TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Februari 25, 2012
Msafara wa Yanga utakaokuwa uwanjani kwa ajili ya mechi ya marudiano ya Ligi ya
Mabingwa Afrika dhidi ya Zamalek itakayochezwa wikiendi ijayo nchini Misri unatakiwa
kuwa na watu wasiozidi 40.
Kwa mujibu wa maelekezo ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) yaliyotumwa
jana Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), ni idadi hiyo tu inayotakiwa kwa
vile Zamalek inakabiliwa na adhabu ya kucheza mechi hiyo bila washabiki.
Adhabu ya Zamalek kutocheza mechi mbili za nyumbani za michuano hiyo bila washabiki
ilitolewa Aprili 20 mwaka jana na Bodi ya Nidhamu ya CAF iliyokutana jijini
Johannesburg, Afrika Kusini.
Mechi dhidi ya Yanga ndiyo itakayokuwa ya kwanza kwa Zamalek kuanza kutumikia adhabu
hiyo iliyotakana na washabiki wake kufanya fujo kwenye mechi ya michuano hiyo mwaka
jana ilipocheza dhidi ya Club Africain ya Tunisia.
Hivyo kila timu (Yanga na Zamalek) katika mechi hiyo inatakiwa kuwa na wachezaji
ambao wana leseni za CAF kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa 2012. Pia benchi la ufundi
katika kila timu linatakiwa kuwa na watu watano.
Kwa klabu zote mbili, kila moja imeruhusiwa kuingia na wajumbe wake wa Kamati ya
Utendaji wasiozidi kumi. Mbali ya klabu hizo mbili, wengine waliotajwa kuruhusiwa
kuingia uwanjani ni vijana 20 watakaofanya kazi ya kuokota mipira (ball-boys).
Mechi hiyo itachezeshwa na waamuzi kutoka Morocco ambao ni Jihed Redouane, Rouani
Bouazza na Bekkali Mimoun wakati mwamuzi wa akiba atakuwa Gihed Greisha wa Misri.
Kamishna wa mchezo huo ni Ben Khadiga wa Tunisia.
MSUMBIJI KUTUA NCHINI FEBRUARI 26
Timu ya Taifa ya Msumbiji (Mambas) itawasili nchini kesho (Februari 26 mwaka huu)
kwa ndege ya South African Airways. Ndege hiyo yenye mruko namba SA 186 inatarajia
kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 7.55 mchana.
Msafara wa Mambas kwa ajili ya mechi dhidi ya Taifa Stars itakayochezwa Jumatano
(Februari 29 mwaka huu) saa 10 kamili jioni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
utakuwa na watu 29. Kati ya hao, 19 ni wachezaji wakati waliobaki ni maofisa wa timu
hiyo.
Mwamuzi wa mechi hiyo Farouk Mohamed na wasaidizi wake Ayman Degaish, B.T Abo El
Sadat na Gihed Greisha kutoka Misri watawasili nchini kesho (Februari 26 mwaka huu)
kwa ndege ya Egypt Air. Kamishna ni Loed Mc Ian kutoka Afrika Kusini.
Tiketi kwa ajili ya mechi hiyo zitaanza kuuzwa Jumanne (Februari 28 mwaka huu)
katika vituo vya vya Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Kituo cha mafuta cha Bigbon
kilichopo Msimbazi (Kariakoo), mgahawa wa Steers ulioko Barabara ya Samora/Ohio,
Kituo cha mafuta cha Oilcom Ubungo na Uwanja wa Taifa.
source
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment
Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.