Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Wednesday, February 29, 2012

JK omba samahani sasa kwa wana-Njombe

Leo nazungumza na Rais Jakaya Kikwete, huku nawe, msomaji wangu ukishiriki kusoma yale nitakayomwandikia hapa kiongozi huyu wa Tanzania na watu wake.
Mheshimiwa rais wangu, samahani ni neno dogo sana, ingawa linabeba maana kubwa na thamani kwa wanaojua umuhimu wake. Kwa wasiojua, tunawasamehe na kuwahimiza kutafuta umuhimu wake. Mara nyingine, samahani hubeba maana sawa na kuomba radhi.
Elimu ya kujua umuhimu wa samahani wala haipatikani shuleni. Haipo darasani; kwamba atasimama mwalimu na kuueleza umma wa darasa kwamba maana ya samahani ni hii na umuhimu wake ni huu.
Ikiwa wapo walioanza kufundishwa umuhimu na matumizi ya - samahani-darasani, basi hao wana ulakini katika mizizi walikotoka.
Mara zote, samahani - huanza kufundishwa kutoka ndani ya familia. Hufunzwa na wazazi. Wakafuata wanafamilia wengine na baadaye jamii inayomzunguka mtoto. Jamii hapa ni majirani. Ni wanamtaa na idadi nyingine ya watu anaokutana nayo mtoto hasa katika viunga vya michezo.
Samahani limekuwa chachu ya kumaliza vinyongo vingi. Limetumika kumaliza migogoro; mikubwa na midogo na zaidi sana limekuwa chanzo cha amani na kujenga daraja la maelewano katika mazingira ambayo yamegubikwa na mifarakano na hata minyukano.
Linaposemwa neno samahani na kukubaliwa na upande wa pili, basi amani hutamalaki na woga, wasiwasi au lawama hupotea kabisa.
Mtu anapoteleza katika kauli na sana sana anaposhindwa kutekeleza ahadi zake, basi hupaswa kuomba samahani na ikibidi, ikifuatiwa na sababu za kushindwa huko.
Ikiwa muungwana ataghafirika katika kauli zake au matendo yake, basi haraka, baada ya kutambua, hujitokeza na kuomba samahani na waungwana wenzie na hata wale wasiokuwa waungwana, humwelewa na kumuheshimu zaidi na zaidi.
Kuomba samahani, siyo utumwa. Sio woga wala kamwe siyo kujidhalilisha mbele ya jamii. Hakuna samahani inayoenda bure. Lazima hubeba heshima inayostahili.
Tena samahani inapoombwa na mtu mkubwa, kiongozi wa familia, kiongozi wa jamii na hata kiongozi wa nchi, hubeba maana kubwa zaidi na kuwa na uzito wake.
Wanaoshindwa kuomba samahani ni watumwa. Ni watu wasiojiamini na mbaya zaidi ni binadamu wasiothamini wengine kwa dhati.
Anayethamini na anayependa wenzake, huumia sana anapogundua ameteleza mahali na haraka haraka, akiwa muungwana wa vitendo, huwaendea na kuwaomba samahani.
Tangu Januari 2, 2012, nimekuwa nikisubiri kupokea samahani ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, Sijaipata. Sijaisikia kutoka kwenye kimywa chako au hata kwa wale wanaomkuzungumzia kwa nafasi yako.
Watanzania wa Njombe hawajakusikia. Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dk Christine Ishengoma hajakusikia. Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Sarah Dumba hajakusikia. Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Georgina Bundala hajakusikia.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima hajamsikia. Mbunge wa Ludewa Deo Filikunjombe hajamsikia. Aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo hajamsikia. Itoshe tu kueleza kwamba hakuna aliyemsikia.
Kwanini hawakusikia? Kwa kuwa hujajitokeza kuomba samahani kwao kwani walikuwapo wote wakati 'ukiapa' kwamba lazima Njombe itakuwa mkoa Januari Mosi, 2012.
Wote tuliokuwapo pale Kijiji cha Mawengi, Ludewa (Mkoa wa Njombe?), tulikusikia na kukuona ukisisitiza kuwa lazima kufikia muda huo Njombe itakuwa mkoa mpya na siyo vinginevyo.
Uliwaeleza wananchi kwamba serikali imekuwa ikitoa ahadi kuhusu mkoa huo na wote waliokuwapo pale, kama kawaida ya Watanzania wengi, tulikuamini na kuamini kuwa kwa kuwa kauli inatoka kwa mkubwa mwenyewe, lazima sasa itakuwa kweli.
Kama nilivyoanza kueleza. Muda sasa umefika kwako, JK kujitokeza na kuomba samahani kwa kushindwa kutekeleza apizo lako kwa watu unaowaongoza.
Ukifanya hivyo utakuwa umeonesha kiwango cha juu mno cha uungwana na uongozi uliotukuka badala ya kuendelea kukaa kimya huku unaowaongoza, hasa wa Njombe wakishindwa kuelewa unafikiria nini baada ya kutotekelezwa kwa uliyoyatoa kinywani mwako na kurekodiwa kwa ajili ya kumbukumbu.
Narudia tena, kuomba samahani siyo woga wala kujidhalilisha, bali ni kiwango cha juu cha uungwana na kujali.
JK jitokeze sasa kuomba samahani na kueleza sababu za kushindwa kutekelezwa kwa apizo lako la kuhakikisha Njombe inakuwa mkoa mpya.
Ukituomba samahani, tutazidi kumheshimu zaidi na kuwa kipimo cha uungwana wake ambao mara nyingi tunauona katika maeneo mengine ya misiba, kutembelea wagonjwa na kuwajali Watanzania wenzake.
Nifikie kwa mawasiliano haya: 0754 020880/0655 274060: simon@simonmkina.com;

 Source: www.simonmkina.com

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.