Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Monday, February 27, 2012

Waraka kwa Rais Jakaya Kikwete (3)



*Tujikumbushe alivyotoboa siri ya mtandao 2005

Makosa yetu mengine hutokana na woga; woga unaotuzuia kumlaumu mkubwa japo tunajua kuwa kakosa, au kumtetea mdogo anayelaumiwa na wakubwa japo tunajua kuwa hana makosa. Na msingi wa woga ni unafsi. Pengine huwa tunaogopa sisi wenyewe kulaumiwa au kupata hasara fulani. Pengine twaweza kuwa hatuna cheo chochote ambacho tunaogopa kupoteza; pengine huwa hatuna wala tamaa yoyote ya kupata cheo fulani. Lakini woga unaweza kutokana na tamaa ya kila binadamu kupendwa na binadamu wenzake. Sisi wote tunayo tamaa hii, au sivyo tusingekuwa binadamu. Woga huu huweza ukamfanya mtu kuvumilia maovu, hasa kama maovu yale yanatendwa na walio wengi kwa walio wachache, au yanatendwa na wakubwa kwa wadogo. Kwa kuogopa kuwaudhi wengi tunawaacha watende makosa bila kuwasahihisha, wasije wakatuchukia. Huu ni unafsi mbaya sana.

Tujisahihishe
Julius K. Nyerere
Mei, 1962

Nimeanza na nukuu hii ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ili kuwajibu wasomaji kadhaa ambao wamediriki kusema nina chuki binafsi dhidi ya Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete. Hao hawanijui. Wapo wanaosema tayari kazi ya 2015 imeanza! Sijui ni nani mwenye mawazo finyu anayeweza kupambana na mtu anayeng’atuka! Anapambana ili iweje? Haya ninayoyaandika, yanatokana na msukumo wa kuwasaidia viongozi wetu, akiwamo Mheshimiwa Kikwete.
Isitoshe, Oktoba, 2005 Mheshimiwa Kikwete mwenyewe akiwa mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), alifanya mahojiano maalumu na aliyekuwa Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Tido Mhando. Katika mahojiano hayo yaliyofanyika London, Uingereza, Mheshimiwa Kikwete alieleza bayana msimamo wake wa kutumia vyanzo mbalimbali kupata kile kilichokuwa kikiendelea mitaani. Alisema:
“…Kuwa rahisi kuyasikia ya watu, hili ndilo jambo kubwa katika uongozi, ili uweze kuwa unayasikia mambo mbalimbali ya watu badala ya kuwa na njia moja ya kusikia wanavyosema wananchi wako. Kwa hiyo, lazima utengeneze namna ya kukutana na watu wengi…unajua tatizo la kusikia mambo ya huku duniani kupitia njia moja, wakati mwingine wanaweza kuwa wanakuletea yale tu ya kukufurahisha…oh, unajua mzee mambo huku ni mazuri, huko mitaani huko kila mtoto anayezaliwa anapewa jina la Jakaya…eh, Jumamosi hii mzee, watoto wote wa kiume waliozaliwa Muhimbili wanaitwa Jakaya…unaendelea hivyo mpaka mambo yanaharibika. Ni lazima pia uwe na namna zako nyingine za kupata habari zako. Nina watu wengi nawafahamu mitaani, kuna mabaraza ya wazee na kadhalika.”
Haya ni maneno yake Mheshimiwa Kikwete mwenyewe aliyoyazungumza Oktoba, 2005. Wengine tuliyazingatia haya na ndiyo maana tumejipachika dhima ya kumweleza kinachoendelea mitaani. Naamini yeye mwenyewe hawezi kushangaa kuona nimeamua kuitumia njia hii ya waraka kumfikishia yale yanayosemwa mitaani. Kama alivyosema mwenyewe, kutegemea njia moja kufikishiwa mambo muhimu, kuna walakini. Wapo wanaolalamika kwamba huenda Usalama wa Taifa hawampi haya, au kama wanampa, basi amekuwa mbishi na mpuziaji. Hata pale alipoamua kuwatumia wazee, amekuwa “akiwahutubia”, huku tukiambiwa kwamba “anazungumza na wazee!”. Wazee anaochangua kuzungumza nao ni mabubu? Mazungumzo gani yasiyoruhusu hoja kutoka upande wa pili?
Nirejee kidogo kwenye mada. Yeyote aliyemsikia Rais Kikwete wakati akihutubia wafuasi wa CCM wana wananchi wakati wa Maadhimisho ya Miaka 35 ya Kuzaliwa kwa CCM yaliyofanyika kitaifa jijini Mwanza, atakubali kuwa maneno anayozungumza Nape Nnauye, huwa ni yake. Ni kawaida ya Rais Kikwete kujaribu kukwepa lawama kila inapowezekana. Amekuwa wakiwatumia kina Nape kufikisha ujumbe, lakini amekuwa mwepesi wa kusema si yeye aliyewatuma. Inaiwia vigumu kuamini kuwa mwajiriwa anaweza kuwa jeuri mbele ya mwajiri. Nape ni mwajiriwa. Haiwezekani akawa anatoa kauli zisizomfurahisha mwajiri wake-Rais Kikwete-halafu akaachwa hivi hivi. Akili ya kawaida inakubali kuwa Rais amekuwa akimtuma Nape kuyasema anayosema, ingawa inawezekana si yote.
Kama hivyuo ndivyo, ebu tujikumbushe hili la kuwazuia wanaotaka urais wasijitokeze sasa. Huko nyuma nimepata kusema kwamba kitendo cha kuwazuia wana CCM na Watanzania wenye sifa zinazostahili kujitokeza sasa kutangaza nia, au kuanza maandalizi, ni kuwaonea. Haiwezekani jambo hilo likawa limehalalishwa kwa Mheshimiwa Kikwete tangu mwaka 1995, lakini sasa likawa haramu kwa wengine.
Kuna faida nyingi kwa mtu anayeutaka urais kujitokeza mapema. Ukiacha faida wanayopata wananchi ya kumtambua, ipo faida nyingine kubwa na muhimu kwake. Nayo ni ya kuupata urais. Kuwekeana vizingiti hakuna maana.
Katika kuthibitisha hilo, ebu turejee tena kwenye maneno ya Mheshimiwa Kikwete aliyoyazungumza alipohojiwa na Tido Mhando na yakarushwa kupitia BBC mnamo Oktoba, 2005.

TIDO: Wakati wa uteuzi wa chama, Rais Mkapa alitoa hotuba ambayo wengi walidhani alikuwa anakupigia debe wewe. Je, hili lilikushangaza hata wewe binafsi?

JK: Yaani wewe kweli mimi nitashinda kwa hotuba ya jukwaani pale. Ndugu yangu, nilishinda kwa jitihada kubwa ambazo niliziweka mimi na marafiki zangu. Ukweli ni kwamba ilituchukua muda kujijenga. Tulitengeneza mtandao wa watu nchi nzima wa watu wanaotuunga mkono. Tulifanya juhudi kubwa ya kuzungumza na wana-CCM.

TIDO: Lakini wakati kiongozi mkubwa kabisa, anapokuja mbele ya wajumbe na kutoa matamshi ambayo yanaonyesha dhahiri yanaelekeza kwamba yeye anamuunga mkono fulani, na ilijihidhirisha hata katika mkutano ule pale watu walipoanza heka heka za Kikwete…Kikwete moja kwa moja.

JK: Mimi sijui ni kupigiwa debe kwa vipi hasa. Hotuba ya Rais, yeye alichokuwa akizungumza tu ni kwamba... Mimi nadhani hotuba yake ilikuwa inasisitiza kwamba; kwanza alichokisema kwamba moja; CCM kama CCM, tuchague watu, lakini tusisahau huyu tunayemchagua sasa, hatimaye tutampeleka kwa watu.Na huko kwa watu, ni lazima sisi kama chama, kama tunataka kushinda, ni lazima tutambue matarajio ya watu. Kwa sababu haiwezekani muwe mmekaa tu pale kwenye mkutano, mkajifanya kama vile mmefunga masikio, yaani mmeziba masikio, na macho mmeyaziba, hamuoni na wala hamsikii huko mnakotoka wanasema nini.Lakini pia, hata wale wanakuja kwenye Mkutano Mkuu wanatoka katika kila wilaya ya nchi yetu. Ni vizuri kwao wakaangalia matumaini ya watu, na muangalie matumaini ya wale mnaowategemea watakwenda kupiga kura. Sasa, sina hakika kama kwa kusema hivyo alikuwa na maana yangu mimi!

TIDO: Kulikuwa na vitu vingi pale. Oh, mchague mtu ambaye amekulia kwenye chama hiki, anayekifahamu vizuri sana. Ukiangalia kwa undani, ukilinganisha na wagombea wenzako uliokuwa nao pale, sifa zote hizo zilikuwa zimeiva kwako.

JK: Lakini, niseme. Hivi, hivi ni mwana-CCM gani, atateua mtu ambaye hana historia na hicho chama. Hata kama utataka kunilaumu kwa hilo, bado nitaendelea kusema si kweli.

TIDO: Hapana si kwamba tunakulaumu, lakini tunasema alionyesha wazi kwamba chama kimchague Kikwete.

JK: Mimi sijui Bwana, sijui. Mimi ningependa kuamini kwamba nilifanya jitihada kubwa kushinda, na wasije wakafika mahali wakarahisisha mitihani niliyoipitia. Nilifanya jitihada kubwa sana. Sisi ni katika wale tunaoamini kwamba mwisho wa uchaguzi mmoja, ni mwanzo wa uchaguzi mwingine. Sisi tulianza mwaka 1995, tukaweka mkakati wa mwaka 2005.Nilifanya kazi kubwa kujenga mtandao. Nilifika mahali, kila mahali ukinitajia Ngara yuko nani, nakwambia yuko fulani. Nikawa nawajua watu kwa majina. Nimefanya kazi kubwa sana. Ndiyo, nakiri kwamba uzoefu wangu nao katika chama ulinirahisishia. Kwamba hawa watu ninawafahamu, nimeshaishi nao, ndiyo msingi ambao mimi ninadhani umesaidia.
Lakini wanaodhani nilishinda kwa hotuba ya Rais wanatafuta kurahisisha tu ili ionekane kwamba kama isingekuwa hotuba ile watu wasingenichagua. Hata kidogo! Mimi nilianza zamani. Ninaamini tu kwamba nilifanya jitihada mimi mwenyewe ya kuwaomba wana-CCM waniunge mkono, na ninashukuru walinikubali baada ya kuwaeleza nia yangu ni nini.

TIDO: Eh, uliwaomba wakupe kijiti ili nawe uweze kuliongoza taifa la Tanzania, na wao wamekupa, unafikiri sasa hivi uko imara zaidi kuliko miaka 10 iliyopita?

JK: Jibu ni ndiyo. Ni kweli tu kwa sababu, kwanza kwa maana tu ya uzoefu wangu katika utumishi wa umma, katika serikali. Lakini miaka 10 hii ambayo nimekuwa katika Wizara ya Mambo ya Nje, imenipa fursa kubwa na pana zaidi ya kuifahamu dunia na pia kufahamu hasa jinsi nchi zinavyoendeshwa.Nimepata uzoefu mkubwa wa kujifunza nchi zinazoendeshwa vizuri, na kwa nini wamefanikiwa. Nchi zinazoendeshwa vibaya, ni kwa nini wameshindwa.

TIDO: Kwa hiyo, unaweza ukasema labda unashukuru kwamba miaka 10 iliyopita ulikosa, na umepata mwaka huu sasa?

JK: Nilisema hivyo mkutanoni pale. Nilisema Mwenyezi Mungu, maana sisi Waswahili, ukishindwa unasema kila jambo ni kwa kheri ya Mwenyezi Mungu, eh kwamba pengine Mungu hakutaka, na alipokataa wakati ule alijua kwamba kuna ka-kipande haka ka-uzoefu ambako nilikuwa sijakapata, nami nikajitahidi kukapata. Nami nasema kwamba sasa nikifanikiwa kuchaguliwa nitakuwa Rais mzuri zaidi.

TIDO: Wengine wanasema hata hayati Mwalimu alikueleza hivyo siku ile hasa baada ya kushindwa, akisema nafasi yako inakuja, subiri. Je, hii ni kweli?

JK: Hayo yaacheni, tuzungumze mambo ya sasa.

Mwisho wa kunukuu
Je, kwa maelezo haya ya Mheshimiwa Kikwete, ya kujiandaa kwa miaka 10 kuupata urais, yanampa ujasiri gani wa kuwazuia wengine kwa miaka hii mitatu iliyosalia nao kujiandaa kuipata nafasi hiyo? Je, kama kwake ilikuwa halali kujiandaa kwa muda wote huo, tena kwa kuwa na mtandao imara, kwanini wengine nao ‘wasimuenzi; kwa njia hiyo? Tutafakari. Itaendelea.

Manyerere J. N
0759 488 955
manyerere@hotmail.com

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.