CHAMA cha NCCR-Mageuzi kimewafungulia mashtaka Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Spika wa Bunge, Anne Makinda na Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah kikitaka viongozi hao wachukuliwe hatua za kisheria kwa madai ya kukikuka Katiba ya nchi.

Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia zinasema kuwa NCCR Mageuzi kinawashtaki viongozi hao kwa kumtambua Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila.

Kafulila ambaye pia ameunganishwa katika mashtaka hayo, alifukuzwa uanachama ndani ya NCCR Mageuzi, Desemba 18, mwaka jana na kikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho zikiwa ni siku 10 tangu alipoenguliwa katika nafasi ya Katibu Mwenezi, akituhumiwa kutoa siri za chama.

“Kweli tumefungua kesi Mahakama Kuu lakini sasa mimi niko nje ya ofisi, naomba umtafute Katibu Mkuu Sam (Ruhuza) ili akupe details (taarifa) zaidi,” alisema Mbatia juzi mchana.

Akizungumza kwa simu, Ruhuza alikiri chama chake kufungua kesi dhidi ya Spika, Katibu wa Bunge na Kafulila, lakini hakuwa tayari kueleza kwa undani madai waliyoyawasilisha mahakamani.

“Ni sahihi unavyosema ndugu yangu. Tumefungua kesi mahakamani dhidi ya hao uliowataja (Spika, Kashililah na Kafulila), lakini siwezi kukuambia vipengele vya madai yetu kwa sababu ni kesi. Fika mahakamani itakapoanza utafahamu kila kitu,” alisema Ruhuza.

Hata hivyo, habari kutoka Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam zinasema NCCR Mageuzi katika kesi hiyo wanaiomba iwachukulie hatua Spika na Katibu wa Bunge kwa kosa la kuvunja Katiba kwa kumruhusu Kafulila kuendelea na kazi za Bunge hali akiwa si mwanachama wa chama chochote cha siasa.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, pia chama hicho kinaiomba Mahakama kumchukulia hatua za kisheria Kafulila kwa kufanya kazi za ubunge hali akijua kuwa hana sifa za kushika wadhifa huo kikatiba baada ya kufukuzwa uanachama ndani ya NCCR Mageuzi.

Taarifa zinasema kesi hiyo imepangwa kwa Jaji Alice Chingwile ambaye pia anasikiliza kesi iliyofunguliwa na Kafulila pamoja na wenzake wakipinga kuvuliwa uanachama.

Dk Kashililah, Kafulila
Katibu wa Bunge, Dk Kashililah alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema: “Mahakamani ni sehemu ya kwenda kupata haki. Iwapo NCCR wanakwenda huko ni sawa kwa sababu wanakwenda kutafuta haki.”

Alisema suala la Spika, Naibu wake pamoja na yeye kushtakiwa kwa mujibu wa nafasi zao siyo jambo la ajabu na kwamba siku ikifika wakiitwa mahakamani watajibu hoja hizo kwa mujibu wa taratibu walizozitumia.

Alipotakiwa kuelezea juu ya namna walivyomruhusu Kafulila kuhudhuria vikao vya Bunge, alisema: “Kwa mujibu wa taratibu, mwenye mamlaka ya kutamka kuwa huyu ni mbunge au siyo mbunge tena ni Spika.”

Lakini akasema suala la Kafulila waliliamua kwa mujibu wa taratibu na sheria baada ya kupokea taarifa za NCCR juu ya kumfukuza uanachama, Msajili wa Vyama vya Siasa na Mahakama.

“Nakiri tulipokea taarifa za NCCR. Vilevile tulipokea za Msajili wa Vyama vya Siasa na pia tulipokea zuio la Mahakama la kumfukuza ubunge Kafulila na hilo ndilo msingi wa hali ya sasa,” alisema Kashilila.

Kwa upande wake, Kafulila alisema: “Ndiyo kwanza nalisikia kwako, sina taarifa. Lakini kama wamenishtaki mimi basi nasubiri pengine nitaarifiwa maana haya mambo ya kisheria yana taratibu zake na wanafahamu jinsi ya kumfikia mtu pale wanapomhitaji.”

Kesi ya awali
Baada ya kuvuliwa uanachama, Kafulila alifungua kesi katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam akiiomba itengue uamuzi wa Halmashauri Kuu (Nec) chama chake kumvua uanachama, uamuzi ambao utekelezaji wake unamfanya apoteze sifa za kuwa mbunge.

Sambamba na kesi hiyo ya msingi, pia Kafulila kupitia kwa wakili wake, Daniel Welwel aliwasilisha maombi akiomba Mahakama iamuru utekelezaji wa chama hicho kumvua uanachama usitishwe hadi kesi ya msingi itakapomalizika.

Desemba 27, mwaka jana, Jaji Chingwile alikubaliana na maombi ya Kafulila hivyo kuamuru NCCR- Mageuzi kutochukua hatua nyingine zozote dhidi ya Kafulia na wenzake hadi kesi yao ya msingi itakapoamriwa.

Mbali na Kafulila, walalamikaji wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa mgombea urais kupitia chama hicho katika Uchaguzi Mkuu 2010, Hashimu Rungwe, Mbwana Hassan, Henry Mapunda, Kayombo Kabutali, Sued Omar, Diamond Mwasampeta na Issa Hussein.

Kesi hiyo namba 218/2011 ilikuwa imepangwa kutajwa Februari 20, mwaka huu lakini iliahirishwa hadi Machi 15, mwaka huu kutokana na Jaji Chingwile kukabiliwa na majukumu ya kusikiliza kesi nyingine za mauaji mkoani Morogoro.

SOURCE: MWANANCHI