Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi


Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi, ameondoa mashtaka aliyoyafungua katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, dhidi ya wabunge watatu aliowalalamikia kwa kumshambulia bungeni na kumhusisha katika kashfa ya uuzaji wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) kwa njia za kifisadi.

Wabunge walioshtakiwa na Dk. Masaburi katika kamati hiyo, ni Halima Mdee (Kawe-Chadema), Godfrey Zambi (Mbozi Mashariki-CCM) na Abdulkarim Shah (Mafia-CCM).

Dk. Masaburi alidai wabunge hao walimshambulia na kumhusisha na kashfa hiyo wakati wakichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Uchukuzi, katika Mkutano wa Nne wa Bunge, mwaka jana.

Katika mjadala huo, wabunge hao na wengine walitishia kutoipitisha bajeti hiyo na kutaka wote waliohusika katika uuzaji wa UDA wawajibishwe.
Pia walitaka Dk. Masaburi ajiuzulu kabla ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, hajaingilia kati na kuunda kamati kuchunguza kashfa hiyo.

Uamuzi wa Dk. Masaburi kuondoa mashtaka hayo dhidi ya wabunge hao, ulijulikana kufuatia kikao cha kamati hiyo, kilichofanyika katika Ofisi Ndogo ya Bunge, jijini Dar es Salaam juzi na jana.

Kikao hicho kiliongozwa na Mwenyekiti wake, ambaye pia ni Mbunge wa Mlalo (CCM), Brigedia Jenerali Mstaafu Hassan Ngwilizi.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zilizothibitishwa na baadhi ya wajumbe wake zinaeleza kuwa, uamuzi huo wa Dk. Masaburi, ulifikiwa baada ya

kumuandikia barua Spika wa Bunge, Anne Makinda, kumueleza juu ya uamuzi wake wa kuondoa shauri hilo.
Kwa mujibu wa habari hizo, barua hiyo kwa Spika iliandikwa na Dk. Msaburi, Januari 12, mwaka huu.

Habari hizo zinaeleza kuwa, Dk. Masaburi, aliithibitishia kamati hiyo jana kuhusu uamuzi wake huo.
Baada ya kuthibitishiwa hivyo, kamati hiyo iliona shauri hilo kuwa halina afya, hivyo kufikia maamuzi ya kutoendelea nalo. Mmoja wa wabunge walioshtakiwa na Dk. Masaburi ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema jana kuwa waliitwa kwenye kikao hicho kwa lengo la kutoa utetezi wao mbele ya kamati hiyo.

“Tulifika kwenye kamati. (Dk. Masaburi) akaanza yeye kuzungumza. Tukamsikiliza,” alisema mbunge huyo.
Alisema tofauti na awali, katika maelezo yake, Dk. Masaburi, aliwatetea wabunge hao akisema walilazimika kutamka waliyoyatamka bungeni kuhusu

kashfa ya UDA kutokana na kupatwa na uchungu kwa kuona ubadhirifu ukifanywa dhidi ya mali za shirika hilo la umma.
“Hata hivyo, alisema kule kunisema moja kwa moja haikuwa 'proper' (sawa),” alisema mbunge huyo.

Alisema baada ya Dk. Masaburi kutoa maelezo yake, walipata fursa ya kutoa ushauri mbele ya kamati hiyo.
Mbunge huyo alisema katika maelezo yao, walisisitiza kwamba yote waliyoyasema bungeni, ikiwamo kudai kueleza kwamba Dk. Masaburi aliingilia mchakato wa uuzaji wa UDA, yalikuwa sahihi.

“Aliingilia mchakato wakati mwenye mali ni serikali, yeye ni msimamizi tu,” alisema.
Alisema baada ya kutoa maelezo yao, walitakiwa na kamati kutoka nje ili wapate kushauriana na baadaye waliitwa tena kuendelea na kikao.

Mbunge huyo alisema waliporudi kwenye kikao, Ngwilizi kwa niaba ya kamati alisema kwa vile Dk. Masaburi amethibitisha kuwa alikwishamuandikia Spika barua kueleza juu ya uamuzi wake wa kuondoa shauri hilo, kamati imeona haina sababu ya kuendelea nalo.

Hata hivyo, mbunge huyo alisema kamati hiyo imemtaka Dk. Masaburi kupeleka barua hiyo mbele ya kamati.
Siku chache baada ya sakata la kashfa hiyo kuibuka na kushikiwa bango na wabunge, Dk. Masaburi, aliwashukia wabunge hao na kuwashutumu

baadhi yao kuwa wanashindwa kufikiri kwa kutumia vichwa na badala yake wanafikiri kwa kutumia 'makalio'.
Dk. Masaburi alitoa kauli hiyo nzito mjini Arusha alipozungumza na waandishi wa habari, ambako alikuwa akihudhuria mkutano wa pamoja wa kamati

za uongozi za serikali za mitaa za nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACLAT), Agosti, mwaka jana. Katika mkutano na wanahabari mjini Arusha, Dk. Masaburi alisema yeye ndiye aliyeibua kashfa hiyo wakati akihoji mali zinazomilikiwa na jiji na kuambiwa UDA imeishauzwa.

“Nilipofuatilia nikakuta imeuzwa Sh. milioni 285! Nilipofuatilia hizo fedha kama zipo nikakuta milioni 200 zimeshaliwa; nikaamua kumsimamisha meneja wa shirika hilo na mhasibu. Sasa leo nageuziwa kibao kuwa mimi ndiye nimeuza inashangaza sana,” alisema Dk. Masaburi.

Dk. Masaburi alipotafutwa jana na NIPASHE kuzungumzia suala hilo, hakupatikana na hata alipopigiwa simu yake ya mkononi hadi tunakwenda mitamboni ilikuwa imezimwa. Naye Mgwilizi alipotafutwa simu yake ilikuwa imezimwa.

SOURCE: NIPASHE