulipewa sumu.

 Wakati nakuandikia waraka huu napenda ujue kwamba, ninaamini katika
ukweli na haki na kamwe, sifanyi kama Pilato kuruhusu hukumu kwa Yesu,
japo yeye haoni kosa.

 Ninachelea kusema kuwa kweli DCI Manumba alitoa taarifa kuhusu afya
yako bila kupanga kwa kuwa siku hiyo alikuwa anazungumzia rasmi
taarifa kuhusu mwenendo wa uhalifu nchini kwa kipindi cha mwaka jana.
Japo hoja hiyo iliyojibiwa kwa ufupi, ndiyo ilitawala vichwa vya
habari siku iliyofuata. Kwetu “sisi washika kalamu”, “bad news, good
news”.

 Manumba alilenga na kujikita kuzungumzia namna kasi ya ukuaji wa
kiwango cha uhalifu ilivyokuwa nchini kwa kipindi cha mwaka jana,
jitihada na mbinu zilizotumika kuukabili uhalifu huo, pamoja na mbinu
za kuudhibiti kwa siku zijazo. Ingawa Mwakyembe usishangae kuona mambo
muhimu yote yaliyotolewa taarifa kuhusu usalama wetu tuliyaacha, ili
tutoe habari kukuhusu, lakini tukiamini itauza!

 Ndiyo maana katika kujibu swali la mwandishi huyo, DCI Manumba
alikuwa makini kusisitiza kuwa, ile ni taarifa kutoka Wizara ya Afya;
kwamba ndiyo inaonesha hivyo, akijua kwamba hazungumzii ushahidi, bali
moja ya vyanzo vyao vya taarifa nyingi walizonazo za uchunguzi wao
kukuhusu.

 Kama mimi ningekuwa ndiye wewe ambaye ni mbunge na mmoja wa mawaziri,
nikizingatia kuwa watu wanapenda kujua hali ya kiongozi wao,
ningejitokeza hadharani kuwaambia wananchi ukweli kuhusu tatizo langu
kabla wengine hawajanisemea kwa usahihi au kimakosa, ama kwa
kuchokozwa waseme kwa mujibu wa taaluma zao.

 Ni bahati mbaya kwamba badala ya kujitokeza, umekuwa kimya hadi
wengine wanakusemea katika mazingira yasiyofaa, ilhali uwezo huo unao
mwenyewe kama ulivyofanya baada ya kuchokozwa na waandishi kupitia kwa
DCI Manumba.

 Kwa mfano, kwa kuwa unakiri kwamba umelishwa au kugusishwa kama si
kunusishwa sumu, siku ile ulipokuwa katika Kanisa la Ufufuo na Uzima
la Kawe, jijini Dar es Salaam ukasema tangu utoke India hiyo ndiyo
ilikuwa siku yako ya kwanza kuvaa viatu, ungesema kabisa pia kuwa
tatizo linalokusumbua kwa mujibu wa vipimo ni hili.

 Kwa kuwa wewe ni msomi na kiongozi mkubwa serikalini, Watanzania hapo
wangetarajia pia useme mwenyewe sumu kama ulipewa, ulilishwa,
uligusishwa au ulinusishwa lini, wapi na nani alihusika ili jamii
imjue ‘mchawi’ wako.

 Ijulikane wazi kuwa viongozi nao ni watu kama ulivyo wewe na mimi,
hawana mkataba rasmi na Mungu juu ya kufa au kuugua. Hawana kinga ya
ziada dhidi ya maradhi kama walivyo watu wengine na kwa msingi huo,
tusiende na kufika mahali ambapo suala la ugonjwa nalo linaweza
kutumika kama mtaji wa kisiasa.

 Hata hivyo waraka wangu kwako Naibu Waziri wangu Mwakyembe, haulengi
kukulaumu au kukuongezea mawazo katika wakati huu mgumu wa changamoto
ya ugonjwa, kwa sababu nadhani katika hilo kuna uwezekano mkubwa
kwamba ulighafirika kutokana na hali ya ugonjwa.

 Wito wangu kwako na kwa wengine wa ngazi yako inapotokea mkapatwa na
mdororo wa afya na kukawa na mkanganyiko wa fikra miongoni mwa watu,
ni vema mnapopata nafasi mjitokeze kuzungumza na wananchi. Kwa sababu
si jambo la ajabu sana wala si wa kwanza kudhoofika kiafya!

 Rafiki yangu Mwakyembe, najua unaumwa na unahitaji mapumziko, lakini
naomba ujue kuwa kiongozi hasa wa serikali kama waziri, anapokuwa
mlalamikaji dhidi ya serikali ile ile anayoitumikia, anatengeneza
mazingira mabaya ya kujishushia heshima na kutoaminika, jambo ambalo
linaifanya jamii imtazame na kumdhania kwamba ana jambo jingine sirini
ila anatafuta pa kutokea.

 Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa yako, nadhani unaamini kuna dalili
ya kutoaminiana ndani ya serikali. Dawa ya hali hii si kulumbana
wakati ambao unahangaikia afya yako, bali ni kuutii wimbo wa msanii
aitwaye ‘20 Percent’, unaosema, “Yanini malumbano, ya nini maneno?
Najiweka pembeni kuepusha msongamano.” Toka, kaa pembeni.

CHANZO: Tanzania daima

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.