Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Tuesday, February 28, 2012

Wahitimu Wa Vyuo Vikuu Wanatakiwa Kufundisha Shule Za Kata



Naomba nichangie kuhusu hili suala la shule za kata na ukosefu wa walimu. Binafsi ninayo maoni tofauti na wengi wanaozibeza kwamba ni mzigo na hazina tija hata kidogo katika maendeleo ya elimu Tanzania.

Kusema ukweli wengi tunakumbuka enzi zile ambazo kulikuwa kuna uhaba wa shule za sekondari kiasi kufaulu darasa la saba ilikuwa ni ndoto za alinacha. Kwa vile wakati ule shule za sekondari hazikuwa nyingi nap engine kila mkoa ulikuwa na walau shule moja au mbili, na kulikuwa na shule zile za kitaifa zilizochukuwa wanafunzi kutoka kila kona ya nchi. Hapo utataja shule za Mazengo, Mkwawa, Ilboru, Msalato, Tabora Girls, Tabora Boys na Mzumbe kutaja chache.

Nafikiri ni kwa kutambua uhaba wa shule za sekondari za kutosha na pia ile hamu kubwa ya kukata kiu ya kupata elimu kwa kila mtanzania ndio serikali yetu ikaja na mpango wa kupanua elimu kwa kuongeza idadi ya shule kwa kuanza na mpango wa shule za msingi na baadae kufuatia na ule mpango wa shule za sekondari.
Kwa bahati mbaya katika utekelezaji wa mipango yote hiyo kumekuwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa walimu na vifaa vya kufundishia kwa ngazi zote. Na kutokana na hili ndio maana watu wengi wamekuwa wakikashifu na hata kutoa kejeli kwa mpango mzima ambao mbali na mapungufu hayo umekuwa na mafanikio ya wastani lakini ambayo ninayo matumaini yatakuwa endelevu.

Kwanza kabisa ni dhahiri kumekuwa na ongezeko la idadi ya wanafunzi wanaojiunga na sekondari tangu kuanzishwa kwa mpango huu. Na hapa wengi wanakosoa kwamba hili halina tija kwa kuwa kwa changamoto zilizopo katika shule zinafanya elimu itolewayo kuwa ya chini na isiyo na tija. Katika hili sipangani na wanaotoa kasoro hizi ingawa naamini bado hata katika hilo kundi la shule za kata wapo baadhi ya watoto wetu wanaofaulu na kuendelea mbele na elimu za juu, tofauti na namna ilivyokuwa zamani wakati ambapo hata upenyo wa kuingia kwenye mfumo wa elimu haukuwepo.

Baada ya kujaribu kutoa hayo maelezo machache sasa naomba nieleze jambo moja ambalo mimi nafikiri linaweza kusaidia kupunguza changamoto ya ukosefu wa walimu katika hizi shule. Nimejaribu kupitia mfumo wa ukopeshwaji wa miko[o kwa ajili ya elimu ya juu na suala la kujiunga na mfumo wa Jeshi la Kujenga Taifa (National Service) na hapa ndio nikaona kuna mwanya wa kupata suluhu ya tatizo hili. Nionavyo mimi serikali inapaswa iandae mpango ambao utwalazimisha wanafunzi wanaohitimu katika vyuo mbalimbali nchini kwenda kufundisha katika hizi shule za kata kwa walau kipindi cha mwaka mmoja.
Kwa kufanya hivi serikali itatakiwa kuwapa posho za kujikimu wahitimu hawa na kwa kiasi fulani cha mshahara, kiasi kinaweza kukatwa kufidia mkopo ambao wahaitimu walikopeshwa na serikali kugharamia elimu za chuo kikuu.
Wapo wanaoweza kuona mpango huu hauna mantiki, lakini kiukweli katika wakati tulionao hatuna suluhisho la haraka na la unafuu kama hili. Wanaweza kuja wasemaji, kwamba wahitimu hao hawatakuwa na weledi wa kiualimu, lakini jawabu ni kwamba katika Tanzania tumekuwa na programu nyingi za kuwapika walimu kwa muda na baadhi zimeweza kutoa walimu ambao wengi tumepitia kwao. Tunakumbuka mpango wa UPE, Mama Sita Programe (VODA FASTA) nk.
Lakini mbali na hilo serikali pia itatatua kwa kiasi tatizo la wahitimu wa vyuo vikuu kukwepa kulipa mikopo baada ya kuhitimu.

Ili kutekeleza na kusimamia mpango huu serikali inapaswa kuwa na mpango wa kutoa vyeti maalumu vitakavyotolewa kwa wale watakaomaliza vyema muda wao kufundisha na hicho ndio kiwe kibali kwa taasisi kumuajiri mhitimu wa chuo.

Najua viongozi wetu wanao nafasi ya kujifunza zaidi namna bora ya utekelezaji wa mpango na mipango zaidi ya kukwamua sekata ya elimu na nyinginezo, kwa hiyo kwa kujifunza zaidi namna ya utekelezaji wanaweza kujifunza katika nchi ya Ghana namna hizi programu zinavyoendeshwa.

Naomba kuwakilisha

Kwa hisani ya Mjengwablog

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.