Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Tuesday, January 10, 2012

CHADEMA: Hatuna uchu na urais


na Charles Misango

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema viongozi wake wa kitaifa hawana muda wala uchu wa kugombania madaraka ya urais kama walivyo baadhi ya viongozi wa vyama vingine vya siasa.
Katika taarifa yake ya kukanusha habari zilizochapishwa na gazeti moja la kila siku kwa lugha ya Kiswahili (sio Tanzania Daima) la juzi Januari 8, 2012, CHADEMA ilisema hakuna ‘mpambano’ kati ya viongozi waandamizi wa chama hicho kama ilivyoandikwa na gazeti hilo.
Imesema kuwa viongozi wake makini hawawezi kuanza mbio za kusaka urais, badala yake, muda wa sasa unatumika kujikita katika kushughulikia na kutafuta ufumbuzi wa vyanzo vya matatizo ya jamii yanayozidi kuongezeka, huku serikali ikiishia kushughulika na matokeo, hivyo kukosa majibu ya kudumu na kuishia kutoa lawama kwa wakosoaji.
“Kwetu, urais si cheo, ni dhamana ya utumishi kwa umma, suala ambalo linazingatia masuala muhimu ambayo ni mahitaji ya wananchi (nchi) na kisha sifa za mtu husika kuwa kiongozi wa nafasi hiyo.
“Kwa sasa ndani ya CHADEMA kitu hicho cha ‘kupamba moto’ kwa ajili ya kuwania urais hakipo na wala hakiwezi kuwepo, hasa kwa sasa ambapo chama kimejikita kuzidi kujijenga kwa kutimiza wajibu wake, kama serikali mbadala inayosubiri kupata ridhaa ya wananchi kuongoza nchi,” ilisema sehemu ya taarifa ya chama hicho kwa vyombo vya habari jana.
CHADEMA imesema kuwa kwa sasa suala muhimu ni namna ya kutafuta mizizi au vyanzo vya matatizo mbalimbali yanayoikabili jamii pana ya Watanzania na kisha kutafuta majibu au suluhisho la kudumu, kwa kushirikiana na wananchi wote wenye nia njema na nchi yao, kwa ajili ya maendeleo ya watu.
Imesema siku zote suala la urais linategemea mahitaji mapana ya Watanzania, na kamwe haliwezi kuamriwa kwa kufuata matakwa, utashi au uchu mtu binafsi.
CHADEMA imedai kuwa hata litakapojitokeza suala hilo litashughulikiwa kwa kuzingatia mahitaji na maslahi mapana ya wananchi na itaamua kwa kufuata katiba, kanuni na taratibu zake, si vinginevyo.
Taarifa hiyo imewataka wananchi wasiwafananishe viongozi wake na wale wa baadhi ya vyama vingine ambao wamekuwa wakilifanya suala la kugombea nafasi ya urais kuwa linaongozwa na kuamriwa kwa utashi binafsi wa mtu, ukiongozwa na uchu na tamaa ya vyeo.
“Mahitaji ya Watanzania ndiyo yaliyotumika kupata wagombea urais wa CHADEMA katika chaguzi kuu mbili za mwaka 2005 na 2010 kwa kuzingatia mtazamo huo, mara zote hizo mbili, wagombea waliombwa, wala hawakuongozwa na uchu au tamaa ya madaraka.
“Hali itakuwa hivyo hivyo wakati ukiwadia wa kumpata mgombea urais wa mwaka 2015, kamwe utashi, uchu au maslahi binafsi ya mtu hayawezi kupewa nafasi ndani ya CHADEMA,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imesema kuwa kinachopewa umuhimu ni utumishi kwa umma, kwa ajili ya maendeleo ya watu na si mbio za kusaka vyeo, na CHADEMA itaendelea kuweka mbele kwanza kabla ya kitu kingine chochote mapambano dhidi ya vyanzo vya matatizo kama vile umaskini, rushwa na ufisadi mwingine lukuki unaozidi kutafuna na kuangamiza taifa na watu wake.

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.