Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Saturday, February 25, 2012

Polisi Wanne Mbaroni Kwa Mauaji Songea

 
Thursday, 23 February 2012 21:22
Mtoto Shangwe Mtaula (16) mkazi wa Mabatini akiwa katika chumba cha wagonjwa mahututi katika Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma alikolazwa baada ya kulipukiwa na bomu la machozi wakati wa vurugu zilizotokea mjini Songea.Picha na Joyce Joliga
IGP MWEMA APELEKA KIKOSI CHA UCHUNGUZI, MAJERUHI HALI MBAYA
Joyce Joliga na Kwirinus Mapunda, Songea Polisi Mkoani Ruvuma, wanawashikilia na kuwahoji askari wake wanne kwa tuhuma za mauaji ya raia kwa kutumia risasi za moto katika vurugu zilizotokea juzi mjini Songea.Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Michael Kamhanda alisema jana kuwa askari hao walikamatwa na wanaendelea kuhojiwa ili kujua kama kulikuwa na uzembe katika utekelezaji wa majukumu yao.“Kwa kuwa tukio hilo limehusisha vifo, hatuwezi kuacha hivihivi tu ni lazima tujiridhishe kuwa askari hao hawakufyatua risasi kwa uzembe,”alisema Kamhanda.

Kamanda huyo alisema askari hao watahojiwa baada ya kuundwa kwa tume maalumu ya kuchunguza tukio hilo, na tume hiyo ikibaini kuwa kulikuwa na uzembe, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao ikiwamo kufikishwa mahakamani.
Hata hivyo kamanda Kamhanda hakutaka kutaja majina, wala vyeo vya askari hao kwa maelezo kwamba ni ni mapema mno, pia sababu za kiusalama.Katika hatua nyingine Kamhanda alisema tayari watu 54 wamefikishwa mahakamani kutokana na vurugu za juzi.

IGP Mwema achunguza
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema ametuma kikosi cha maofisa waandamizi kutoka makao makuu ya jeshi hilo, kikiongozwa na Mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo, Kamishna Paul Chagonja kwenda mjini Songea kufanya uchunguzi wa ghasia hizo.

Chagonja akizungumza na Mwananchi jana alisema maandamano hayo hayakuwa ya amani bali ya kihuni kwani yalilenga kuvamia ofisi za serikali ikiwemo Ikulu ndogo na Ofisi ya Mkuu wa mkoa. Chagonja alikuwa akijibu swali lililotaka aeleze endapo haoni kama polisi imetumia nguvu kubwa kutawanya raia waliokuwa wakiandamana kwa amani.

"Maandamano ya amani watu wanavamia Ikulu, maandamano ya amani watu wanazingira ofisi ya mkuu wa mkoa?"
"Sijafika huko ndo naelekea lakini, yale si maandamano ya amani. Yaani wahuni wanataka kuivuruga nchi waachiwe? Kuweni wazalendo, msiwe kama labda ninyi ni waandishi wa BBC kutoka Uingereza, hii ni nchi yenu."

Alifafanua kwamba, maandamano ya amani yanafahamika kwani watu hulazimika kuomba kibali na kuweka wazi ajenda ya maandamano "Lakini siyo maandamano yale, watu hayakuwa na kibali chochote, wahuni wamejiingiza wanataka kuvuruga nchi tu."

Mkuu huyo wa operesheni alitetea polisi akisema,"Usifikirie polisi hawana akili. Haiwezekani watu wazima na akili zao wenye mafunzo wafyatue hovyo risasi za moto kwa raia. Hakuna askari anapenda kuua raia..., lakini watu wanavamia Ikulu, ofisi ya mkuu wa mkoa, magari ya polisi hapo kuna amani kweli?"

Alitoa angalizo kwamba ni lazima hata vyombo vya habari, viache ushabiki badala yake viangalie maslahi ya taifa kwani nchi ikivurugika wao pia hawatasalimika na kusisitiza, "Kuweni wazalendo bwana, msifikirie kulishutumu jeshi la polisi tu."

Wakati IGP akituma kikosi hicho, wanaharakati, wanasiasa na wasomi wamekosoa matumizi makubwa ya nguvu za polisi dhidi ya raia na waandamanaji waliokuwa wakifikisha ujumbe wao kwa mkuu wa mkoa kupinga mauaji ya watu tisa yaliyofanywa kwa imani za ushirikina.

Juzi wananchi waliokuwa wakiandama kupinga mauaji hayo, walipambana na polisi ambapo watu wanne waliuawa na wengine 41 kujeruhiwa.

Hali za majeruhi Majeruhi wanane kati ya 11 waliolazwa katika Hospitali ya mkoa wa Ruvuma, jana waliruhusiwa. Majeruhi wengine 30 walipatiwa matibabu juzi na kuruhusiwa kurudi nyumbani kwao.

Mganga mfawidhi wa hospitali ya Mkoa wa Ruvuma, Dk Benedicto Ngaiza alisema tayari wagonjwa wanane kati ya kumi na moja waliolazwa katika hospitali hiyo wameruhusiwa na kwamba ni wagonjwa watutu ndio waliobaki.
Mmoja wa wagonjwa hao, Shangwe Mtaula (16) mkazi wa Mabatini hadi jana alikuwa hajitambui kutokana na kipigo cha polisi kilichosababisha kuumia vibaya katika paji lake la uso.

Muuguzi wa wodi alimolazwa mgonjwa huyo, Hildetha Mhonyo alisema binti huyo alifikishwa hospitalini hapo juzi saa tano asubuhi akiwa hajitambui na hivyo alilazwa katika wodi ya wagonjwa mahututi.

Muuguzi huyo alisema, bado hali ya Shangwe si nzuri ingawa jana alianza kuzungumza kwa taabu na kwamba anaonekana kuwa na maumivu makali kwenye paji lake la uso, huku macho yake yaonekana kuvimba.Mgonjwa mwingine ni Esta Mbali (29) mkazi wa Mshangano, ambaye amelazwa wodi namba tano baada ya kupigwa risasi katika bega lake la kushoto na kuumizwa vibaya.

Mgonjwa huyo anasema, hali yake inaendelea vizuri kwa sasa baada ya kupata matibabu. Alisema, katu hatasahau tukio hilo kwani alikuwa akitoka hospiatali kumsalimia binamu yake ambaye alikuwa amejifungua na wakati akiwa njiani alikutana na kundi kubwa la watu wakiandamana na baadaye polisi walianza kuwatawanya kwa mabomu ya machozi, ambapo alifanikiwa kukimbia na kujificha kwenye nguzo ya umeme, lakini ghafla alisikia kitu cha moto kikimuumiza begani mwake . Alisema alipatwa na kiwewe na kuanza kukimbia ovyo, hali iliyosababisha mwili mzima kulowa kwa damu ambayo wakati huo hakuweza kufahamu chanzo chake.

Esther aliendelea kusimulia kuwa baada ya kutokwa damu nyingi, aliishiwa nguvu na kuanguka, hadi aliposaidiwa na wasamaria wema ambao walimpakia kwenye gari na kumkimbiza hospitalini.
Mwingine ni Sinje Mchompa (29) mkazi wa Bombambili, ambaye alijeruhiwa katika tukio hilo na kuumizwa vibaya na kipande cha bomu mdomoni eneo la SODECO, wakati alipokuwa akielekea Mabatini.

Sinje alisema alipokuwa katika eneo hilo ndipo vurugu zilianza na kwamba alishtukia akipigwa na kitu kinachosadikiwa kuwa ni kipande cha bomu mdomoni na kutoboka mdomo hali iliyosababisha meno kuuma sana.

Mgonjwa huyo ameomba msaada wa kupatiwa matibabu zaidi ili hali yake iweze kurejea kama awali.
Kwa upande wake Matroni wa hospitali ya mkoa wa Ruvuma Helta Soko, ametoa ushauri kwa wananchi kuacha tabia ya kufanya vurugu katika maeneo ya hospitalini kwani hali hiyo inasababisha usumbufu kwa wagonjwa waliolazwa.

Kauli ya Helta inatokana na baadhi ya wananchi kupiga kelele wakati walipokuwa wakiwarushia mawe wauguzi na askari waliokuwa wakipeleka mwili wa mmoja wa waliokufa katika tukio hilo katika chumba cha maiti.



Habari tulizozipata wakati tukienda mitamboni zinasema, kwa mara nyingine, jana saa 12 jioni, polisi mjini Songea walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwaokoa watu wawili waliokuwa wakipigwa na wananchi wakiwatuhumu kwamba ni majambazi wanaojihusisha na vitendo vya mauaji ya wananchi.

Watu hao ambao walijeruhiwa vibaya walikamatwa na wananchi katika eneo la Mkuzo nje kidogo ya Manispaa ya Songea baada ya kujitambulisha kwa wenyeji kwamba wao walikuwa wakitatafuta shamba la kununua, huku mmoja wao ambaye ni mwanamke akitoroka na kukimbilia kusikojulikana.

Kutokana na kuwatilia mashaka, wananchi hao waliwazingira na kuwaweka chini ya ulinzi kisha kuwafikisha nyumbani kwa kiongozi wa Serikali ya mtaa wa Mkuzo, John Moyo na baadaye walianza kuwapiga baada ya kutokea utata katika maelezo yao.Soma zaidi www.mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.