Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Tuesday, September 24, 2013

ICC yamruhusu William Ruto kurejea Kenya

 23 Septemba, 2013 - Saa 09:19 GMT

Ruto alifikishwa ICC kwa tuhuma za uhalifu dhidi ya binadamu
Majaji katika mahakama ya kimataifa kuhusu uhalifu wa kivita ICC wameahirisha kesi ya naibu Rais wa kenya William Ruto kwa juma moja ili kumpa mda kurejea nyumbani kushughulikia hali ya kiusalama inayokumba taifa hilo.
Watu wanoaminika kuwa magaidi wa Al Shabaab wameteka jumba la kifahari lenya maduka la Westgate jijini Nairobi na kuwazuilia mateka wakenya kadhaa.

Vikosi vya usalama vyaingia Westgate

 23 Septemba, 2013 - Saa 15:32 GMT

Jeshi la Kenya linasema kuwa limedhibiti jengo hilo ingawa hali bado ni mbaya
Milio mikubwa ya risasi na milipuko imesikika huku juhudi za usalama zikiendelea katika jengo la Westgate ambako wanamgmbo wa Al shabaab wameteka jengo hilo pamoja na wakenya wachache ambao wangali kuokolewa.
Kwa mujibu wa waziri wa usalama Joseph Ole Lenku, vikosi vya usalama vimeweza kudhibiti jengo hilo nje na ndani na kwamba ni mateka wachache waliosalia katika jengo hilo.
Serikali inasema watu 62 wameuawa lakini shirika la Red Cross lilisema kuwa idadi hiyo ni 69.
Westgate ni jumba la kifahari lenye maduka na mikahawa karibia themanini .
Milio hiyo ilidumu kwa dakika tatu na kufuatiwa na moshi mkubwa juu ya jengo hilo. Hakuna taarifa kamili kuhusu kilichosababisha moshi huo.
Sehemu ya jengo la Westgate ikitoa moshi
Wapiganaji wa Al shabaab wamewateka nyara raia ambao idadi yao haijulikani. Walikuwemo ndani ya jengo wakiendelea na shughuli zao kuanzia Jumamosi mchana wakati wapiganaji wa Al shabaab walipowavamia na kuanza kufyatua risasi kiholela.
Inaarifiwa kuna maiti kumi katika ghorofa ya kwanza ya jengo hilo.
Aidha wapiganaji hao wanaoaminika kuwa wanachama wa Al Shabaab ni kati ya kumi na kumi na watano na bado wangali ndani ya jengo hilo.
Ripoti zinasema kuwa ufyatulianaji mkubwa wa risasi pamoja na milipuko imesikika katika jengo hilo kwa takriban dakika 15.
Harakati za kuendelea kumaliza operesheni hiyo zinaendelea lakini hali ya mateka walio ndani ya jengo hilo inaendelea kudorora.
Rais Kenyatta amesema kuwa jeshi linajitahidi kuhakikisha kuwa linakabiliana vilivyo na wanamgambo hao.
Wakenya waliofanikiwa kuondoka katika jengo la Westgate kwa usaidizi wa polisi
Helikopta za polisi zinazunguka juu ya jengo hilo pamoja na ndege za kijeshi kushika doria. Vikosi vya usalama vinaendelea na operesheni kujaribu kuwanusuru waathiriwa wakati hali ikiwa ni ya ati ati katika eneo la shambulizi.
Awali jeshi la Kenya lilisema limeweza kudhibiti jengo hilo lote ingawa bado limetaja hali kuwa tete mno hasa katika kujaribu kuwaokoa mateka waliosalia ndani ya jengo hilo.
Ripoti zinasema kuwa watu 69 wamefariki katika shambulizi hilo la Al Shabaab kufikia sasa huku 175 wakijeruhiwa. Baadhi wametibiwa na kuondoka hospitalini. Baadhi ya majeraha waliyopata ni majereha ya risasi na kutokana na guruneti ambalo Al shabaab waliwarushia wale waliokuwa ndani ya mikahawa siku ya Jumamosi.
Kundi hilo limekiri kutekeleza shambulio hilo kutokana na hatua ya Kenya kupeleka majeshi yake nchini Somalia ili kukabiliana na wapiganaji hao.

Chanzo: BBC

Chenge (Mb) amesema kodi ya kadi za simu (SimCardTax) ni sahihi kwa utafiti wao; aulizwe kupitia 0754782577 atoe maelezo zaidi na vielelezo vya ziada

Posted: 25 Jul 2013 04:35 AM PDT
Leo tarehe 25 Julai 2013 chombo kimoja cha habari kimemnukuu Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti Andrew Chenge (Mb) akisema kwamba uamuzi kuhusu kodi/tozo ya kadi/laini za simu haukuwa wa kubahatisha. Chenge amesema kwamba kamati yake ilifanya utafiti wa kina na kisha kufikia uamuzi wa kuona tozo hiyo ni sahihi.

Ni muhimu akatakiwa kupitia namba yake 0754782577 atoe maelezo zaidi kuhusu usahihi wa tozo hiyo na aeleze ni wapi wananchi na wadau mbalimbali wanaweza kupata vielelezo vya utafiti walioufanya.

Aidha, wenye maswali kuhusu nini hasa kilijiri kwenye kamati ya bajeti mpaka kamati hiyo ikakataa jedwali la marekebisho nililowasilisha tarehe 27 Juni 2013 kabla ya muswada wa sheria ya fedha kupitishwa bungeni tareheb 28 Juni 2013 kwa kuwa yeye ambaye ndiye msemaji wa kamati ameanza kutoa majibu. 

Pia, aeleze iwapo yupo tayari kumshauri Spika aruhusu kamati ya bajeti ikutane kwa dharura wiki ijayo kufanya kazi ya kupitia matumizi ya Serikali kwa lengo la kuanisha maeneo ambayo Serikali inaweza kubana matumizi kwa haraka kufidia pengo la bilioni 178 zinazotafutwa kwenye tozo hiyo ya simu. Hatua hii itawezesha kodi hiyo kuacha kutozwa bila ya kulazimika hata kuongeza vyanzo vingine vya fedha iwapo Serikali inasuasua kupanua wigo wa mapato.

Izingatiwe kuwa katika kuwawakilisha wananchi kuepusha kutozwa kodi ya kumiliki kadi ya simu na nyingine zenye kuongeza gharama za maisha kwa wananchi, kabla ya kupitishwa kwa muswada wa sheria ya fedha nilichukua hatua kuanzia bungeni katika mkutano uliopita wa Bunge.

Niliwasilisha kwa Bunge kupitia ofisi ya Katibu wa Bunge jedwali la marekebisho ya sheria hiyo kwa mujibu wa Kanuni ya 86 (11) ambapo pamoja na mapendekezo mengine nilitaka kifungu katika jedwali la marekebisho la Serikali kilichopendekeza kuanzisha ushuru huo kiondolewe.

Ikumbukwe kwamba kwamba katika mchango wangu kwa kuzungumza bungeni nilisema muswada wa sheria ya fedha wa mwaka 2013 ni “muswada wa majanga” ambao utaleta athari za ongezeko la bei ya bidhaa na huduma muhimu.

Hata hivyo, Kamati ya Bajeti chini ilikataa mapendekezo hayo, hata hivyo kwa kuwa masharti ya kanuni za kudumu za Bunge yanakataza mbunge mwingine kutoa taarifa za majadiliano ya ndani ya kamati sitaeleza kwa undani yaliyojiri katika kikao cha kamati tajwa. 

Hivyo taarifa rasmi na sababu za mapendekezo hayo kukataliwa zinaweza kutolewa na mwenyekiti wa kamati hiyo Mh. Andrew Chenge (Mb) kwa kuulizwa kupitia namba yake ya simu ya mkononi/kiganjani (0754782577).

Uongozi bora na uraia mwema wenye uwajibikaji ni chimbuko na chachu ya ukuaji endelevu wa uchumi wa nchi na ustawi wa maisha ya wananchi.

Kwa ufupi nilielelezwa kwamba tayari chanzo hicho cha mapato na vingine vilishaingizwa katika bajeti ya Serikali kwa ajili ya matumizi ya kawaida na ya miradi ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2013/2014 na kupigiwa kura ya ndio na wabunge wengi kabla ya muswada huo wa sheria ya fedha kujadiliwa. Hivyo nilitakiwa kuwasilisha mapendekezo ya vyanzo mbadala vya kuziba pengo litakalotokana na kufuta ushuru huo na kodi zingine nilizopendekeza zifutwe au zipunguzwe. 

Katika muktadha huo kwa upande wa sekta ya mawasiliano pekee, nilipendekeza vyanzo mbadala vyenye jumla ya zaidi ya bilioni 400 za kitanzania ambazo ni zaidi ya lengo lililowekwa na Serikali bila ya kuongeza mzigo wa gharama kwa wananchi wa kawaida. Nilitoa ushuhuda wa kitakwimu kutoka nchi ya Ghana ambayo makampuni ya simu yanachangia asilimia 10 ya mapato ya nchi hiyo bila kuongeza mzigo mkubwa wa gharama kwa watumiaji wa kawaida wa huduma za simu ya kiganjani/mkononi.

Kati ya mapendekezo niliyotoa ni pamoja na kutaka marekebisho ya Sheria ya Mawasiliano ya njia Kieletroniki na Posta ya mwaka 2009 ili kuipa uwezo wa kutosha Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) kufanya ukaguzi wa uwekezaji unaofanywa na makampuni ya simu. Hata hivyo, mapendekezo hayo yalikataliwa na kamati ya fedha chini ya uenyekiti wa Andrew Chenge (Mb).

Ifahamike kuwa kwa kurejea masharti ya Kanuni ya 109 (2) niliwasilisha pia katika ofisi kwa Katibu wa Bunge kabla mjadala kuhusu muswada huo kufungwa mapendekezo ya ziada ya vyanzo mbadala vya mapato vya kuziba pengo lililotokana na marekebisho niliyotaka yafanyike kwa lengo la kupunguza mzigo wa gharama za maisha kwa wananchi kutokana na ongezeko la kodi.

Marekebisho hayo yangechangia katika kudhibiti udanganyifu unaofanywa na makampuni mengi ya simu juu ya uwekezaji na faida wanayoipata. Marekebisho hayo yangewezesha pamoja na mambo mengine makampuni mengi kuorodheshwa katika soko la hisa la Dar Es Salaam na pia kudhibiti usajili wa makampuni katika nchi zenye mfumo wa kuwezesha ukwepaji kodi (Tax Heavens).

John Mnyika (Mb)
25 Julai 2013

Waraka kuhusu muswada wa Baraza la Vijana la Taifa wa Mwaka 2013

Vijana wenzangu na wote wenye dhamira ya kuwezesha maendeleo ya vijana nchini, salaam! 

Mtakumbuka kwamba mwezi Januari 2013 nilitoa taarifa kwa umma ya kueleza kuwa niliwasilisha kwa Katibu wa Bunge Muswada Binafsi wa Sheria ya Baraza la Vijana la Taifa na kuomba hatua za ziada toka ofisi ya Bunge kwa kuzingatia Kanuni ya 21 na Kanuni ya 81 ya Kanuni za Kudumu za Bunge. 

Toka wakati huo muswada huo mpaka sasa Mei 2013 haujachapwa katika gazeti la Serikali na nimepokea barua toka kwa ofisi ya Bunge kwamba wamepokea ushauri toka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa muswada huo hauwezi kuchapishwa katika gazeti la Serikali kwa kuwa umekiuka masharti ya ibara ya 99 ya Katiba ya Nchi. 

Sababu ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutoa ushauri huo ni kuwa muswada unalenga pamoja na mambo mengine kupitia kifungu cha 31 kipengele cha kwanza kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kwa madhumuni ya kugharamia shughuli za baraza la vijana la taifa, mipango ya baraza na kutekeleza miradi ya vijana kwa ajili ya maendeleo ya vijana. 

Kwa maoni yangu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ametoa ushauri huo bila kuzingatia kwamba kifungu cha 31 kipengele cha pili kinataja vyanzo mbalimbali vya fedha za mfuko ikiwemo kutaja kuwa fedha za mfuko zitatokana na fedha zilizotengwa na Serikali na Bunge kwa ajili ya Baraza kwa mujibu wa Ibara ya 135 kifungu cha pili cha katiba ya Nchi.

Ibara ya 135 (2) ya Katiba ya Nchi inatamka kuwa “fedha ambazo hazitawekwa kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali ni zile zote ambazo zimetajwa na sheria ya kwamba zitumike kwa shughuli maalum au ziwekwe kwenye mfuko mwingine kwa ajili ya matumizi maalum”. 

Hivyo, ni maoni yangu kuwa ibara hiyo ya Katiba ya Nchi inaweza kutumika kuwezesha kuanzishwa kwa Baraza la Vijana na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana bila kufungwa na Ibara ya 99 ya Katiba kifungu cha kwanza ambacho kimeweka masharti kuwa “Bunge halitashughulikia jambo lolote kati ya mambo yanayohusika na ibara hii isipokuwa kama Rais amependekeza kwamba jambo hilo lishughulikiwe na Bunge na pendekezo hilo la Rais liwe limewasilishwa kwenye Bunge na Rais.” 

Kifungu cha pili kinataja mambo yanayohusika na ibara hiyo ya 99 ni pamoja na muswada wa sheria kwa ajili ya “kuagiza kwamba malipo au matumizi ya fedha yafanywe kutokana na Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali au mfuko mwingine wowote au kubadilisha kiwango hicho kwa namna nyingine yoyote isipokuwa kupunguza”. 

Toka Sera ya zamani ya maendeleo ya vijana ya mwaka 1996 itamke kwamba Serikali itawezesha kuanzishwa kwa Baraza la Vijana na suala hilo kurudiwa katika Sera mpya ya mwaka 2007; miaka takribani 17 imepita marais wote wa awamu husika na mawaziri wenye dhamana hawajawasilisha bungeni muswada huo hali ambayo imenifanya niandae muswada binafsi kuwezesha baraza kuundwa. 

Muswada wa Sheria ya Baraza la Vijana la Taifa 2013 niliouwasilisha kwa maoni yangu hauna lengo la kuagiza malipo au matumizi ya fedha yafanywe kutokana na Mfuko mkuu wa Hazina ya Serikali au Mfuko mwingine wowote kwa mujibu wa ibara ya 99 bali unalenga kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kwa kuzingatia masharti ya Ibara ya 135. 

Hata hivyo, kwa kuwa muswada huu unahusu mustakabali wa vijana na ni suala la kitaifa kupitia waraka huu naomba kupata maoni yenu kuhusu suala hili, mapendekezo ya marekebisho yanayohitajika kufanyika na hatua zinazopaswa kuchukuliwa. 

Maoni, mapendekezo na hatua hizo zitumwe kupitia mbungeubungo@gmail.com au kwa Afisa wa Ofisi ya Mbunge Ubungo Gaston Garubimbi (0715825025) kabla ya tarehe 24 Mei 2013. 

Nakala ya rasimu ya muswada wa Baraza la Vijana la Taifa wa mwaka 2013 inapatikana katika mtandao wa http://mnyika.blogspot.com kwa ajili ya rejea. 


Aidha, nawaalika kushiriki mikutano ya kupokea maoni kupitia mtandao huo tarehe 20 mpaka 23 Mei 2013 saa 9 alasiri mpaka 10 Jioni ambayo nitashiriki na kutoa maelezo ya zaidi kwa kadiri itakavyohitajika. 

Natarajia kupokea maoni ya vijana na wananchi wengine bila kujali tofauti mbalimbali kwa kuwa madai ya kutaka kuundwe Baraza la Vijana la Taifa yamekuwa yakitolewa na vijana, asasi na taasisi kwa muda mrefu. 

Vyama vya siasa kwa kuzingatia matakwa hayo viliahidi kutekeleza azma hiyo kwa mfano Ilani ya CHADEMA ya mwaka 2010-2015 kipengele 6.4.1 (viii) ilitamka “Kwa kuwa vijana ndio kundi kubwa hapa nchini, na kwa kuwa uhai wa muda mrefu wa taifa letu upo mikononi mwa vijana, Serikali ya CHADEMA itawezesha vijana kuunda Baraza la Vijana (BAVITA) ambalo limekwamishwa na Serikali ya CCM kwa muda mrefu”. 

Kwa upande mwingine, Ilani ya CCM ya mwaka 2010-2015 iliahidi katika kipengele 80 (k) “Kuhamasisha ushiriki wa vijana katika ngazi mbalimbali za maamuzi ikiwa ni pamoja na kukamilisha uanzishaji wa Baraza la Vijana”. 

Mwaka 2011 niliihoji Serikali bungeni ni lini itakamilisha uanzishwaji wa baraza hilo na ikaahidi kwamba kazi hiyo itakamilishwa katika mwaka wa fedha 2011/2012 hata hivyo sasa ni Mei 2013 Serikali haijakamilisha. 

Hivyo vijana, wabunge na wananchi kwa ujumla ni muhimu kuboresha muswada huo na uwasilishwe bungeni kuwezesha baraza la vijana na mfuko wa maendeleo vijana kuanzishwa; maslahi ya umma kwanza. 

Wenu katika uwakilishi wa wananchi,

John Mnyika (Mb) 
19 Mei 2013 
Dodoma
 

Muswada wa Baraza la Vijana 2013-Rasimu ya Kwanza; pakua hapa (download here):
https://docs.google.com/file/d/0B8xvLNf5FlohSHJPX2trR3p6YzQ/edit?usp=sharing

Monday, January 28, 2013

Tamko la makanisa ya P.C.T mkoa wa Mtwara kuhusu gesi ya Mnazi Bay Mtwara

 

by Strictly Gospel


Baada ya kufuatilia kwa undani, na kwa upana kuhusu swala la gesi ambalo linaendelea kuwa ni mgongano au, ni mgogoro kati ya Serikali na wananchi wa Mkoa wa Mtwara/Lindi kuhusu ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kwenda kinyerezi Dar- es –Salaam, tumebaini yafuatayo:-
1. Hakuna Sera ya gesi ambayo husababisha kupatikana Sheria baada ya kupelekwa Bungeni na kuidhinishwa bali kilichopo ni rasimu ya sera ambayo haina ushirikishwaji wa mawazo ya wananchi wa Mkoa wa Mtwara na Lindi, ambako vyanzo vya gesi hiyo ipo.
2. Elimu kuhusu gesi na manufaa yake kwa wananchi haikutolewa ili kujua haki zao kwa madhara yatokanayo na (Uvunaji) uzalishaji wa gesi hiyo, na jinsi watakavyonufaika.
Chama cha Mapinduzi katika Ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2010 inatamka wazi katika Ibara ya 63 kifungu cha H na K juu ya gesi ya Mnazibay Mtwara na Songo songo Kilwa, Lindi kuhusu umeme wa (240 MW) Kinyerezi na (300MW) Umeme wa Mnazi bay Mtwara……
-Vifungu hivi vinafafanua:
• Gesi ya Mnazi bay itakuwa kwa ajili ya Mitambo ya kuzalisha umeme ambayo itajengwa Mtwara (300MW)
• Mitambo ya kuchakata gesi kujengwa Mtwara
• Ujenzi wa viwanda Mtwara ili malighafi itokanayo na gesi itumike kutengeneza mbolea, plastic vikiwemo na viwanda vya Cementi
2. Gesi ya Songo songo inafafanua wazi kuwa gesi hiyo itapelekwa Kinyerezi . Dar –es –Salaam kwa madhumuni hayo hayo.
• Kuendeleza viwanda mbali mbali
• Kuzalisha umeme (240 MW)
• Kuchakata gesi kwa kujenga mitambo
Katika ahadi ya Rais wa Jahuri ya Muungano wa Tanzania alizotoa wakati wa Kampeni za uchaguzi katika hotuba yake ya tarehe 29/10/2010 alitamka wazi kuwa Mkoa wa Mtwara uwe tayari kwa maendeleo makubwa ambayo yanakuja kutokana na gesi iliyogunduliwa katika Mkoa wa Mtwara huko Mnazi bay
Alimainisha/aliainisha juu ya viwanda mbalimbali vitakavyojengwa hapa mkoani vya mbolea,cement, plastic n.k na kuwataka wananchi wajiandae kupokea maendeleo hayo kwa kujenga nyumba nzuri zenye sifa kwa ajili ya wageni. Pia wawasomeshe watoto wao ili wawe na elimu ya juu na kupata ajira katika Makampuni yanayokuja.
Hata baada ya uchaguzi Rais wetu alipokuja kuwashukuru wananchi wa Mkoa wa Mtwara kwa kumchagua, alitamka tena katika hotuba yake akisisitiza ahadi yake ya kujenga viwanda ambavyo vitaleta maendeleo kwa Mikoa ya Kusini na kusababisha ajira kwa wana kusini, na kuagiza kwa Meya wa Manispaa Mtwara/Mikindani kuwapa maeneo ya kujenga viwanda hivyo, kwa kile kilichoonekana kukosa maeneo ya ujenzi huo kwa makampuni hayo. Ahadi hizi alizozitoa kwa wananchi kwa ujumla wao wamezipokea na kuendelea kuzifanyia kazi.
Chanzo cha Matatizo: Mara baada ya kuonekana kile walichokitarajia wananchi wa Mkoa wa Mtwara kwa kutumia gesi ya Mnazi bay kuleta maendeleo yao kuwa imeamriwa kusafirishwa kwa bomba na kupelekwa Kinyerezi Dar –Es –Salaam ili kuzalisha umeme na kuchakata gesi na mitambo hiyo iwe huko.(Mgeuko wa Ilani ya Uchaguzi, na kutozingatia ahadi zake mwenyewe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa kinyume na kauli za usemi wake mwenyewe kwa kukitangaza kituo cha Kinyerezi kuwa ni sehemu ya mitambo ya gesi ya Mnazi bay-Mtwara na Songosongo-Lindi na kwamba bomba hilo litachukua miezi (18) mpaka kukamilika kwake, kwa matamshi haya ndiyo yaliyoleta hasira na chuki kwa wananchi wa Mtwara/Lindi kwa ujumla.
Hali hii imewafanya wananchi wa Kusini kutokuwa na Imani na Serikali na viongozi wake wahusika na sakata hili la gesi kwa semi mbalimbali za viongozi hawa-Mfano.
(1) Kwa hali yoyote gesi lazima itoke Mtwara (Kwa gharama yoyote ile) kwa kukubali ama kutokubali itakwenda Kinyerezi kwa bomba
(2) Kuitwa wahaini wananchi wa Mkoa wa Mtwara kwa kuandamana
(3) Kuitwa wajinga, hawakusoma na kuwa watu wa vijiweni wasio na elimu ya gesi
(4) Nitafanya lolote hata kama nitalaumika na Mataifa mengine lakini wapo watakaochekea yatakayotokea na kauli zinazobadilika kila kunapokucha.
(5) Usemi wa kuigawa nchi vipande vipande
Viongozi hawa hawajui kuwa chanzo kipo kwao wenyewe, kwa kutozingatia kuwa wananchi hao ambao hawana elimu kama yao wanao upeo mkubwa wa kufikiri na kutoa maamuzi kama wanavyotoa wao….
Mfano.
(1) Gesi haitoki Mtwara
(2) Tupo tayari kufa wote kwa ajili ya gesi
(3) Haiwezekan mitambo ya aina zote
-Kufua umeme
-Kuchakata gesi
-Kunufaisha viwanda vya Dar-es-Salaam kwa gesi yetu
-Mikataba ya gesi ya Mnazibay kufutwa ili kuanzisha mikataba iliyo na manufaa kwa Mkoa wa Mtwara na wananchi wake.
(4) Kwa nini bomba la gesi kujengwa kwa muda wa miezi 18 na bara bara kwa miaka 51 ya uhuru haimalizwi kujengwa. Je kwenye gesi kuna nini nyuma yake.?
Hiki ni kiini cha matatizo yote kwa wananchi wa mkoa wa Mtwara kuandamana na mikutano mbalimbali ya kuhamasisha kutokubali gesi kuondoka Mtwara
Nukuu za Wananchi wa Mkoa wa Mtwara/Lindi
1-Kung’olewa kwa Reli
2-Kung’olewa kwa mashine za maji Newala na kupelekwa Dodoma.
3-Kung’olewa kwa taa za kuongoza ndege uwanja wa Mtwara na kupelekwa Uwanja wa KIA Moshi
4-Kuondolewa kwa Mtwara Korido
5-Kuwekezwa kwa bandari ya Mtwara kwa muda usiojulikana inaonyesha jinsi Serikali na viongozi wake wanavyohujumu Mikoa ya Kusini na wananchi wake kwa ujumla.
-Wananchi wa Mkoa wa Mtwara na Lindi wamefikia ukomo sasa wa kutengwa kimaendeleo, kimazingira na kutendewa uonevu wa makusudi na kilio chao cha mwisho ni hiyo gesi ambayo kauli mbiu yao ni GESI HAITOKI MTWARA KWA BOMBA KWENDA KINYEREZI DAR-ES-SALAAM.
-Wananchi wote wameungana juu ya kuitetea gesi kutoka Mtwara, badala yake Serikali ifuate mikataba ya kwanza inayohusu gesi ya Mtwara pamoja na Ilani ya uchaguzi ya CCM ifuatwe na Rais atekeleze ahadi zote alizotoa hapo kwanza na afute kauli yake ya kupeleka gesi Kinyerezi, na wala Serikali isitumie nguvu katika swala zima la gesi ya Mnazibay Mtwara.
TAMKO LA UMOJA WA MAKANISA YA KIPENTEKOSTE –P.C.T MKOA WA MTWARA
1. P.C.T kwa kuzingatia mwono uliopo wa hali tete yenye mwelekeo wa kumwagika damu na kuigawa nchi vipande vipande na kuondokewa amani, yafuatayo yafanyike
• Serikali isitishe mpango wake wa kuondoa gesi kutoka Mnazi bay Mtwara kwa kuisafirisha kwenda Kinyerezi Dar –es Salaam kwa bomba.
• Mitambo ya kuchakata gesi ijengwe Mtwara ili gesi isafirishwe kama mazao ya gesi na mabaki yake kutumiwa katika viwanda vya mbolea na plastic.
• Mitambo ya kuzalisha umeme ijengwe Mtwara na kusafirisha umeme na kuunganisha gridi ya Taifa.
• Viwanda vilivyoahidiwa vya mbolea,plastic,cemet n.k vianze kujengwa sasa na isiwe propaganda tu ya kisiasa toka kwa viongozi kwa kuondoa dhana iliyotokea huko nyuma ya kuonekana Kusini ni ukanda wa vita usiendelezwe.
Mfano kule Kilwa Lindi ambako ahadi ya kujenga kiwanda cha mbolea kwa gesi ya Songo songo mpaka leo hakijajengwa kwa kuwapatia nafasi ya ajira na kujiajiri kutokana na viwanda hivyo
• Serikali iwe sikivu kwa kilio cha muda mrefu cha wananchi wa Mikoa ya Mtwara na Lindi ambako vyanzo vya uchumi wa gesi vipo kwa kutekeleza madai yao, kwa kuwa hawapingi kupelekwa umeme gridi ya Taifa na kuuza gesi iliyochakatwa tayari kwa kuliingizia Taifa mapato.
• Serikali ikamilishe sera za gesi na mafuta na kupatikana sheria ambayo italinda mikataba yote inayofanywa na serikali juu ya gesi na kulinda wananchi wa eneo husika mikoa ya Mtwara na Lindi kwa madhara yanayotokana na gesi kwa kuwashirikisha kutoa mawazo yao.
• Mazungumzo yafanyike kati ya Serikali na wananchi katika kupata ufumbuzi wa swala la gesi kwa njia ya Amani na wala isitumie nguvu zilizonazo kwani kufanya hivyo ni kuleta maafa yasiyo ya lazima kwa Taifa.
• -Serikali isisikilize wabunge wadanganyifu ambao hawana makubaliano na wananchi katika majimbo yao wanayotoka, ambao huchochea mgogoro huu kwa lengo lao binafsi.
• Viongozi ambao wametoa matusi kwa wananchi wafute usemi wao kwa wananchi wa Mkoa wa Mtwara ambao wamewaita wahaini kwa kuwaomba radhi bila masharti yeyote kwani semi hizo huleta chuki, uhasama, na matengano katika nchi, na kusababisha nchi isitawalike.
• Serikali ya Chama Cha Mapinduzi itekeleze Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2010 Ibara 63 Kifungu H na K ambavyo vipo wazi, hasa kwa kuzingatia kuwa sera zinazotekelezwa sasa na Serikali ni zile zote zilizoandikwa kwenye Ilani ya uchaguzi.
• Serikali irudishe tumaini kwa wananchi wa Mikoa ya Kusini na amani inayoonekana kutoweka kwa matamshi yanayoashiria kumwagika kwa damu bila kujali kuwa nchi ilipatikana bila kuwaga damu.
• Serikali iwatambue wananchi wa Mikoa ya Kusini kuwa wana haki ya kutimiziwa matakwa yao kama wananchi wa mikoa mingine kwa kupata maendeleo kutokana na vyanzo vya uchumi vilivyopo katika maeneo yao.
-Sisi viongozi wa dini tunamwomba Mungu awape hekima viongozi wetu wa Serikali kwa sababu wamepewa dhamana na Mungu kuliongoza Taifa.
-Ukamilifu wao wenye haki utawaongoza, bali ukaidi wao wenye fitina utawaangamiza Methali 11:3
-Asiyemcha Mungu humpoteza jirani yake kwa kinywa chake, bali wenye haki watapona kwa maarifa. Methali 11:9
Imesainiwa na 
BISHOP C. CHILUMBA
MWENYEKITI MKOA
PAMOJA NA:-
PASTOR SELEKWA
KATIBU PCT- MKOA WA MTWARA
Nakala:
• Mwenyekiti PCT Taifa-Dar –es –Salaam
• Maaskofu na Wachungaji wote wa PCT Mkoa wa Mtwara.

Sunday, January 27, 2013

Mtikila amemtaka JK atangaze Kusitisha Mradi wa gas

TAARIFA YA DEMOCRATIC PARTY (DP) KUHUSU

GESI NA MASLAHI YA MTWARA CORRIDOR
DP tunatoa tahadhari kwamba hali inayoendelea kuwa mbaya huko Kusini mwa Nchi yetu, inazidishwa na ukosefu mkubwa wa uzalendo na hekima katika utawala wa juu wa CCM, kiasi cha kuzidi kuumwagia gesi moto unaowaka badala ya kutumia historia ya tatizo lenyewe ambayo peke yake ndiyo inayoweza kuwapa busara ya zimamoto! Tunapenda ieleweke kuwa madai kwamba umeme wa gesi hiyo ufuliwe kule kule Kusini yanatoka katika uchungu wa wananchi wote wa Kusini mwa Tanganyika yaani Mtwara Corridor, uchungu wa kudhulumiwa, kudhalilishwa na kusahauliwa kabisa kimaendeleo tangu tulipotapata uhuru mpaka leo. Serikali ndiyo chombo hasa cha kuzungushia gurudumu la maendeleo, ambalo lilielekezwa Kaskazini tu mpaka Kusini kukabaki pori na giza nene, kiasi kwamba watumishi wa umma walipokuwa wanapangiwa kufanya kazi Kusini, mara nyingi ikiwa kama adhabu, waliamua kuacha kazi. Kupuuza upande mmoja wa nchi kimaendeleo huwa ni bomu la hatari litakaloteketeza hapo baadaye, kama inavyokuwa hivi leo Wananchi wa Mtwara Corridor wanafahamu kwamba sumaku ya wawekezaji wa miradi mikubwa ya kuwaletea maendeleo ni nishati na miundombinu, lakini watawala wa CCM waliwanyang’anya Reli ya Kusini kwa uharamia wa kung’oa mpaka mataruma na kufutilia mbali hata na tuta lenyewe! Wananchi wa Kusini ni binadamu wanaoumia kwamba hata barabara ya kuwaunganisha na dunia nyingine haijaisha mpaka leo, lakini wanayaona makufuru ya ufujaji wa kutisha wa serikali ya CCM hiyo hiyo wa mabarabara ya Jijini Dar es Salaam sasa kukwanguliwa lami nzuri kabisa ya mabilioni ya fedha, ambayo ingeishi zaidi ya miaka saba mingine! Serikali ndiyo yenye jukumu la kuweka misingi yote ya uchumi wa nchi, kwa ajili ya maendeleo ya Taifa na maisha bora ya wananchi wenyewe, lakini mbali ya ule uharamia wa kuwang’olea ile reli, fungu la uboreshaji wa Bandari ya Mtwara ambayo ndiyo yenye kina kikubwa zaidi cha asili kinachofaa zaidi kuliko hata bandari ya Dar es Salaam, sasa ni fungu la kujengea bandari ya Bagamoyo nyumbani kwa Kikwete, ambapo ni hatua kadhaa tu jirani ya Dar es Salaam! Zao la pamba ambalo utawala wa mkoloni ulilijengea msingi imara kwa ajili ya uchumi wa nchi na wananchi wake, lilishamiri vizuri zaidi Kusini kama ulivyoshamiri hata mkonge. Lakini kwa kutowathamini watu wa Kusini na kutojali kabisa hatima yao kiuchumi na kimaisha, utawala wa CCM uliyanyima mazao hayo kipaumbele kule na hata ule msukumo unaopasa, wakati kule Kaskazini mwa nchi hiyo hiyo umeme ulisha sambazwa mpaka migombani!
Zao la korosho lililobaki angalau katika uwezo wao ulio duni, limekuwa kama mnyororo wa utumwa, kwa sababu wakivuna hawapati kitu bali kupunjwa kabisa bei kama zikinunuliwa. Ni zao linalotajirisha sana ma--------- kwa kuwakondesha vibaya sana walalahoi wa Kusini.
KUHUJUMIWA KWA MAONO YA SHUJAA OSCAR KAMBONA
Watu wa Mtwara Corridor wanafahamu kwamba shujaa Oscar Kambona ndiye hasa aliyefanikiwa kuiombea Nchi yetu msaada wa China wa Reli ya Uhuru, na uwezo wake wa kisiasa na hasa baada ya kung’ara katika ukombozi wa Afrika na uhusiano wake binafsi na Chou en Lai ulivyotusaidia. Tunajua kwamba kwa ajili ya hazina za Taifa letu za mafuta na gesi kule Kusini, pamoja na rutuba isiyo kawaida kwa ajili ya kilimo, pamoja na raslimali za madini ya thamani njia yote, achilia mbali wanyamapori Selous, na chuma cha Liganga na mkaa wa mawe Mchuchuma, reli hiyo ilikuwa ianzie Bandari ya Mtwara iliyopangiliwa pia uboreshwaji wa nguvu, na ilikuwa iende mpaka Ziwa Nyasa baada ya kona ile ya kwenda Liganga na Mchuchuma hadi Rukwa kwenye shaba. Hauwezi kusahaulika ushuhuda kwamba baada ya shujaa Kambona kuelezea baraza la mawaziri mafanikio haya ya safari yake China, na hasa Bandari ya Mtwara na reli ya uhuru wetu wa kiuchumi, alitukanwa na mkuu wake kwamba ni mkabila sana, kwa ‘kosa’ la kutaka hiyo miundombinu ya bandari na reli iwe Kusini! Mzalendo Oscar Kambona alijitetea kwa hekima ya rohoni kiasi cha kuwatoa machozi baadhi ya wenzake kwamba, “Mimi si mkabila wala sina kosa, kama kuna mwenye makosa basi ni Mwenyezi Mungu”. Alipotakiwa aeleze ana maana gani alisema, ‘Kwa sababu Mungu angetuwekea kule Kilimanjaro au Musoma hizi hazina za gesi, mafuta, madini ya thamani na Selous ya wanyamapori, chuma na mkaa wa mawe na shaba reli ingepita, lakini sasa alikosea akaweka Kusini. Hakuna mwehu wa kubisha kwamba maono haya ya hayati Oscar Kambona yalikuwa ya uzalendo wa hali ya juu kwa ajili si ya watu wa Kusini, bali kwa muujiza wa maendeleo ya kiuchumi ya Taifa la wana wa Tanganyika kuwa katika kilele cha Afrika na hata dunia. Hatushangai kwamba ingawa shujaa Oscar Kambona ndiye aliyeanzisha Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), kwa maono yake binafsi ambayo Nyerere ilibidi ayaafiki, Kambona akayauza kwa rafiki yake mpenzi Ahmed Sekou Toure aliyempa cheki tupu ya kwanza, wakamhusisha shujaa Kwame Nkurumah aliyetoa cheki ya pili, na walipomshirikisha Mfalme Haile Selasie naye akatoa cheki ya tatu, shujaa Oscar Kambona akaupambisha moto wa ukombozi wa Afrika, mpaka wivu ulipompiga vita kali hadi akaikimbia Nchi yake. Ni dhahiri kwamba watu wa Kusini ya Tanganyika au Mtwara Corridor walikuwa na sababu ya kumpenda na kumheshimu hayati Oscar Kambona, kwa sababu maono yake kwa ajili ya hatima ya Taifa letu yalikuwa baraka kwao. Lakini hakuna hata choo ya Jiji iliyoweza kuitwa jina la shujaa Oscar Kambona, licha ya sifa na heshima aliyoiletea Nchi yetu, hii ni aibu! Nyerere alipogeuka kuwa adui mkuu wa shujaa Oscar Kambona watu wengi wa Kusini waliteseka kwa ajili hiyo, na koroboi ya maendeleo Kusini ilionekana kuzimika kiaina, hadi ilipoibuliwa upya na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) mikakati mipya ya maendeleo ya Kusini, kwa jina la Mtwara Corridor, iliyofanyiwa kazi kwa dhati na mzalendo Simbakalia ambaye sasa ndiye Mkuu wa Mkoa wa Mtwara. Koroboi hiyo ikazimika tena alipoondolewa huyu kutoka NDC.
UFUMBUZI WA MOTO WA HASIRA ULIOLIPUKA KUSINI
Moto huu usipozimishwa kwa hekima ya hali ya juu, si ajabu ukaimeza mikoa yote ya Kusini yaani Mtwara, Lindi, Ruvuma, Mbeya, Iringa, Morogoro na hata Rukwa, tukakuta yanazaliwa mataifa mawili mpaka ukiwa Reli ya Kati! Tumeeleza kwa kifupi sana historia na sababu za msingi za hasira za watu wa Kusini, kwamba wao pia ni binadamu, na kwamba lugha yao ya amani ilipuuzwa kwa miaka yote 52 tangu nchi yetu ilipopata uhuru. Lakini tunapinga propaganda za uwongo za watawala waliosababisha hasira hii, kwa ukweli kwamba: 1. Watu wa Kusini hawazuii gesi isitoke kwa sababu ni nyingi sana na hazina yetu ni ya pili duniani kwa uwingi. Wao wanataka umeme ufuliwe kule kule kwa sababu utaleta mapinduzi ya maendeleo kule. 2. Faida ya pili ni kwamba nyaya zitakazo zoubeba umeme kuupeleka mpaka Kenya na Uganda tukitaka, lazima njia nzima zitakuwepo transfoma za kuusambaza mpaka miisho yote ya nchi mpaka vitongoji vyote. Kwahiyo wananchi wa Kusini ndio wazalendo na siyo watawala wa CCM. 3. Wanataka mabomba ya gesi yaanze kuisafirisha baada ya kufuliwa umeme, ili na yenyewe pia humo njiani yachomekwe mabomba yatakayoieneza nchini kote, kusudi iwe nishati mbadala ya Taifa kwa ajili ya kuiokoa miti yetu kwa ajili ya vizazi vyetu vyote vijavyo. Mungu ametuzibulia hazina ya gesi wakati nchi yetu inaelekea kuwa jangwa kutokana na kuteketezwa miti yote kwa kutumiwa kama nishati. Hawa ndio wazalendo na siyo watawala wa CCM. 4. Ukweli kwamba ufisadi wa kutisha umetembea katika mikakati hiyo ya kuufulia hapa Jijini umeme wa gesi ya Kusini, hivyo kwamba kiburi cha watawala na kutojali maslahi ya Taifa kama umeme utafuliwa kule kule Kusini, ni kwa sababu mafisadi hawana jinsi kwavile mabilioni ya watu walishakula sehemu kubwa, na sasa wanatafuta kulazimisha ili wapate lile fungu nono la mwisho. Saa ya ukombozi ni sasa! Njia pekee ya kuzimisha moto huu kule Kusini na kurejesha amani ni Rais Jakaya Kikwete kutoa Tamko la kukubali kufuliwa umeme kule kule Kusini kwa sababu ni kwa maslahi ya Taifa. DP tupo tayari kufanya usuluhishi kama kutakuwepo uwazi kwa upade wa serikali, kwa ajili ya hatima ya Nchi yetu. Rais Jakaya Kikwete analazimika pia kutamka bayana kipaumbele kwa ubereshaji wa Bandari kuu ya Mtwara, ikibidi hata kwa kusitisha mradi wa Bandari ya Bagamoyo. Hii ni kwa maslahi ya Taifa letu. Rais Jakaya Kikwete anapaswa kutamka bayana kuhusu ukamilishaji wa barabara ya Kusini.
Rais Kikwete anakabiliwa na utanguaji wa ufisadi wote uliofanyika Mtwara Corridor mpaka Ludewa kwenye miradi ya Chuma cha Liganga na Mkaa wa mawe Mchuchuma. Saa ya ukombozi ni sasa! Mchungaji C. Mtikila, Mwenyekiti0713 430516

Mtikila amemtaka JK atangaze Kustisha Mradi wa gas Mtwara mara moja Press Leo Traventne Hotel Dar!!!


Mch Mtikila amekusudia kutoa tamko leo saa tano asubuhi, Hotel Traventine la kumtaka Rais Kikwete atangaze Kusitishwa kwa mradi wa Kusafirisha gas Kutoka Mtwara kuja Dar Mara moja ili kudumisha amani Mtwara!!!.Asipofanya hivyo ipo hatari mapinduzi ya utawala wake yaka anzia Mtwara.

Update: Mtikila ameshatoa Tamko:
TAARIFA YA DEMOCRATIC PARTY (DP) KUHUSU
GESI NA MASLAHI YA MTWARA CORRIDOR
DP tunatoa tahadhari kwamba hali inayoendelea kuwa mbaya huko Kusini mwa Nchi yetu, inazidishwa na ukosefu mkubwa wa uzalendo na hekima katika utawala wa juu wa CCM, kiasi cha kuzidi kuumwagia gesi moto unaowaka badala ya kutumia historia ya tatizo lenyewe ambayo peke yake ndiyo inayoweza kuwapa busara ya zimamoto! Tunapenda ieleweke kuwa madai kwamba umeme wa gesi hiyo ufuliwe kule kule Kusini yanatoka katika uchungu wa wananchi wote wa Kusini mwa Tanganyika yaani Mtwara Corridor, uchungu wa kudhulumiwa, kudhalilishwa na kusahauliwa kabisa kimaendeleo tangu tulipotapata uhuru mpaka leo. Serikali ndiyo chombo hasa cha kuzungushia gurudumu la maendeleo, ambalo lilielekezwa Kaskazini tu mpaka Kusini kukabaki pori na giza nene, kiasi kwamba watumishi wa umma walipokuwa wanapangiwa kufanya kazi Kusini, mara nyingi ikiwa kama adhabu, waliamua kuacha kazi. Kupuuza upande mmoja wa nchi kimaendeleo huwa ni bomu la hatari litakaloteketeza hapo baadaye, kama inavyokuwa hivi leo Wananchi wa Mtwara Corridor wanafahamu kwamba sumaku ya wawekezaji wa miradi mikubwa ya kuwaletea maendeleo ni nishati na miundombinu, lakini watawala wa CCM waliwanyang’anya Reli ya Kusini kwa uharamia wa kung’oa mpaka mataruma na kufutilia mbali hata na tuta lenyewe! Wananchi wa Kusini ni binadamu wanaoumia kwamba hata barabara ya kuwaunganisha na dunia nyingine haijaisha mpaka leo, lakini wanayaona makufuru ya ufujaji wa kutisha wa serikali ya CCM hiyo hiyo wa mabarabara ya Jijini Dar es Salaam sasa kukwanguliwa lami nzuri kabisa ya mabilioni ya fedha, ambayo ingeishi zaidi ya miaka saba mingine! Serikali ndiyo yenye jukumu la kuweka misingi yote ya uchumi wa nchi, kwa ajili ya maendeleo ya Taifa na maisha bora ya wananchi wenyewe, lakini mbali ya ule uharamia wa kuwang’olea ile reli, fungu la uboreshaji wa Bandari ya Mtwara ambayo ndiyo yenye kina kikubwa zaidi cha asili kinachofaa zaidi kuliko hata bandari ya Dar es Salaam, sasa ni fungu la kujengea bandari ya Bagamoyo nyumbani kwa Kikwete, ambapo ni hatua kadhaa tu jirani ya Dar es Salaam! Zao la pamba ambalo utawala wa mkoloni ulilijengea msingi imara kwa ajili ya uchumi wa nchi na wananchi wake, lilishamiri vizuri zaidi Kusini kama ulivyoshamiri hata mkonge. Lakini kwa kutowathamini watu wa Kusini na kutojali kabisa hatima yao kiuchumi na kimaisha, utawala wa CCM uliyanyima mazao hayo kipaumbele kule na hata ule msukumo unaopasa, wakati kule Kaskazini mwa nchi hiyo hiyo umeme ulisha sambazwa mpaka migombani!
Zao la korosho lililobaki angalau katika uwezo wao ulio duni, limekuwa kama mnyororo wa utumwa, kwa sababu wakivuna hawapati kitu bali kupunjwa kabisa bei kama zikinunuliwa. Ni zao linalotajirisha sana ma--------- kwa kuwakondesha vibaya sana walalahoi wa Kusini.
KUHUJUMIWA KWA MAONO YA SHUJAA OSCAR KAMBONA
Watu wa Mtwara Corridor wanafahamu kwamba shujaa Oscar Kambona ndiye hasa aliyefanikiwa kuiombea Nchi yetu msaada wa China wa Reli ya Uhuru, na uwezo wake wa kisiasa na hasa baada ya kung’ara katika ukombozi wa Afrika na uhusiano wake binafsi na Chou en Lai ulivyotusaidia. Tunajua kwamba kwa ajili ya hazina za Taifa letu za mafuta na gesi kule Kusini, pamoja na rutuba isiyo kawaida kwa ajili ya kilimo, pamoja na raslimali za madini ya thamani njia yote, achilia mbali wanyamapori Selous, na chuma cha Liganga na mkaa wa mawe Mchuchuma, reli hiyo ilikuwa ianzie Bandari ya Mtwara iliyopangiliwa pia uboreshwaji wa nguvu, na ilikuwa iende mpaka Ziwa Nyasa baada ya kona ile ya kwenda Liganga na Mchuchuma hadi Rukwa kwenye shaba. Hauwezi kusahaulika ushuhuda kwamba baada ya shujaa Kambona kuelezea baraza la mawaziri mafanikio haya ya safari yake China, na hasa Bandari ya Mtwara na reli ya uhuru wetu wa kiuchumi, alitukanwa na mkuu wake kwamba ni mkabila sana, kwa ‘kosa’ la kutaka hiyo miundombinu ya bandari na reli iwe Kusini! Mzalendo Oscar Kambona alijitetea kwa hekima ya rohoni kiasi cha kuwatoa machozi baadhi ya wenzake kwamba, “Mimi si mkabila wala sina kosa, kama kuna mwenye makosa basi ni Mwenyezi Mungu”. Alipotakiwa aeleze ana maana gani alisema, ‘Kwa sababu Mungu angetuwekea kule Kilimanjaro au Musoma hizi hazina za gesi, mafuta, madini ya thamani na Selous ya wanyamapori, chuma na mkaa wa mawe na shaba reli ingepita, lakini sasa alikosea akaweka Kusini. Hakuna mwehu wa kubisha kwamba maono haya ya hayati Oscar Kambona yalikuwa ya uzalendo wa hali ya juu kwa ajili si ya watu wa Kusini, bali kwa muujiza wa maendeleo ya kiuchumi ya Taifa la wana wa Tanganyika kuwa katika kilele cha Afrika na hata dunia. Hatushangai kwamba ingawa shujaa Oscar Kambona ndiye aliyeanzisha Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), kwa maono yake binafsi ambayo Nyerere ilibidi ayaafiki, Kambona akayauza kwa rafiki yake mpenzi Ahmed Sekou Toure aliyempa cheki tupu ya kwanza, wakamhusisha shujaa Kwame Nkurumah aliyetoa cheki ya pili, na walipomshirikisha Mfalme Haile Selasie naye akatoa cheki ya tatu, shujaa Oscar Kambona akaupambisha moto wa ukombozi wa Afrika, mpaka wivu ulipompiga vita kali hadi akaikimbia Nchi yake. Ni dhahiri kwamba watu wa Kusini ya Tanganyika au Mtwara Corridor walikuwa na sababu ya kumpenda na kumheshimu hayati Oscar Kambona, kwa sababu maono yake kwa ajili ya hatima ya Taifa letu yalikuwa baraka kwao. Lakini hakuna hata choo ya Jiji iliyoweza kuitwa jina la shujaa Oscar Kambona, licha ya sifa na heshima aliyoiletea Nchi yetu, hii ni aibu! Nyerere alipogeuka kuwa adui mkuu wa shujaa Oscar Kambona watu wengi wa Kusini waliteseka kwa ajili hiyo, na koroboi ya maendeleo Kusini ilionekana kuzimika kiaina, hadi ilipoibuliwa upya na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) mikakati mipya ya maendeleo ya Kusini, kwa jina la Mtwara Corridor, iliyofanyiwa kazi kwa dhati na mzalendo Simbakalia ambaye sasa ndiye Mkuu wa Mkoa wa Mtwara. Koroboi hiyo ikazimika tena alipoondolewa huyu kutoka NDC.
UFUMBUZI WA MOTO WA HASIRA ULIOLIPUKA KUSINI
Moto huu usipozimishwa kwa hekima ya hali ya juu, si ajabu ukaimeza mikoa yote ya Kusini yaani Mtwara, Lindi, Ruvuma, Mbeya, Iringa, Morogoro na hata Rukwa, tukakuta yanazaliwa mataifa mawili mpaka ukiwa Reli ya Kati! Tumeeleza kwa kifupi sana historia na sababu za msingi za hasira za watu wa Kusini, kwamba wao pia ni binadamu, na kwamba lugha yao ya amani ilipuuzwa kwa miaka yote 52 tangu nchi yetu ilipopata uhuru. Lakini tunapinga propaganda za uwongo za watawala waliosababisha hasira hii, kwa ukweli kwamba: 1. Watu wa Kusini hawazuii gesi isitoke kwa sababu ni nyingi sana na hazina yetu ni ya pili duniani kwa uwingi. Wao wanataka umeme ufuliwe kule kule kwa sababu utaleta mapinduzi ya maendeleo kule. 2. Faida ya pili ni kwamba nyaya zitakazo zoubeba umeme kuupeleka mpaka Kenya na Uganda tukitaka, lazima njia nzima zitakuwepo transfoma za kuusambaza mpaka miisho yote ya nchi mpaka vitongoji vyote. Kwahiyo wananchi wa Kusini ndio wazalendo na siyo watawala wa CCM. 3. Wanataka mabomba ya gesi yaanze kuisafirisha baada ya kufuliwa umeme, ili na yenyewe pia humo njiani yachomekwe mabomba yatakayoieneza nchini kote, kusudi iwe nishati mbadala ya Taifa kwa ajili ya kuiokoa miti yetu kwa ajili ya vizazi vyetu vyote vijavyo. Mungu ametuzibulia hazina ya gesi wakati nchi yetu inaelekea kuwa jangwa kutokana na kuteketezwa miti yote kwa kutumiwa kama nishati. Hawa ndio wazalendo na siyo watawala wa CCM. 4. Ukweli kwamba ufisadi wa kutisha umetembea katika mikakati hiyo ya kuufulia hapa Jijini umeme wa gesi ya Kusini, hivyo kwamba kiburi cha watawala na kutojali maslahi ya Taifa kama umeme utafuliwa kule kule Kusini, ni kwa sababu mafisadi hawana jinsi kwavile mabilioni ya watu walishakula sehemu kubwa, na sasa wanatafuta kulazimisha ili wapate lile fungu nono la mwisho. Saa ya ukombozi ni sasa! Njia pekee ya kuzimisha moto huu kule Kusini na kurejesha amani ni Rais Jakaya Kikwete kutoa Tamko la kukubali kufuliwa umeme kule kule Kusini kwa sababu ni kwa maslahi ya Taifa. DP tupo tayari kufanya usuluhishi kama kutakuwepo uwazi kwa upade wa serikali, kwa ajili ya hatima ya Nchi yetu. Rais Jakaya Kikwete analazimika pia kutamka bayana kipaumbele kwa ubereshaji wa Bandari kuu ya Mtwara, ikibidi hata kwa kusitisha mradi wa Bandari ya Bagamoyo. Hii ni kwa maslahi ya Taifa letu. Rais Jakaya Kikwete anapaswa kutamka bayana kuhusu ukamilishaji wa barabara ya Kusini.
Rais Kikwete anakabiliwa na utanguaji wa ufisadi wote uliofanyika Mtwara Corridor mpaka Ludewa kwenye miradi ya Chuma cha Liganga na Mkaa wa mawe Mchuchuma. Saa ya ukombozi ni sasa! Mchungaji C. Mtikila, Mwenyekiti0713 430516

Zitto alipuka, amtaka JK aende Mtwara

Ifuatayo ni kauli ya Zitto Kabwe katika mkutano wake na waandishi wa habari Dar es Salaam, leo. Chini yake kuna kauli ya Ikulu iliyowahi kutolewa pia katika vyombo vya habari Oktoba mwaka juzi Katika kulinganisha kauli hizi mbili, Zitto anaona serikali inajikanganya, na inatafuta wachawi wa mgogoro wa Mtwara, badala ya kutafuta suluhu. Zisome mwenyewe.
 
 
 
 
 
TAARIFA YA NDUGU ZITTO KABWE (MB) KUHUSU YANAYOENDELEA

MTWARA NA MRADI WA BOMBA LA GESI ASILIA

 

Serikali iache kutafuta mchawi, iende Mtwara

 

Katika kipindi cha wiki nne sasa kumekuwa na maandamamo, malumbano na vurugu kuhusu mradi wa kujenga bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam. Mradi huu wa kutandaza bomba la urefu wa kilometa 542 ni mkubwa sana hapa nchini, na una thamani kubwa zaidi kuliko miradi mingine yote  ya miundombinu iliyopata kutokea hapa nchini. Mradi huu utajengwa kwa mkopo wa dola za Kimarekani 1.2 bilioni kutoka Benki ya Exim ya China.

 

Wananchi wa Mtwara kupitia maandamano ya tarehe 27 Desemba 2012 wametaka kujua hatma ya maendeleo ya mikoa wa kusini kutokana na mradi huu wa bomba la gesi. Serikali imewajibu wananchi hawa kwa kuwaita wahaini, watu hatari na wasio elewa. Imefika mahali inapotosha madai yao kwamba hawataki gesi itoke Mtwara.

 

Kimsingi Serikali haijajibu hoja yeyote ya msingi ya wananchi wa Mtwara kuhusu mradi wa kusafirisha gesi. Badala yake imekuwa ikijaribu kupotosha madai ya watu wa Mtwara kupitia mikutano na vyombo vya habari.

 

Tangu maandamano haya yatokee, na baadaye mikutano ya hadhara na
hatimaye matukio ya kusikitisha ya kuharibu mali za watu, mauaji ya
watu na majeruhi mbalimbli, Serikali na hasa Wizara yenye dhamana ya
mradi huu, imekuwa ikitoa matamko kwenye vyombo vya habari badala ya
kwenda Mtwara kuzungumza na wananchi, kusikiliza madai yao na kuona
namna ya kutekeleza madai hayo. Kutokana na Serikali kutofanya hivyo,
kusikiliza na kuzungumza na wananchi wa Mtwara, vurugu mbaya sana zimeendelea mkoani humo.


Mwezi uliopita, Desemba 2012, tatizo lilionekana kuwa ndogo na lenye kuhusiana zaidi na ukosefu wa kushirikishwa kwa wananchi. Badala ya kushughulikia
tatizo likiwa bado ndogo, Serikali imeona njia pekee ya kushughulikia suala hili ni kutafuta mchawi na kwa wiki zote hizi imekuwa ikisemakuwa wanasiasa na makampuni ya uwekezaji ya nje yanachochea mgogoro

huu.

 

Leo hali iliyopo mkoani Mtwara inasikitisha sana, maana mali za wananchi zinaharibiwa, nyumba zinachomwa moto na watu wanapoteza maisha. Tunalaani matukio haya kwa nguvu zetu zote, maana kinachotokea Mtwara si Utanzania. Tusipowasikiliza wananchi na kutatua mgogoro huu kwa kuwashirikisha, hali itazidi kuzorota wakati tukitupiana lawama.

 

Hivi sasa serikali imeona njia pekee ya kushughulikia suala hili ni kutafuta mchawi na kwa wiki zote hizi imekuwa ikisema kuwa wanasiasa na makampuni ya uwekezaji ya nje yanachochea mgogoro huu.

 

Kwanza, Serikali imekuwa ikiaminisha umma kwanza suala hili limechukuliwa kisiasa. Pili, Serikali imekuwa ikirudia kusema kuwa baadhi ya makampuni ya uwekezaji nchini na mataifa ya Magharibi yamekuwa yakichochea wananchi wa Mtwara.

 

Katika mwendelezo wa mtindo wa Serikali wa ‘management by press conferences’ jana Jumamosi Naibu Waziri wa Nishati na Madini ndugu George Simbachawene aliwaambia wahariri kwamba mimi Zitto Kabwe ninachochea wananchi wa Mtwara, ninatumiwa, na si mzalendo. Vile vile alitoa vielelezo kadhaa kuonyesha kuwa mradi wa kujenga bomba la gesi ni gharama sawasawa. Akasisitiza kwamba mimi ni mwongo.

 

Katika kipindi chote cha mgogoro wa Gesi Mtwara, sijafika Mtwara. Sijafanya mkutano wowote na waandishi zaidi ya kuandika mawazo yangu, kama Mtanzania kuhusu suala hili.

 

Nimeandika makala nne na zimechapishwa katika magazeti kadhaa hapa nchini na kwenye blogu yangu (www.zittokabwe.com).

 


 

Sitaki kubishana na Naibu Waziri ama Kiongozi yeyote ya Serikali kwa sasa. Hatuwezi kuendelea kulumbana, kuzozana, kuzodoana na kurushiana maneno wakati nchi yetu inaungua. Huu sio wakati wa kutafuta mchawi bali kutafuta majawabu ya changamoto zilizopo mbele yetu.

 

Yanayotokea Mtwara ni fundisho kwetu kwa Taifa namna ya kukabili changamoto za utajiri wa rasilimali, ili kuweka mkakati, mambo haya yanayotokea Mtwara yasitokee tena Tanzania. Tutaweza kuzuia maafa haya iwapo tutaweka uwazi katika mikataba, tutashirikisha wananchi kwenye unyonyaji wa maliasili za nchi, na iwapo tutaweka uwajibikaji.

 

 

Rais Kikwete Kikwete ana majibu; ayatoe sasa kwa wana Mtwara

 

Kwa mujibu wa Mpango Kabambe wa Umeme nchini (Power System Master Plan), kulikuwa na mradi wa kufua umeme MnaziBay, ambao Rais Jakaya Kikwete aliagiza utekelezwe mara moja. Serikali ieleze umma kuhusu mradi huo wa kujenga kituo cha kufua umeme 300MW MnaziBay Mtwara na kujenga msongo wa umeme wa 300KV mpaka Singida. Umeishia wapi? Ikumbukwe kuwa mnamo tarehe 12 Oktoba 2012, Rais Jakaya Kikwete alipokea ripoti ya ujenzi wa mradi huu kutoka makampuni ya China National Machinery & Equipment Import & Export Corporation (CMEC) ya China na Siemens ya Ujerumani, ambayo kwa pamoja yalitarajia kujenga kituo kikubwa cha kuzalisha umeme kutokana na gesi katika eneo la Mnazi Bay, mjini Mtwara na pia kujenga njia ya kusafirisha umeme ya kilomita 1,100 kutoka Mtwara hadi Singida. Mradi huu ungegarimu dola za kimarekani milioni 684 na Rais aliagiza utekelezwe haraka sana. Huu mradi uliishia wapi? Kwa nini Serikali ipo kimya kuhusu mradi huu ambao ungejibu kabisa maswali ya watu wa Mtwara? Taarifa ya Ikulu kuhusu mradi huu imeambatanishwa hapa.

 

Tufanyeje?

 

Hapa tulipofikia ni lazima kwanza kabisa kusikia kilio cha wananchi wa Mtwara ikiwemo kuelewa madai yao. Swali kubwa kubwa la watu wa Mtwara na Kusini kwa ujumla ni ‘tunanufaikaje’? Jibu la swali hili si ahadi za miradi bali ni vitendo. Hapa ndipo serikali inaposhindwa kushughulikia suala hili, kutoelewa madai ya wananchi na kuyapotosha.Viongozi wa kisiasa wenye ushawishi kutoka pande zote, chama tawala na vyama vya upinzani, waende Mtwara kuzungumza na wananchi, lakini wawasikilize kwanza.

 

  1. Lazima viongozi tujenge utamaduni wa kusikiliza wananchi na si kuwahutubia tu. Wananchi wa Mtwara wana madai ambayo lazima viongozi tukae kitako kuwasikiliza kisha kufanya nao majadiliano ambayo yatatoa mwafaka. Rais mstaafu, Ndugu Benjamin Mkapa ameshatoa kauli kuhusu suala hili. Ni wakati mwafaka sasa kwa viogozi wengine kumuunga mkono kwa kwenda Mtwara na kukaa na wananchi wa Wilaya zote za Mtwara, kusikiliza hoja zao na kuona namna ya kupata ufumbuzi wa suala hili. Wakati hatua hii inachukuliwa, wananchi waombwe kutulia na kuacha vurugu za aina yeyote ile, na Serikali isimamishe mradi mpaka hapo suluhu na wananchi itakapopatikana.

 

  1. Wakati juhudi hizo zinaendelea Serikali iweke wazi mkataba wa ujenzi wa bomba, kwani ni dhahiri gharama za mradi huu ni kubwa mno kulingana na uhalisia wa miradi ya namna hii duniani kote. Katika taarifa zote kwa umma Serikali imekuwa ikisema kwamba mradi utagharimu jumla ya dola za kimarekani 1.2 bilioni, lakini katika taarifa ambayo Wizara ya Nishati na Madini imesambaza jana kwa wahariri wa vyombo vya habari nchini imesema mradi utagharimu dola za kimarekani milioni 875. Usiri katika mkataba huu unaashiria kwamba Serikali inaficha kitu. Hivyo njia pekee ni kutaka mkataba uwe wazi kwa wananchi.

 

  1. Wakati tunawataka wananchi wa Mtwara kuruhusu utulivu, ni vema Serikali ijiandae kutoa majawabu ya madai ya wananchi hao. Majawabu ya Serikali yajikite kueleza wananchi wa Mtwara wanafaidikaje na rasilimali ya gesi asilia kwa maendeleo yao. Wananchi wa Mtwara wanataka uwajibikaji wa Serikali kwenye utajiri wa nchi, na wamechoka na porojo za orodha ya miradi isiyotekelezwa.

 

Viongozi twendeni Mtwara kusikiliza wananchi wetu. Nchi inaungua na hatuwezi kuendelea kuzozana badala ya kuzima moto huu hatari kama vita vya MajiMaji. Mimi nakwenda Mtwara haraka na mara baada ya viongozi wangu wa chama kutoa ridhaa.

 

 

ZITTO KABWE

Mbunge, Kigoma Kaskazini (Chadema)

Waziri Kivuli wa Fedha

Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni


KAULI YA IKULU


• Mradi kabambe wa umeme kujengwa
• Rais Kikwete apokea ripoti ya maandalizi
• Utagharimu mabilioni ya fedha
• Utaunganisha mikoa yote kwenye Gridi ya Taifa

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumatano, Oktoba 12, 2011, amepokea ripoti kutoka makampuni mawili ya kimataifa kuhusu Mpango Kabambe ya mradi mkubwa wa umeme ambao utaunganisha kwenye Gridi ya Taifa mikoa yote sita ambayo kwa sasa haiko kwenye gridi hiyo.

Rais Kikwete amepokea ripoti hiyo kutoka makampuni ya China National Machinery & Equipment Import & Export Corporation (CMEC) ya China na Siemens ya Ujerumani ambayo kwa pamoja yanatarajia kujenga kituo kikubwa cha kuzalisha umeme kutokana na gesi katika eneo la Mnazi Bay, mjini Mtwara na pia kujenga njia ya kusafirisha umeme ya kilomita 1,100 kutoka Mtwara hadi Singida.

Mradi huo mkubwa wa umeme wa megawati 300 utakaogharimu karibu dola za Marekani milioni 684 na utakaozalisha umeme wa moja kwa moja na wenye nguvu kubwa ya 300 kV (300 kV High Voltage Direct Current – HVDC) utagharimiwa kwa pamoja na mkopo kutoka Benki ya Exim ya China na Serikali ya Tanzania.

Umeme kutokana na mradi huo utaunganishwa kwenye gridi ya taifa na kutoka Singida hatimaye utavutwa kupelekwa katika mikoa ya Kaskazini Magharibi mwa Tanzania ya Kagera, Kigoma na Rukwa ambako pia utaongeza upatikanaji wa umeme katika machimbo ya madini yaliyoko katika mikoa hiyo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mbali na mikoa hiyo mitatu, pia mikoa ya Lindi na Mtwara ambayo nayo haiko katika Gridi ya Taifa nayo itaunganishwa katika Gridi hiyo kupitia umeme huo.

Kuunganishwa kwa mikoa hiyo sita katika Gridi ya Taifa kupitia umeme wa mradi huo pamoja na Mkoa wa Ruvuma ambao utaunganishwa katika Gridi hiyo kwa mradi unaogharimiwa na Serikali ya Sweden kutakamilisha mpango wa Serikali ya Awamu ya Nne kuunganisha mikoa yote ya Tanzania kwenye umeme wa Gridi ya Taifa.

Kwa sasa Mkoa wa Kagera unahudumiwa na umeme kutoka Uganda, wakati Mikoa ya Kigoma na Rukwa inahudumiwa na umeme wa mafuta ya dizeli. Mikoa ya Mtwara na Lindi inapata umeme wake kutoka kampuni ya Wentworth ambao haujaunganishwa kwenye gridi ya taifa.

Kuunganisha mikoa yote ya Tanzania kwenye Gridi ya Taifa ilikuwa moja ya ahadi kubwa zilizotolewa na Serikali ya Rais Kikwete wakati anaingia maradakani na kwa kuuunganisha mikoa hiyo sita kwenye Gridi hiyo, Serikali hiyo itakuwa imetimimiza ahadi hiyo.

Akipokea ripoti hiyo, Rais Kikwete ameishukuru Wizara ya Fedha, Wizara ya Nishati na Madini pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa juhudi zao zilizofanikisha makubaliano ya kujengwa kwa mradi huo mkubwa wa umeme ambao utachangia kuongeza wingi wa umeme nchini katika kipindi ambacho kwa miezi kadhaa Tanzania imekabiliwa na mgawo wa umeme kutokana na ukame uliokausha maji kwenye mabwawa makubwa ya uzalishaji umeme nchini.

Rais Kikwete pia ameitaka Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Benki ya EXIM ya China kuhakikisha kuwa fedha za kutekeleza mradi huo zinapatikana haraka iwezekanavyo na pia ameitaka TANESCO na makampuni ya CMEC na Siemens baada ya kupatikana kwa fedha kuanza ujenzi wa mradi huo kwa kasi na kuukamilisha katika muda na ubora unaotarajiwa.

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu
DAR ES SALAAM.

12 Oktoba, 2011

CHADEMA Ianzishe mabadiliko ya Ndani; Vinginevyo kuiondoa CCM 2015 ni ndoto

Na M. M. Mwanakijiji

Kama kuna vitu vya kusikitisha na wakati mwingine kukatisha tamaa ni mgongano ambao umekuwa ukifukuta kwa muda ndani ya CHADEMA kiasi cha kuwa kama doa chafu ambalo halipaswi kuvumilika. Mambo ambayo yametokea Arusha, Mwanza, Mbeya na sasa BAVICHA yanaashiria kuwa kama CDM haitaamua kujiangalia ndani na kuanzisha mabadiliko ya mfumo na muundo wake basi kuiangusha CCM na kuiondoa madarakani mwaka 2015 itakuwa ni ndoto ya kutamania tu lakini kamwe haitatokea.

Migongano hii ambayo imeishia katika watu kutimuana na kutuhumiana imesababisa watu kuzungumzia migogoro ndani ya chama kuliko maono yake kwa taifa. Wiki hizi chache zilizopita zimesababisha mazungumzo mengi ndani ya CDM na nje yake yawe ni kuhusiana na kundi la vijana ambao walituhumiwa kuendesha uasi ndani ya chama kuliko kuzungumzia mipango ya CDM kushika dola. Tumeshuhudia kwa masikitiko makubwa wale wanaoitwa wapiganaji wakitumia muda mwingi kupigana wenyewe kwa wenyewe na sisi ambao tuko kwenye mitandao ya kijamii tumeshuhudia siyo tu kurushiana risasi bali mishale, visu, misumari, mawe na ndoana! Inaudhi, inasikitisha na inaacha maswali mengi kweli.


Tushukuru Mungu CHADEMA haikushinda uchaguzi mkuu wa 2010?

Jinsi ambavyo migogoro na milumbano ya chini kwa chini kati ya viongozi wa CDM ambayo yamefikia mahali pa kulipuana kumenifanya nibakie na swali ambalo limenikaa kichwani kwa wiki sasa; je wale waliounga mkono CDM washukuru Mungu kuwa haikushinda uchaguzi mkuu? Swali hili linakuja kwa sababu najiuliza kama CDM wangeshinda mwaka 2010 wangeunda serikali ya namna gani? Je wangeweza kuaminiana?

Je wangeweza kuunda serikali ya namna gani? Je siyo kwamba wao kwa wao wangeanza kuhujumiana na kurushiana vijembe? Kwa wale ambao tulikuwa tunafuatilia siasa za ndani ya CCM hasa baada ya kujiuzulu kwa Lowassa Februari 2008 tunakumbuka jinsi ndani ya CCM kulivyozuka malumbano ya wao kwa wao, kunyemeleana, kuchimbana na hata – tukiamini maneno ya Rais Kikwete Butiama – ilifika mahali wao kwa wao CCM wanaogopa kuachiana glasi za maji mezani kwa kuhofia kutiliana sumu. Je hili ndilo ambalo nalo lingetokea ndani ya CDM? Leo hii tunaona kuwa CCM chama chenye mifumo ya zamani na ambacho kina nyenzo nyingi za kushughulikia uasi imeshindwa kufanya hivyo je CDM ingeweza?

Tumeshuhudia pamoja na majigambo yote ya “kujivua gamba” CCM imeshindwa kujisafisha na badala yake wameamua kuvumiliana, kubebana na kulindana huku wale waliokuwa ni watuhumiwa vitendo vya ufisadi wakijipanga vizuri zaidi kuweza kuendesha kampeni ya kufa mtu kuugombea urais. Sasa kama CCM pamoja na watu wake wote mashuhuri ambao walijipambanua kuwa ni wapinga ufisadi leo si wameshindwa? Wameshindwa si kwa sababu hawakuwa na nia bali kwa sababu mgawanyo ulioko ndani yake ni zaidi ya maslahi; ni mgongano wa binafsi (personal conflict) na hauaisha na naweza kusema hautaisha hadi ama Lowassa awe Rais mwaka 2015 au akataliwe. Na akiwa Rais nina uhakika wa kutosha tu kuwa mpasuko wa CCM utakuwa ni kamili!

Sasa leo CDM ambao wanatarajiwa kuwa ndio wenye kuleta nuru mpya ya uongozi inapofika mahali wanachubuana wenyewe, hakuna nidhamu na kushindana kila siku kama wangeweza kuuchukua Urais kweli nchi ingekuwa salama? Je, kama mgongano huu ukiendelea kuvumliwa na kudharauliwa huku viongozi wakuu wa chama wakifunika vichwa vyao kama mbuni wakidai ati hakuna ‘mgongano’ ni ‘demokrasia’ kweli CDM itaweza kupambana na CCM na kushinda uchaguzi mkuu? Kama leo kina Maige wananukuliwa wakimchimba vijembe Katibu wao wa Uenezi Nape si tunaweza kukuta hay ohayo yanatokea ndani ya CDM kama ingeunda serikali ambapo baadhi ya wabunge wake au viongozi wake wangeanza kuirushia vijembe serikali yao au viongozi wao?


Mfumo wa CDM wa sasa unalea mno uzembe na viongozi wanaosumbua!

Wengi wetu tumekuwa tukilalamika sana jinsi serikali ya CCM chini ya Rais Kikwete ilivyojenga mfumo wa kubebana, kulindana na kuvumiliana kiasi kwamba hadi mtu afukuzwe kazi au aondolewe kwenye naffasi yake basi ni lazima awe amevurunda mno – awe ameboronga. Na hata akiboronga bado kuna muda mrefu sana wa mtu huyo kupewa nafasi nyingine sehemu fulani. Mfumo huu wa CCM ndio uliozaa ufisadi na matokeo yake kwa taifa ni maangamizi.

Sasa mfumo kama huo huo ukiangalia kwa karibu unaona ukifanya kazi ndani ya CDM. Ni mfumo wa kuvumiliana, kusubiriana na kutegeana. Ni mfumo ambao kwenye serikali ya CCM utasikia wanasema “mwenye ushahidi alete” wakati kwa CDM ni mfumo “kutafuta ushahidi zaidi”. Matokeo ya mifumo yote miwili ni kuwa serikali inalea viongozi wabovu, wabinafsi na hatari kwa taifa na CDM inajikuta inavumilia viongozi wabovu, wabinafsi na hatari kwa maslahi ya chama. Matokeo yake ni kuwa CDM itajikuta na yenyewe inazaa serikali dhaifu!


CDM ibadilike sasa vinginevyo ijiandae kuwa msindikizaji

Sasa ninachokisema hapa ni kuwa uongozi wa CDM usijifanye wao Mbuni; wanafichwa kichwa mchangani. Tatizo la CCM ambalo limechelewesha chama hicho kujisafisha na kuweza kubadilika ni imani kuwa kinapendwa. Na kweli wapo watu wanaoipenda CCM kama mtoto anavyompenda mzazi wake. Wapo ambao wameapa kabisa kuwa liwalo na liwe wao na CCM milele. Mapenzi ya namna hii hayajali ubovu, mapenzi ya namna hii hayajali CCM inatawalaje au inaongoza vipi. NI mapenzi ambayo ‘hayaoni wala hayasikii’. Ni sawa na mapenzi ya wapendanao wawili ambapo licha ya mausia ya watu kuwa mmoja wao ni jambazi au ni kahaba wapenzi hao hawataki kusikia maneno hayo kwani wanaona ni ya watu wenye wivu, ambao hawataki mapenzi yao yafane. Hadi siku moja mmoja auawe kwenye matendo yake machafu ndio watu wanaanza kushangaa ‘mbona sikujua’!


Mabadiliko ya msingi ya CDM ni lazima yaanzie kwenye Katiba yake

Binafsi naamini kuwa mojawapo ya mambo yaliyochangia kwa kiasi kikubwa kwa CDM kushindwa kwenda Ikulu mwaka 2010 ni Katiba yake ambayo imenakili kwa kiasi kikubwa mfumo ule ule wa CCM – yaani Chama kimejengwa kutoka makao makuu na kinaongozwa kutoka juu. Ni mfumo mbaya kwa sababu unategemea maamuzi ya juu kuweza kugusa uongozi wa chini kabisa na katika demokrasia mfumo huu ambao umetengenezwa kutoka juu kwenda chini ni mfumo mbaya. CDM inajikuta inalazimika kujibu na kushughulikia mambo yanayotokea chini kutoka makao makuu.

Ipo mifano mingi ya kkuweza kuonesha hili likifanyika lakini miwili inatosha kuitaja hapa. Baada ya baadhi ya viongozi wa CDM Karatu kuangaza kugongana ilimlazimu Mwenyekiti wa Taifa Mbowe kwenda Karatu na kujaribu kupatanisha pande mbili na kujaribu kkutafuta suluhisho. Na tumeambiwa suluhisho limepatikana. Jingine na suala la BAVICHA ambapo baadhi ya vijana wamejikuta wakitumuliwa toka BAVICHA na CDM kutokana na lundo la tuhuma dhidi yao. Uamuzi huo umechukuliwa na BAVICHA Taifa. Sasa baadhi ya watu wanaweza kuona ni jambo zuri lakini kwangu linathibitisha tu ubovu wa mfumo huo – huwezi kutatua kila kitu toka makao makuu! Ni lazima Chama kiwe na mifumo inayoweza kushughulikia matatizo ya chini au ya ngazi fulani na yakaishia huko huko bila kulazimika kwenda makao makuu.

Ili kuweza kuleta mabadiliko ambayo yataisaidia CDM kujipanga naamini mabadiliko ya harakaya Katiba ya CDM yanahitajika. Kama nilivyowahi kuandika nyuma kuhusu CCM kuwa ilihitaji Mkutano Mkuu Maalum wa Chama ili kijisafisha – hawakufanya hivyo – naamini CDM nayo inahitaji Mkutano wake Mkuu (Baraza Kuu) kuweza kukaa chini na kupitisha mabadiliko ya msingi ya Katiba ili kuweza kukipanga chama. Mabadiliko hayo ni lazima –kwa maoni yangu – iweke mambo yafuatayo (pamoja na mengine mengi).



  • a. Viongozi wa juu wa Chama wa Kitaifa wasiwe wabunge – Wabunge wawe wabunge wasishike nafasi za uongozi makao makuu ya chama – hili nimuhimu kwa ajili ya kuweza kusimamiana (checks and balances).
  • b. Viongozi wa kitaifa wanaotaka kugombea nafasi yoyote ya kuchaguliwa (ubunge, udiwani au Urais) ni lazima waachie madaraka (wajiuzulu) nafasi zao mara wanapotangaza nia ya kugombea nafasi hizo. Hii itazuia viongozi wa kitaifa kutumia raslimali za chama kusaidia kampeni zao au za watu wao wa karibu.
  • c. Mgawanyo wa fedha za ruzuku uongozwe na kanuni zilizowekwa kikatiba ambapo kiasi kikubwa cha fedha kinaenda mikoani na ngazi zachini kujenga chama badala ya kutumika makao makuu. Makao makuu ipewe uwezo wa kubuni na kuendesha miradi ya chama kukipatia kipato.
  • d. CDM irudishe chama kwenye majimbo kuonesha kuwa kinaamini kweli sera ya majimbo. CDM imekuwa ikiuza sera kuwa wakishika madaraka wataongoza nchi wa kuweka madaraka katika majimbo zaidi. Sasa kama hili kweli wanaamini ni jambo zuri basi waanze nalo kwenye chama. Kwanini chama kiko too centralized? Naamini CDM kitoe madaraka makubwa kwa chama mikoani au kwa kuunganisha mikoa na hivyo kuwa na makao makuu ya chama ya Kanda ambayo yatashughulikia shughuli zote za chama katika ngazi hizo. Kama majimbo ni mazuri kwa uendeshaji wa serikali bila shaka ni mazuri kwa uendeshaji wa chama! Hii pia itasaidia kuondoa watu wanaotaka kwenda kufanya kazi makao makuu ya taifa! Wengine waende kwenye kanda huko!
  • e. Mfumo wa nidhamu ubadilishwe ili masuala ya nidhamu yashughulikiwe katika mfumo mmoja, unaoeleweka na ambao unafanya kazi kwa haraka, kwa uwazi, na kwa uhuru. Mfumo unaosubiri miaka au miezi kushughulikia migongano kwenye majimbo au ngazi fulani ni mfumo mbaya. Ni muhimu mfumo uwepo ambao mara tatizo linapojitokeza linashughulikiwa mara moja na kumalizwa siyo kuachwa kiporo wiki baada ya wiki miezi baada ya miezi na hata inakuwa miaka baada ya miaka. Huo ni mfumo mbaya.
  • f. Kurasimisha M4C kama taasisi ya chama. Sasa hivi M4C sijui ni kitu gani ndani ya chama. Niliandika hili wiki chache zilizopita kuwa mojawapo ya matatizo mengine ni hili la M4C kutokuwekwa katika utaratibu unaoleweka ambao utaondoa hisia ya kuwa M4C inaendesha na makao makuu tu na itaweka utaratibu wa wazi kwa wanachama na mashabiki wa michango inayopatikana na inavyotumika. M4C ni lazima iwekwe kama taasisiya chama, uongozi wake utambulishwe rasmi ukiwa unajulikana majukumu yake na mipaka yake. Isije CDM ikajikuta imetengeneza chama ndani ya chama


CDM ikiamua kujipanga vizuri na kufanya maamuzi ya haraka, thabiti na kuharakisha maamuzi hayo – yakiwemo ya mabadiliko ya Katiba inaweza kujipa nafasi ya kushinda uchaguzi mkuu ujao. Sasa hivi baada ya kuupoteza mwaka 2012 sioni ni jinsi gani bila mabadiliko ya ndani ya chama tena makini, ya makusudi nay a haraka CDM itaweza kushinda uchaguzi mkuu ujao. Na hili ni la kwanza hatujagusa suala la mabadiliko ya sera na maono.

Heri na fanaka za mwaka mpya mpendwa mzalendo


Niandikie: mwanakijiji@jamiiforums.com