Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Sunday, February 26, 2012

Je, Ukahaba nchini uvikwe taji la Heshima?


HIVI karibuni Shirika la Uchumi la Wanawakae Tanzania SUWATA liliendesha semina maalum kwa ajili ya makahaba jijini juu ya namna ya kuepuka kupata mimba au maambukizo ya UKIMWI.
Katika Semina hiyo iliyofanyika katika hoteli ya Ambassador Plaza na kuwashirikisha changudoa zaidi ya thelathini, mbinu mbalimbali za kinga kama vile matumizi ya Kondom na kadhalika zilifundishwa.
Mkurugenzi wa SUWATA Mama Magreth Kota alikaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa semina hiyo ina nia njema kwani baada ya kuwafunza changudoa hao mbinu za kujihami na mimba na magonjwa ya zinaa ,hatua itakayofuata ni kuwashawishi waachane kabisa na biashara yao hiyo ya kuuza miili.
Kwa mtazamo wa juu juu Semina hiyo inaweza hasa kwa jamii inayoelekea katika upotofu kuonekana yenye manufaa. Lakini ukweli ni kwamba madhara yake ni makubwa kuliko faida.
Kwanza hatua hiyo japo inajenga uhusiano mzuri kati ya jamii ya kawaida na ile ya changudoa lakini pia inawafanya changudoa waanze kuhisi kutambuliwa kwa shughuli yao haramu ya kujiuza. Kwa nini wasihisi hivyo wakati jamii imejitolea kuwafundisha mbinu za kupunguza hatari zinazowakabili katika kazi hiyo ya ukahaba? Lipi litakalowafanya wasitafsiri hatua hiyo kama kibali cha jamii kwa 'endeleeni na ukahaba, lakini jilindeni?"
Jamii nyingi za Magharibi (nchi za Ulaya na Marekani) zimefikia mahali pa kuzitambua tabia chafu za makahaba na hata mashoga kuwa halali na hata kuwalinda kwa sheria.
Vyama vya Makahaba katika nchi hizo vimeandikishwa na vinaendesha shughuli zake na kuandikisha wanachama wapya bila matatizo na hata kufanya sherehe za maadhimisho mbalimbali ya kutukuza uovu wao.
Tunachelea kwa mafunzo haya yanayotolewa kwa Changudoa ni hatua za awali za kuelekea katika upotovu huo wa kimagharibi. Tunaamini pia kwamba jamii ya Watanzania isipopiga vita hatua hiyo ingali katika hatua za awali kwa kuwa sisi nasi si kisiwe pekee katika dunia hii iliyopunguzwa sana ukubwa wake na sayansi katika muda mfupi tutafikia pale tusipotaka kufika.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa SUWATA baada ya mafunzo hayo shirika lake litawashawishi machangudoa waachane kabisa na 'kazi' yao.
Sisi tunaamini kuwa baada ya kuwafundisha changudoa namna ya kufanya kazi yao kwa 'usalama zaidi' kama waitavyo kazi ya kuwashawishi waachane na ukahaba inakuwa ngumu maradufu.
Unawezaje kumsaidia adui yako kuimarisha silaha zake kisha useme hiyo itakurahisishia kupigana naye vita? Moja ya vikwazo vinavyopambana na changudoa hivi sasa ni hofu ya ujauzito na magonjwa ya zinaa ikiwa ni pamoja na Ukimwi.
Tunaamini kuwa njia bora ya kuwasaidia ingekuwa kuwapatia semina juu ya ubaya wa kazi ya ukahaba na kuwapatia uwezo, nyenzo na mbinu za kuendesha miradi halali mbadala ya itakayowezesha kupata riziki zao.
wale walioathiriwa sana na shughuli ya ukahaba wangepatiwa huduma ya muda mrefu ya ushauri nasaha.
Lakini kuwapa semina ya namna ya kujiepusha na maambukizi ya zinaa wawapo katika uovu wao ni kuuvika taji la heshima ukahaba wao.

Chanzo: http://kiongozi.tripod.com

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.