Aziza Masoud ALIYEKUWA Meneja wa Kampeni za Urais wa CUF mwaka 2010, Said Miraji na wenzake jana waliwasilisha rasmi kwa Msajili wa Vyama vya Siasa maombi ya usajili wa muda wa chama cha Alliance for Democratic Change (ADC). Juzi, Miraji na aliyekuwa mgombea ubunge wa Temeke kwa tiketi ya CUF, Adawi Limbu walijitoa chama hicho na kutangaza kusudio la kusajili chama kipya. Jana, ujumbe wa chama hicho uliwasili katika Ofisi ya Msajili, Dar es Salaam saa 7:30 mchana ukiongozwa na Miraji ambaye alijitangaza kuwa ni Kaimu Mwenyekiti na Katibu Mkuu wake, Limbu na kupokewa na Wangalizi wa Ofisi ya Msajili, Galasia Simbachawene. Akizungumza na viongozi hao, Simbachawene alisema kulingana na taratibu za usajili wa vyama, maombi ya chama kabla ya kuwasilishwa kwa msajili yanahitaji kupatiwa muda ili yapitiwe na maofisa mbalimbali akiwemo Mwanasheria wa Ofisi ya Msajili. “Nimepokea maombi. Msiwe wasiwasi yameshafika kwa Msajili. Utaratibu uliopo ni kwamba maombi yanapokewa na kupewa muda zaidi wa kuyapitia kwa kushirikiana na mwanasheria ili kuona kama yamekamilika baada ya hapo yatawasilishwa rasmi kwa Msajili,” alisema Simbachawene. Vitu vilivyowasilishwa jana ni barua ya maombi ya usajili, rasimu ya katiba ya chama iliyoambatanishwa na hati ya kwenda kwa msajili (PF1) pamoja na hati ya kiapo ya kuwa chama cha jamii chini ya Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992. Miraji alisema wameamua kuanzisha chama hicho baada ya kutoona chama chochote cha siasa kinachowafaa kujiunga akisema karibu vyote vinafanana tabia. “Tumeamua kuanzisha chama cha siasa lakini, kitajikita kijamii zaidi. Hatujafanya uamuzi wa kishabiki kwani siasa za nchi hii zilivyo, si rahisi mtu kutoka chama kimoja kwenda kingine kwani vyote vinafanana, vina maneno matamu sana hasa CCM ,” alisema Miraji. Alisema ili kupata maoni ya wananchi kuhusu katiba ya chama hicho, rasimu ya katiba hiyo itaingizwa kwenye mitandao ya kompyuta pamoja na magazeti na majarida na kusambazwa katika maeneo mbalimbali. “Hatupo tayari kuwa na katiba ya mtu mmoja wala watu 100 tu, lazima tukusanye maoni ya muundo wa katiba kutoka kwa watu mbalimbali kupitia mitandao na kutoa matangazo kwenye magazeti yatakayoweza kuwafikia watu katika maeneo yote,” alisema Miraji. Alisema katika katiba ya chama chao vitu walivyozingatia ni pamoja na ukomo wa madaraka na kuweka kamati maalumu ya usuluhishi ambayo haitawahusisha viongozi wa juu wa chama ili kuepeka kuwafukuza wanachama wanapofanya makosa ambayo yanaweza kurekebishika. Kwa upande wake, Limbu alisema wananchi wanapaswa kuwa macho na vyama taasisi kwani viongozi wa vyama vya siasa wanafanya vyama hivyo kama mtaji. “Chama hiki hakina mwenyewe watu wanaruhusiwa kuja kujiunga wasisubiri mpaka wafukuzwe katika vyama vingine ambavyo havijui umuhimu na thamani ya wanachama,” alisema Limbu. Limbu aliwataka wanasiasa walio kwenye vyama visivyo na msimamo kuhamia chama hicho ili waweze kutetea haki za wananchi na kuwapa mwelekeo wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Walikitabiria kifo CUF Walipokuwa wakitangaza kujitoa CUF, Miraji na mwenzake walikitabiria kifo cha chama hicho wakisema kimepoteza mwelekeo kutokana na kuongozwa na watu wanaodhani ni mali yao. Pia walimshutumu Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Julius Mtatiro wakisema ameamua kwa makusudi kukiua.Hata hivyo, Mtatiro alijibu tuhuma hizo akisema, “Said Miraji ni mfuasi wa Hamad Rashid kwa muda mrefu sana. Amekuwa akikihujumu chama yeye na Hamad Rashid, kuondoka kwake siyo tishio la CUF. Nafahamu anakwenda kukabidhiwa chama na Hamad Rashid kama kaimu mwenyekiti hadi Hamad atakamoliza ubunge wake, tunamtakia kila la heri katika kujitoa CUF.” Mwananchi.co.tz |
Jisikie huru kabisa kuchangia lolote linalohusiana na jamii, uchumi, siasa, imani na elimu katika Blog yetu. Tunakaribisha habari, taarifa, picha za matukio, maoni na ushauri ili kuwekana sawa katika dunia yetu hii ndogo. Wote mnakaribishwa katika kuimarisha mshikamano wa kuleta mabadiliko ya kweli nchini mwetu!!
Pages
Forums
- Critical Analysis (11)
- Education Issues (15)
- Geology and Mining (21)
- International News (37)
- National News (147)
- Political Issues (67)
- Religious Issues (28)
- Social Issues (79)
- Sports (19)
Tuesday, February 28, 2012
Waliojitoa CUF waanzisha ADC
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Sasa vyama vitakuwa utitiri
ReplyDelete