Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Friday, January 13, 2012

Hamad Rashid ageukwa kwao

HAMADI Hamad Rashid ageukwa kwao

Na Mwandishi wetu
12th January 2012
Mbunge wa Jimbo la Wawi, Hamad Rashid MohamedMatawi 21 ya Chama Cha Wananchi (CUF) katika ya Jimbo la Wawi kisiwani Pemba yatafanya maandamano kulipongeza Baraza Kuu la CUF kwa uamuzi wake wa kumfukuza uanachama Mbunge wa Jimbo hilo, Hamad Rashid Mohamed (pichani).
Hayo yameelezwa na wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya CUF ya jimbo hilo katika mkutano wa waandishi wa habari uliotishwa kwa lengo kutoa tamko la jimbo kuhusiana na hatua ya Baraza Kuu kumvua uanachama Hamad.
Kamati hiyo imesema maandamano hayo yatafanyika wakati wowote kwa kuwa walikuwa wanasubiri kumalizika kwa Maadhimisho ya Miaka 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambayo yanafikia kilele chake leo.
Walisema Hamad ni chaguo la Baraza Kuu la Uongozi la CUF, hivyo kumfukuza ni ukombozi kwa wakazi wa jimbo hilo na kuongeza kuwa wanasubiri awarejeshee jimbo ili wachague mbunge mwingine wanayemtaka.
Walisema walimkataa wakati wa kura za maoni mwaka 2005 na kumpitisha kwa kura nyingi, Yusufu Salim, ambaye alikuwa chaguo lao, lakini cha kushangaza ni kuwa Baraza hilo ndilo lililombeba na kumpeleka kwa wananchi ili apigiwe kura na kulitupia mbali chaguo la wananchi wa Wawi.
Mwakilishi wa Jimbo la Wawi, Malim Salehe Juma, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Chake Chake, alisema kuwa Hamad halikuwa chaguo la wanachama wa Jimbo la Wawi ila walilazimika kumchagua kwa shingo upande kwa vile Baraza hilo lilikuwa likimpenda.
“Sisi tunashukuru sana kurejeshewa jimbo letu namtaona jinsi siku ya mandamano wananchi watakavyokuwa wamefurahi kwani jimbo letu sasa limepata ukombozi kutoka Baraza Kuu kwa kumfukuza kipenzi chao na kutuachia jimbo letu huru,” alisema.
Mwakilishi huyo, alisema baada ya kutolewa kauli ya Hamad kwenda kinyume na taratibu za chama na kufukuzwa uanachama, alifanya kazi ya kupita katika matawi 21 yaliyomo katika Jimbo hilo kuwaeleza wanachama wa chama hicho na wote waliafiki.
Afisa wa Uchaguzi wa Wawi, Yadilu Said Salimu, alisema kwa kiasi kikubwa alishiriki kusimamia uchaguzi wa Hamad hivyo anaelewa vyema kuwa si chaguo la wakazi wa jimbo hilo.
“Mimi namwambia asidanganyike akaona kuwa alipata kura nyingi akadhani watu wa Wawi wanampenda sana ni kwa sababu walikuwa tu wanakipenda chama na pale walikipigia chama, ajaribu aingie chama kingine aone,” alisema.
Yusuf Said Sefu, alisema wakazi hao na wanachama wa CUF walimwita Hamad kwenye Mkutano Mkuu wa jimbo hilo ili kujibu tuhuma, lakini walishangazwa walipoona ameshindwa kujitetea.
Mjumbe mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la Bimariam, alisema kwa kiasi kikubwa Baraza hilo liliwachelewesha kumbakiza ndani ya jimbo hilo na kuwazoroteshea maendeleo yao kwa muda mrefu.
Kesi kuanza wiki ijayo
Maombi ya Hamad na wenzake 10 ya kutaka Mahakama Kuu Dar es Salaam iiamuru Bodi ya Wadhamini wa CUF kujieleza kwa nini wasitiwe hatiani kwa kukiuka amri yake, sasa yatasikilizwa Januari 19, mwaka huu.
Maombi hayo yatasikilizwa na Jaji wa Mahakama hiyo, Augustine Shangwa, ambaye kesi ya msingi namba 1/2012 iliyofunguliwa na Hamad na wenzake dhidi ya wadhamini hao iko mbele yake.
Mbali na wadhamini hao, Hamad na wenzake waliiomba mahakama iwaamuru pia wajumbe wa Baraza hilo, akiwamo Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, kujieleza kwanini wasitiwe hatiani kwa kukiuka amri hiyo.
Pia wanaiomba mahakama hiyo ibatilishe uamuzi wa Baraza hilo la kuwavua uanachama Januari 4, mwaka huu, kwa madai kwamba, walikiuka katiba ya chama hicho.
Kabla ya uamuzi huo wa kuwavua uanachama, Januari 3, mwaka huu, Hamad Rashid na wenzake waliwasilisha ombi Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam chini ya hati ya dharura wakiomba mkutano wa Baraza Kuu la CUF uliokuwa ukitarajiwa kufanyika Zanzibar, uzuiwe kuwajadili.
Kupitia kwa mawakili wao, kampuni ya uwakili ya GF Law Chambers Advocates, walidai baraza hilo lina nia ya ama kuwasimamisha au kuwavua uanachama na kwamba, uamuzi huo ungeathiri haki zao za kikatiba.
Walida kuna kesi ya msingi ya madai namba 1/2012 waliyoifungua mahakamani hapo wakihoji muundo wa Kamati ya Nidhamu na Maadili ya CUF na uteuzi wa wajumbe wa kamati hiyo.
Tayari Jaji Shangwa katika uamuzi wake wa Januari 4, mwaka huu, aliamuru CUF kusitisha uamuzi wa ama kuwasimamisa au kuwavua uanachama walalamikaji hao.
Hamad juzi alirejea amri hiyo ya Mahakama Kuu chini ya Jaji na kueleza kwamba CUF waliikaidi na badala yake kuendelea na kutekeleza azma yake ya kuwavua uanachama.
Katika hati ya kiapo cha Hamad iliyowasilishwa mahakamani hapo, alidai kwamba baada ya mahakama kutoa uamuzi huo, wakili wake akisaidiana na mtumishi wa mahakama aliyemtaja kwa jina la Khatibu, waliwasilisha taarifa ya amri hiyo ya mahakama katika ofisi za CUF Buguruni saa 6:20 mchana. Hata hivyo, alidai afisa wa CUF aliyejulikana kwa jina la Mikidadi Nyandula alikataa kuipokea.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.