Kamati Maalum ya CHADEMA kuhusu Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 itawasilisha taarifa yake kwa Kamati Kuu leo tarehe 22 Januari 2012.
Taarifa kuhusu maamuzi ya kamati kuu ikiwemo kuhusu mkutano na Rais Jakaya Kikwete juu ya Sheria ya mabadiliko ya katiba itatolewa baada ya kamati kuu kumaliza kikao chake.
Kamati Maalum ya Kamati Kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) iliyoundwa kwa ajili ya kukutana na Rais Jakaya Kikwete kuhusu sheria ya mabadiliko ya katiba ya mwaka 2011 ilikutana tena na Rais jana tarehe 21 Januari 2012 Ikulu Dar es salaam.
Katika mazungumzo hayo Kamati Maalum ya CHADEMA ikiongozwa na mwenyekiti Freeman Mbowe ilitaarifiwa hatua ambayo imefikiwa na serikali katika kuanza kuiboresha sheria ya mabadiliko ya katiba ya mwaka 2011 ili ikidhi mahitaji ya kujenga kuaminiana na muafaka wa kitaifa kwa mawasiliano na mashauriano na wadau mbalimbali.
Baada ya mazungumzo hayo, Kamati Maalum itawasilisha taarifa yake kwa Kamati Kuu ya Chama katika mkutano wake ulioanza leo tarehe 22 Januari 2011 Jijini Dar es Salaam.
Taarifa zaidi kuhusu maamuzi ya Kamati Kuu baada ya kupokea taarifa ya kamati maalum itatolewa baada ya kumalizika kwa kikao cha kamati kuu kwa wakati ambapo wanahabari na umma utajulishwa.
Itakumbukwa kwamba tarehe 27 na 28 Novemba 2011 Rais Kikwete alifanya mkutano wa siku mbili na viongozi wa CHADEMA kuhusu muswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba na pande mbili kukubaliana kuhusu haja ya sheria husika kufanyiwa marekebisho kwa mashauriano na wadau mbalimbali kwa lengo la kudumisha muafaka wa kitaifa kwenye mchakato wa katiba mpya.
Mkutano huo ulitokana na azimio na Kamati Kuu ya CHADEMA katika kikao chake maalum kilichofanyika tarehe 20 Novemba 2011 Dar es Salaam, pamoja na mambo mengine, kilipokea na kujadili kwa kina taarifa ya majadiliano na kupitishwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011.
Kamati Kuu iliazimia kwamba Ushiriki wa CHADEMA katika mchakato mzima wa kupata Katiba Mpya uliowekwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba utategemea utayari wa Serikali ya Rais Kikwete kufanya mabadiliko ya kimsingi katika sheria hiyo kwa lengo la kujenga muafaka wa kitaifa juu ya mchakato huo; na kutokana na azimio hili kamati kuu iliunda kamati maalum kwa ajili ya kukutana na Rais kumshauri asisaini sheria husika.
Aidha Kamati Kuu iliazimia kuwa CHADEMA itaendelea kutoa elimu kwa wananchi na wadau wote juu ya ubovu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na juu ya haja ya kuwa na sheria itakayoweka utaratibu bora zaidi wa kuunda Tume Shirikishi ya Katiba kwa lengo la kukusanya maoni ya wananchi, kuandaa ripoti na Rasimu ya Katiba Mpya, Bunge Maalum la Katiba na usimamizi wa kura ya maoni itakayowezesha wananchi kufanya maamuzi kwa uhuru na kwa haki.
Kamati Kuu iliwaagiza wabunge na viongozi wote wa chama katika ngazi zote kufanya mikutano ya ndani na ya hadhara yenye lengo la kuwaelimisha wananchi juu ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na madhara yake kwa mchakato wa kupata Katiba Mpya na bora kwa nchi yetu kwa lengo la kuunganisha umma wa watanzania kuweza kufanya mabadiliko ya msingi.
Imetolewa na:
John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi
No comments:
Post a Comment
Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.