Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Wednesday, February 29, 2012

Pinda atoboa siri juu ya uwekezaji kwa maliasili

                                             Waziri Mkuu wa Tanzania, 

Mizengo Pinda
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amesema ili nchi iweze kunufaika na maliasili ilizonazo, kuna haja ya kutumia wawekezaji wa ndani na kama itashindikana basi utumike mfumo wa ubia katika utafutaji wa maliasili hizo.
Aliyasema hayo Februari 28, 2012 wakati akifungua majadiliano yaliyohusu Jinsi ya kutumia vema maliasili na kuhakikisha zinalitajirisha bara la Afrika yaliyofanyika kwenye hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam.
Amesema mikutano ya majadiliano kama hiyo inapaswa kusaidia kutoa mafunzo kwa Watanzania ili wajue namna ya kusimamia vizuri zaidi maliasili za nchi yao. “Tunapaswa tuwafundisha watu wetu jinsi ya kuwekeza katika utaalamu, mitaji, mitambo na kwenye teknolojia ili tuache kutegemea vyanzo vya kutoka nje ya nchi,” alisema.
Amesema: “Tusipofanya hivyo tutajikuta tunaangukia katika balaa la kutonufaika na maliasili zetu ambalo limezikumba nchi nyingi za Afrika ambazo zimefanikiwa kugundua rasilmali kama vile almasi, mafuta, gesi na dhahabu katika nchi zao,” alionya.
“Balaa ama laana ya kutonufaika na rasilmali imezikumba nchi nyingi za Afrika, sina haja ya kuzitaja majina. Wengi wetu tumeshuhudia jinsi ambavyo ugunduzi wa maliasili ulivyochangia kuleta vita vya wenyewe kwa wenyewe, vita baina ya nchi; tumepoteza fedha nyingi, tumepoteza maisha ya watu wengi wasio na hatia hasa wanawake na watoto na wengine wamebakia vilema kutokana na vita hivyo,” aliongeza.
Amesema Tanzania iko tayari kushirikiana na wabia wa maendeleo, taasisi za kimataifa, sekta binafsi au watu binafsi ili kuhakikisha inajengea uwezo wananchi wake katika maeneo tofauti yakiwemo ya utafutaji, uongezaji thamani na uuzaji wa maliasili tulizonazo.
“Hii ndiyo njia pekee ambayo itahakikisha kwamba nchi na wananchi wake wanafaidika na maliasili zilizopo,” alisisitiza.
Naye Prof. Paul Collier wa Chuo Kikuu cha Oxford cha Uingereza anayeshughulikia masuala ya uchumi wa Afrika ambaye alikuwa mtoa mada katika majadiliano hayo, alisema Tanzania na nchi za Afrika hazijengea uwezo watu wake ili waweze kuwekeza vya kutosha kwenye utafutaji wa maliasili na ndiyo maana bara hili limeendelea kubaki maskini.
“Ili kunufaika na sekta hii inabidi kuwekeza zaidi, kufanya tathmini ya maliasili mlizonazo, kuzipangia matumizi bora, kulinganisha matumizi ya sasa na kuangalia maisha ya baadaye yatakuwaje na kutunza akiba kutokana na maliasili mlizonazo,” alisema.
Naye Balozi wa Finland nchini, Bibi Sinikka Antila alisema hivi sasa Tanzania imevumbua maliasili nyingi zinazoweza kuiletea utajiri mkubwa lakini akasisitiza haja ya kusizimamia vizuri ili kuhakikisha kuwa zinawanufaisha wananchi wote.
Akitoa mfano wa kutokuwepo usimamizi katika rasilmali, Balozi huyo alisema uvunaji magogo haujatungiwa sheria kali na wala hautozwi kodi inavyostahili na matokeo yake, nchi inapoteza asilimia 90 ya mapato kutokana na mazao ya misitu. “Usimamizi endelevu wa misitu ndiyo msingi wa uchumi imara”, alisisitiza.
Mapema, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Prof. Joseph Semboja alisema taasisi hiyo imeandaa majadilianio hayo ili kutoa fursa kwa viongozi waweze kujadiliana na kubadilishana uzoefu kwenye masuala ya utunzaji maliasili.
Alisema kikao hicho ni mwanzo wa mikutano ambayo taasisi hiyo imejipanga kuifanya ili kuwapa nafasi viongozi wapate mbinu kuboresha utendaji kazi wao. Alisema mwezi ujao, taasisi yake itaandaa mkutano kwa ajili ya Wakuu wa Tume za Uchaguzi kutoka nchi 16 ili wabadilishane uzoefu katika eneo hilo.


Short URL: http://www.thehabari.com/?p=14022

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.