Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Thursday, February 23, 2012

NIDHAMU YA MAISHA


                                                  
Tunaishi katika dunia yenye vitu vingi vinavyochanganya kuchagua.Wengine husema tunaishi katika dunia iliyochanganyikiwa iliyojaa mazuri,mabaya,ujinga,hatari,majanga,magonjwa,umaskini,utajiri,ndoto za maisha yetu,uchafu wa kila aina, matukio yanayotuchanganya na mengine mengi.Na katika hayo yote tunao uhuru wa kuchagua yale tuyatakayo.Na muda mwingine ni vigumu hata kujua au kuyafikia yale tuyatakayo kutokana na uwingi wa mambo yanayochanganya.Hata yale ambayo muda mwingine huwa tunayaona ni sahihi hugeuka tena kuwa tofauti.Katika hayo yote upo uwezekano wa kuchagua na kufanikiwa katika uchaguzi lakini si rahisi kama hakutakuwa na nidhamu ya maisha. Kila kitu, kila matokeo tuliyonayo maishani hata kama hatuyapendi yamesababishwa na sisi wenyewe kwa kujua au hata kutokujua. 
Umaskini ama utajiri umesababishwa, magonjwa na hata laana Fulani vyote vimesababishwa  na sisi wenyewe au na waliotutangulia. Na hata sasa tunayoyatenda na kuyafikiri sasa yatakuwa matokeo ya maisha yetu kesho. Tunaishi katika dunia ya kupanda na kuvuna na hii ni kanuni. Kila anayepanda mihogo ni lazima avune mihogo kamwe hawezi kuvuna korosho.Hivyo basi kila siku unayoishi sasa unasababisha kitu Fulani maishani. 
Kila hatua unayoichukua leo unatengeneza au unaharibu maisha yako. Ni kweli waliotutangulia wamesababisha mengi tunayoyaishi leo lakini leo hii tunayoyaishi tunayasababisha ya kesho na hatuwezi kukumbatia umaskini eti kwasababu waliotutangulia walikuwa hivyo bali tunaweza kuchukua hatua sasa tukasababisha ya kwetu kwa muda wetu,mazingira yetu pasipokujali nani alitufikisha hapa tulipo leo.
 Katika maisha tunayoyaishi sasa kila mmoja anatengeneza matokeo ya maisha yake ya baadaye kwa kujua au kutokujua.Dunia ina vitu vingi sana vinavyochanganya vyenye kila sababu zinazoweza kutufanya tuharibu maisha yetu ya kesho hivyo basi bila nidhamu ya maisha huku tukijua tunataka nini na kwasababu gani lazima tutaendelea kuharibu mifumo ya maisha yetu ya kesho

. Muda mwingine matukio ya maisha hutufanya tusahau yatupasayao kufikiri kuhusu sisi hata kusahau nini tunaweza na nini tufanye. Hivyo tunapoishi maisha yetu sasa tutambue kuwa inawezekana tunatengeneza au tunabomoa na hivyo basi  tukiujua ukweli huu itatufanya tujue nini tuchague,nani tuwe naye,wapi tuende,nini tusome au kwa kifupi tutaishi kwa nidhamu huku tukiwa na malengo Fulani tunayotaka kuyafikia.
Na maisha yetu yawe ni mazuri au mabaya,tuwe tunayapenda au hatuyapendi yamesababishwa na sisi wenyewe kwa kujua au kutokujua hivyo basi tunapotafuta chanzo cha kufeli au kufaulu kwetu tusisahau kujichunguza wenyewe ndani yetu,tunapomtafuta mchawi wa maisha yetu tusisahau kujichunguza wenyewe kwani ndiko kutokako mazuri au mabaya ya maisha yetu.Tukijua ukweli huu tutaweza kubadili hatima ya maisha yetu huku tukijua kabisa maisha yetu ya baadayae yatakuwaje na huu ndio mfumo ambao watu waliofanikiwa sana na wanaoyaishi maisha ya furaha hutumia.
Watu wote wenye maisha mazuri na ya furaha wanajua siri ya nidhamu ya maisha na waliyajua haya mapema kuwa hatima ya maisha ya binadamu mhusika ipo katika kila maamuzi yake anayoyachukua kila siku na mafanikio huja pale atakapoamua kuwa na nidhamu ya maisha yake mwenyewe. Ni uchaguzi wetu kutengeneza au kuharibu, ni uchaguzi wetu kuyapata tuyatakayo maishani au kuyakosa.Bila nidhamu ya maisha hakuna makubwa ya maisha tutakayoyaona.Kila kitu kimesababishwa.
Na Geophrey A. Tenganamba, Mwandishi wa Vitabu vifuatavyo; Kichwa Chako ni Dhahabu ya Utajiri, The Richest Goldmine na  Nguvu ya Kujitajirisha. Ukitaka vitabu tumia namba +255714477218 au email:gtlivemore@gmail.com utaletewa mahali ulipo. Hata kwa huduma nyingine za maisha na biashara tumia waweza kuwasiliana na mwandishi huyu.

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.