Jan 21st 2012, 11:57
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimemteua Ali Mbarouk Mshimba
kuwa mgombea wa Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kwa tiketi ya
CHADEMA katika Jimbo la Uzini.
Uteuzi huo umefanywa na Kamati Kuu ya chama taifa katika mkutano wake wa
kawaida uliofanyika Dar es salaam tarehe 20 Januari 2012 chini ya uenyekiti
wa Makamu Mwenyekiti Taifa (Bara) Said Amour Arfi (Mb) na Katibu Mkuu Dr.
Wilbroad Slaa.
Maamuzi hayo yalipitishwa kwa kauli moja na kamati kuu ya chama taifa baada
ya kupokea taarifa ya mchakato wa uteuzi wa awali uliofanywa na ngazi
husika za CHADEMA Jimbo la Uzini iliyowasilishwa na Naibu Katibu Mkuu
(Zanzibar) Hamad Musa Yusuph.
Katika taarifa hiyo Kamati Kuu ya Chama Taifa ilielezwa kwamba uchukuaji
fomu za uteuzi wa ndani ya chama ulianza tarehe 15 Disemba 2011 na
kuhitimishwa tarehe 15 Januari 2012. Jumla ya wanachama watatu walichukua
fomu za kugombea.
Kura za maoni za uteuzi wa mgombea zilifanywa tarehe 17 Januari 2012,
ambapo Ali Mbarouk Mshimba alikubaliwa kwa kura zote 126 za wajumbe
waliohudhuria mkutano mkuu wa jimbo, kati ya wajumbe 130 waliopaswa
kuhudhuria kutoka katika shehia zote 13 za Jimbo la Uzini.
Mapendekezo hayo ya jimbo la Uzini ya kumteua Ali Mbarouk Mshimba
yaliridhiwa na kikao cha Kamati ya Utendaji ya Wilaya ya Kati
kilichofanyika tarehe 18 Januari 2012.
Ali Mbarouk Mshimba alizaliwa tarehe 10 Aprili 1966 katika Kijiji cha
Tunduni, Jimbo la Uzini, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Zanzibar. Ali
Mbarouk Mshimba ni Katibu wa CHADEMA wa Jimbo la Uzini na ni Mwalimu wa
Skuli Msingi Mchangani Chamba.
Ali Mbarouk Mshimba amesoma Shule ya Msingi Uzini mwaka 1977 mpaka 1984 na
Shule ya Sekondari ya Fidel Castro mwaka 1984 mpaka 1987 na baadaye kusoma
mafunzo ya ualimu ya miaka miwili katika ngazi na nyakati mbalimbali mwaka
2006 mpaka 2008 (Special Certificate in Teacher Education through Teachers
Advancement Program) yaliyoratibiwa na Wizara ya Elimu na Ufundi Stadi ya
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Imetolewa tarehe 21 Januari 2011 na:*
Dadi Kombo Maalim*
Afisa Mwandamizi wa Habari na Uenezi*
Ofisi ya Makao Makuu Zanzibar*
No comments:
Post a Comment
Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.