Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Saturday, February 25, 2012

DANGURO LA WATOTO DAR

Na Richard Bukos
GESTI moja maarufu (jina tunalo) iliyopo Buguruni Malapa, Dar es Salaam imegeuzwa danguro la watoto, Risasi Jumamosi limeinyaka.
Katika msako wa kila siku unaofanywa na jeshi la polisi, gesti hiyo imekuwa ikikutwa na watoto wanaochukuliwa mikoani kwa lengo la kufanyishwa biashara hiyo haramu ya ngono.
Kwa mujibu wa mtoto mmoja aliyehojiwa na Risasi Jumamosi baada ya kutelekezwa katika gesti hiyo aliyefahamika kwa jina la Rehema mwenye umri wa miaka 15, aliyetoka kwa wazazi wake huko Mwanga mkoani Kilimanjaro alichukuliwa na mwanamke mmoja aliyemtaja kwa jina la Vero kwa lengo la kuja kumtafutia kazi za ndani.
“Baada ya kufika Dar, sikutafutiwa hiyo kazi matokeo yake alinileta kwenye hii gesti na kuanza kunifanyisha ukahaba ili tupate fedha ya kulipia chumba wakati ananitafutia kazi,” alisema binti huyo.
Binti mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Ashura mwenye umri wa miaka 14, akiwa na wenzake wawili, Jenipher na Rose, aliliambia gazeti hili kuwa, yeye na wenzake
 walifika kwenye gesti hiyo kwa kuwa hawana sehemu ya kulala.
“Mimi kwetu ni Ifakara, Morogoro, nimeletwa maeneo haya na mama yangu mdogo, sina pa kulala, nimeona niungane na wenzangu ili nipate pa kulala,” alisema Ashura na kuongeza:
“Mama mdogo aliniambia ili nipate fedha za kujikimu na kulipia chumba lazima niwakubali wanaume wanaokuja hapa kutuchukua kwani siwezi kupata kazi kwa sababu hata shule ya msingi sikumaliza.”

NGONO BUKU MBILI TU!
Alipoulizwa malipo anayopata anapochukuliwa na mwanaume, Ashura alisema:
“Mwanaume mwenye huruma anaweza kukupa pesa nyingi lakini wengi wanatoa buku mbili kwa usiku mmoja na chumba analipia yeye.”
WENGINE HAWATUMII KINGA
Alipoulizwa kama yeye na wenzake wanatumia kinga wanapokutana na wanaume hao, Ashura alizungumza kwa niaba ya wenzake:
“Kuna wanaume waelewa, hao huwa wanatumia, lakini kuna wengine hawatumii hasa walevi au anaweza kukudanganya
 kuwa wanatumia alafu mkishaingia chumbani wanakubadilikia.”

POLISI WAVAMIA, WASHUHUDIA UCHAFU
Risasi Jumamosi lilishuhudia operesheni iliyoendeshwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalum hivi karibuni ambapo vijana hao wa Kamanda Suleiman Kova walishuhudia uchafu wa aina yake katika gesti hiyo hivyo wakawakamata mabinti hao na kuwapeleka kituoni kwa mahojiano zaidi.

RISASI JUMAMOSI MZIGONI
Gazeti hili lilizama ndani ya gesti hiyo ili kuzungumza na uongozi wake ambapo kwa mujibu wa mwanamke aliyekutwa mapokezi aliyejitambulisha kwa jina la Miriam, nyumba hiyo ya wageni inamilikiwa na mwanamke mmoja aliyetajwa kwa jina la Mama Maporoni.
“Mimi nimeachiwa madaraka yote hapa, mama hayupo labda nikupe namba yake (huyo mmiliki) ili akupe ufafanuzi kamili,” alisema mwanamke huyo aliyeonesha kupigwa na butwaa baada ya mwandishi kujitambulisha.
Juhudi za kumpata mmiliki huyo anayedaiwa kufanya biashara hiyo kwa muda mrefu ziligonga mwamba baada ya simu yake kuita bila ya kupokelewa.

KAMANDA SHILOLGILE
Akizungumzia msako huo unaoendelea, Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Kamanda Faustine Shilogile alisema operesheni hiyo inaendelea na wahusika wote wakibainika watafikishwa kwenye vyombo vya sheria.

KUTOKA RISASI JUMAMOSI
Tunatoa pongezi kwa jeshi la polisi kwa operesheni hiyo iliyolenga kufuta biashara hiyo haramu ya ngono, lakini ni vema askari hao wakaongezewa nguvu.

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.