Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Saturday, February 25, 2012

TAARIFA YA CHADEMA KUHUSU MAPATANO YA MR SUGU NA RUGE


TAARIFA KWA UMMA
Idara ya Sanaa ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) imepokea taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa kuhusu mapatano baina ya Mheshimiwa Joseph Mbilinyi (Mb) na Rugemalira Mutahaba.
Taarifa hiyo ya tarehe 21 Februari 2011 imeeleza pamoja na mambo mengine kuwa pande mbili hizo zimekubaliana kushirikiana kufanikisha haki na jitihada za kuinua maslahi ya wasanii. Aidha, pande mbili hizo zimekubaliana kufanya jitihada za pamoja kuunganisha vyama vya wasanii vya TUMA na TFU ili kutetea maslahi ya wasanii wakiwa na umoja zaidi.
Idara ya Sanaa ya CHADEMA inatambua kwamba makubaliano hayo ni hatua ya kwanza kwa pande hizo mbili na wadau wanaoshirikiana nao katika jitihada za kuboresha sanaa nchini hususan ya muziki wa kizazi kipya; hivyo hatua zaidi zinapaswa kufuata.
Idara ya Sanaa ya CHADEMA inampongeza Mbilinyi maarufu kama Sugu ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Habari, Vijana na Utamaduni kwa kuendeleza harakati za kupigania haki za wasanii ndani na nje ya bunge hali ambayo imeibua mjadala na hatimaye kufikiwa kwa makubaliano hayo. Kusainiwa kwa makubaliano hayo ya kuunganisha nguvu kumedhihirisha kwamba ‘palipo na msuguano pana mwendo’ (where there is friction, there is movement).
Kwa kuwa mashahidi katika mapatano hayo ni Waheshimiwa Dr. Emmanuel Nchimbi (Mb) ambaye pia ni Waziri wa Habari, Vijana na Utamaduni na Tundu Lissu (Mb) ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Sheria na Katiba; idara ya sanaa inatarajia kuwa kwa misingi ya makubaliano yaliyofikiwa yanayohusu hatua za kiserikali na kibunge nguvu za ziada zitaunganishwa kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji.
Idara ya Sanaa ya CHADEMA inatarajia kwamba kwa makubaliano hayo sasa wadau wote wataunganisha nguvu za pamoja ili wasanii waweze kuwakilishwa ipasavyo na chama chao chenye kutambuliwa rasmi na Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA).
Aidha, idara ya sanaa ya CHADEMA inatambua kuwa kufuatia mapatano hayo sasa serikali inapaswa kuanza utaratibu wa kuhakikisha kwamba vifaa vya studio vilivyotolewa na Rais Jakaya Kikwete inawekwa chini ya chombo ambacho wasanii wengi wataweza kunufaika.
Idara ya Sanaa ya chama, inatambua kwa mujibu wa katiba ya CHADEMA chama kinaamini katika falsafa ya nguvu ya umma, hivyo jitihada zozote za kuunganisha nguvu za pamoja kwenye mambo ya kudai haki za msingi ni suala linalohitaji kuungwa mkono. Aidha, kwa mujibu wa katiba ya CHADEMA chama kinaamini kwenye itakadi ya mrengo wa kati inayotaka pamoja na mambo mengine fursa kutolewa kwa wote zenye kuhakikisha pamoja na mambo mengine vipaji vya vijana vinaendelezwa.
Hivyo, Idara ya Sanaa ya CHADEMA itaendelea kufuatilia hatua zinazochukuliwa za kuunganisha nguvu za pamoja kutetea haki za wasanii ikishirikiana na Waziri Kivuli wa Habari, Vijana na Utamaduni, Joseph Mbilinyi na wadau wengine.
Imetolewa tarehe 24 Februari 2012 na:
Fulgence Mapunda (Mwana-Cotide)
Afisa wa Idara ya Sanaa

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.