Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Saturday, January 21, 2012

Waziri awakimbia madaktari



•  Matibabu yasimama hospitalini

na Nasra Abdallah

NAIBU Waziri wa Afya, Dk. Lucy Nkya, jana alishindwa kutokea katika ukumbi wa DonBosco, Upanga, kuonana na madaktari takriban 500 kutoka hospitali zote za jiji la Dar es Salaam na mikoani.
Dk. Nkya alikuwa akutane na madaktari hao katika ukumbi huo kuanzia saa nne asubuhi ili kutafuta suluhu ya madai yao mbalimbali ambayo yamezua mvutano mkubwa baina yao na serikali.
Akitoa taarifa ya kutofika kwa naibu waziri huyo, makamu wa rais wa chama cha madaktari (MAT), Primos Saidia, alisema juzi walituma barua wizarani wakitaka kukutana naye na akakubali.
Alisema kutokana na kutokea kwa msiba wa Mbunge wa Arumeru Mashariki Jeremiah Sumari walilazimika kugharimia ukumbi mwingine wa Don-Bosco na kumpa taarifa ya mabadiliko hayo.
Majira ya saa nane za mchana, Tanzania Daima ambalo lilikuwepo ukumbini hapo muda wote wa kikao cha madaktari hao, lilimshuhudia makamu wa rais wa chama cha madaktari hao akisimama na kutoa taarifa ya kutofika tena kwa waziri huyo kuonana nao.
Saidia alisema kuwa alikuwa amepata taarifa kwa njia ya simu kutoka kwa Dk. Nkya ikimjulisha kutofika kwake, badala yake akataka akutane na madaktari hao katika ukumbi wa Anatoglou ndani ya nusu saa.
“Nimepigiwa simu na Waziri Nkya na kunitaarifu kwamba madaktari wamfuate Anatoglou na kuwa kama wasipotokea ndani ya nusu saa anaondoka zake,” alisema Saidia.
Taarifa hiyo iliwakasirisha madaktari hao ambao waliazimia kwa kauli moja kutotekeleza agizo la waziri huyo. Wakizungumza kwa hasira, baadhi yao walisema kuwa agizo la waziri huyo lilikuwa ni kitendo cha dharau kwao na kilichoonyesha kuwa hakuwa na nia ya kukutana nao kama alivyokubali tangu awali.
Walisema kuwa muda wa nusu saa alioutoa waziri huyo kutoka eneo hilo la Upanga hadi Mnazi Mmmoja, ulikuwa mdogo sana na ilikuwa dalili ya wazi ya kiongozi huo wa wizara kuwakimbia.
Kutokana na hatua hiyo, madaktari hao walipendekeza kuonana na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa vile viongozi wakuu wa Wizara ya Afya walikuwa wameshindwa kutimiza wajibu wao.
Mkutano huo ulioanza juzi, ulikuwa ni kwa ajili ya kujibu kauli ya serikali iliyotolewa dhidi ya madai yao ambapo walidai tamko hilo la Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii lilikuwa la kisiasa zaidi kuliko uhalisia.
Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (Mat) Dk. Namala Mkopi, alisema madai ya madaktari ni kuitaka serikali iwapatie nyumba za kuishi, kuongezewa posho za muda wa ziada za kazi ambazo sasa ni sh 10,000.
Akizungumza katika mkutano huo juzi, mjumbe wa Mat Dk. Hamis Kigwangalla alisema wanataka posho iwe sh 200,000 na mshahara wa kima cha chini uwe sh milioni 3.5.
Dk. Kingwangalla ambaye ni Mbunge wa Nzega (CCM), aliongeza kuwa madaktari wanayo haki ya kulipwa kiasi hicho cha fedha kwa kuwa serikali ina fedha na ndiyo maana imewaongezea wabunge posho za vikao.
Alisema imefika wakati taaluma ya udaktari iheshimiwe na kuthaminiwa kwani ni kazi ya wito huku akipendekeza kufutwa kwa utaratibu wa kutoa vibali kwa vigogo kwenda kutibiwa nje ya nchi, kwa madai kuwa ndicho kinachowatia kiburi viongozi wa serikali hadi kuwapuuza madaktari.
Aidha, chama hicho kinataka kurejeshwa kwa madaktari wote waliokuwa wakifanya mazoezi ya vitendo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kupitiwa upya uamuzi wa kuhamishwa madaktari bingwa 61 kutoka hospitali hiyo ya taifa.
Madaktari 194 waliokuwa wakifanya mazoezi ya vitendo Muhimbili waliondolewa na kupelekwa katika vituo mbalimbali baada ya kuibuka mgogoro wa malipo.
Hali ni tete hospitalini
Wakati madaktari hao wakiendelea na mkutano huo, habari za kuaminika zimebainisha kuwa hali katika hospitali za rufaa na mikoa ni tete kutokana na wagonjwa kukosa matibabu ya uhakika.
Taarifa zilizothibitishwa na chama hicho cha madaktari zimebainisha kuwa hospitali tano za rufaa nchini tayari madaktari hao wameshindwa kufanya kazi kutokana na kutolipwa fedha zao.
Akithibitisha taarifa hizo, Dk. Mkopi alizitaja hospitali hizo kuwa ni pamoja na ile ya Muhimbili, Bombo (Tanga), Mount Meru (Arusha), Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na hospitali ya manispaa ya Temeke.
Alisema katika maeneo ambayo madaktari wanaendelea na kazi ni kutokana na vituo, hospitali au halmashauri sehemu husika kuwakopesha wataalamu wao ili kuwawezesha kuendelea na maisha yao ya kila siku huku wakitoa huduma wakati ufuatiliaji ukiendelea serikali kuu.
Chama hicho pia kimebaini kuwa hali hiyo inaenea katika hospitali nyingine zenye madaktari na inaleta mzigo kwa madaktari bingwa na waandamizi na kuonya kuwa inaweza kuleta mgogoro katika fani yote ya udaktari nchi nzima.
“Chama kinatafsiri kitendo cha kutowalipa madaktari malipo yao na kuwafanya waishi kwa shida kwa muda huo wote kuwa ni kitendo cha dharau kwa fani ya udaktari na huduma wanazotoa kwa wananchi.
“Huu tunauita udhalilishaji wa hali ya juu kwa madaktari na namna serikali isivyojali huduma za afya kwa wananchi inaowaongoza,” alisema Mkopi.
Alisema chama kinalaani kitendo cha serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa jamii, kutowalipa madaktari malipo yao halali hadi kufikia mgomo unaowafanya wananchi kukosa huduma stahili za matibabu.
Dk. Mkopi aliitaka jamii na serikali ielewe wazi kuwa madaktari kuwepo kazini bila malipo kwa muda mrefu ni uvunjifu wa haki za binadamu, kinyume na kiapo cha udaktari na kusababisha utoaji wa huduma hafifu na vitendo vya uvunjifu wa sheria kama kukaribisha mazingira ya rushwa.
Alisema sehemu ya kiapo cha udaktari inasema: “Wakati nikishika kiapo ijaliwe kwangu kufurahia maisha na kazi yangu, jamii inikumbuke na kuniheshimu nikiwa hai au nimekufa. Dk. Mkopi alisema chama kinaona wataalamu hao hawana hatia ya uvunjifu wa kiapo chao katika kutoa huduma kwa Watanzania kutokana na serikali kutokutimiza wajibu wake kama inavyoelezwa kwenye kiapo na makubaliano ya kazi.
Aliwataka viongozi wa wizara na taasisi kuacha kutumia lugha za vitisho wakati kama huu hasa baada ya kushindwa kuwalipa madaktari stahili zao.
TUGHE yatangaza mgogoro na serikali
Kutoka Bukoba, Bigambo Jeje anaripoti kuwa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya Nchini (TUGHE) kimetangaza mgogoro na serikali na kuahidi kuifikisha mahakamani baada ya kuwapunguzia kima cha mishahara baadhi ya watumishi walioko katika ajira ya utumishi wa umma hivyo kuvunja sheria na kanuni zinazoongoza sekta hiyo.
Miongoni mwa wizara zinazokusudiwa kushtakiwa na TUGHE ni pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa sanjari na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma ambazo ama kwa makusidi au kutaka watumishi waichukie serikali yao, zimekiuka waraka na maagizo ya Katibu Mkuu Kiongozi.
Katibu Mkuu wa TUGHE nchini Ally Kiwenge ametangaza mgogoro huo mjini Bukoba baada ya kupata taarifa za watumishi mbalimbali wa serikali mkoa wa Kagera wakiwemo maafisa tarafa kuwa wamepunguziwa kima cha mishahara yao kwa kigezo cha kutokuwa na elimu ya shahada ya kwanza ya chuo kikuu, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Kiwenge alisema kuwa kwa mujibu wa Waraka Namba 1 wa Katibu Mkuu Kiongozi wa mwaka 2010, mtumishi yeyote mwenye cheo cha juu anaporejeshwa kwenye cheo cha chini, mshahara wake unabaki palepale na akafafanua kwamba katika hali yoyote ile ya mshahara binafsi, mtumishi hapaswi kurekebishiwa na kupangiwa mshahara mdogo bali anahama na mshahara wake.
Alisema kilichotokea kwa watumishi wa mkoa wa Kagera na mikoa mingine hapa nchini ni ukiukaji wa sheria za umma na kuwa moja kwa moja serikali imevunja sheria ya ajira na mahusiano kazini Na. 6 ya mwaka 2004 ibara ya 28 kifungu kidogo cha kwanza kinachomtaka mwajiri kupunguza au kukata mshahara wa mfanyakazi kwa malipo yaliyoidhinishwa kisheria kama kodi ya serikali na si vinginevyo.
Alisema baada ya kukamilisha zoezi la ufuatiliaji wa takwimu za wafanyakazi wote ambao ni wanachama wa chama hicho, waajiri wote walioenda kinyume na sheria hizo za utumishi wa umma watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka hayo na wale watakaotumia mali za serikali yakiwemo magari wakati wa uendeshaji wa kesi hizo, watawashtaki kwa kutumia vibaya mali za nchi.
Kufuatia tangazo hilo Kiwenge amewaagiza makatibu wote wa chama hicho mikoa yote ya Tanzania Bara kuendesha zoezi la kukusanya na kuhakiki madai ya wafanyakazi wa serikali kuu na afya waliopunguziwa mishahara na waajiri wao kwa makusudi, kabla ya TUGHE makao makuu kuishtaki serikali mahakamani.

Na Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.