Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Saturday, January 14, 2012

Ufisadi wa aina yake-Urambo

LAITI MHESHIMIWA SITTA ANGEJUA URAMBO INAVYOTAFUNWA VITA YA UFISADI ANGEIHAMISHIA JIMBONI MWAKE

Nduguwana Jf,
Kupitia safu hii napenda niufahamishe umma wa watanzania na hasa tume ya maadili ya viongozi na TAKUKURU ngazi ya taifa, Mkoa na wilaya ya Urambo.
Mwaka mmoja uliopita Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo alifanya sherehe na watumishi wake kujipongeza eti wamepata hati safi ya ukaguzi toka kwa Mkaguzi wa hesabu za serikali nilishangaa sana kwa jinsi ninavyofahamu matumizi mbaya ya fedha katika halmashauri yetu. Nililazimika kuamini kuwa kupata hati safi ni ufundi wa kuandika uwongo na si hali halisi, kwani matumizi ya kuanzia wakuu wa idara na vitengo hadi Mkurugenzi matumizi yao hayalingali na hali halisi ya vipato vyao wamekuwa ni watu wakulipuka ki-maendeleo ya ghafla unaweza kudhani watu wapo kwenye mgodi wa dhahabu au almasi lakini ajabu bado watu wakapewa hati safi!

Kubwa kuliko yote ni pale Mkurugenzi alipotumia milioni zaidi ya mia tano kwa kununua Katapila bovu na gari bovu na madiwani hawana uwezo wa kumdhitibiti kwa kuwa vitu vyote hivyo vimenunuliwa kwa idhini yao baada ya kuwa wameletewa taarifa nzuri wakati hali halisi haikuwa hivyo, na hata hivyo madiwani wanakosa nguvu kwa kutopata sapoti kutoka kwa wabunge wao ambao ni wenye uelewa mpana zaidi kuliko wao. Katapila pamoja na gari lililonunuliwa kwa matumizi ya Mkurugenzi kwa Mamilioni halijatembea muda mrefu limepaki.

Tofauti na magari yote ya Wakurugenzi waliomtangulia, gari hili toka limeletwa limekuwa likipelekwa kwenye matengenezo mara kwa mara ili kujiongezea ulaji, na kama ilivyokuwa kwenye gari, katapila lenyewe hata miezi mitatu haikupita likapaki mpaka leo. Mheshimiwa Sitta ameingia kwenye vita kali sana ya kupambana na mafisadi kiasi cha yeye mwenyewe kuishi kwa mashaka na kubadili namba za simu kila mara kama alivyodai mwenyewe kwenye mahojiano na ITV kwa kuhofia maisha yake, lakini hawa ambao wanaiangamiza Wilaya yake ambayo wananchi wa hapo ndiyo waliomchagua na kumfanya afahamike nchi nzima mbona hawachukulii hatua yoyote kwa uhujumu wanaoufanya?

Mwandishi mmoja wa gazeti aliwahi kuandika kuwa haoni usafi wa Sitta ambaye amejizolea sifa kwa watanzania kuwa yeye ni mtu safi hapendi kuona watanzania wakidhulumiwa haki zao wakati yeye ameng’ang’ania kuishi kwenye nyumba ya Spika inayolipiwa mamilioni ya walipa kodi wa Tanzania na wakati huo huo kusababisha nyumba ya mama Makinda kujengwa kwa dharula ili iwe na hadhi ya kuishi Spika wa Bunge la Tanzania. Nalazimika kuamini maneno ya mwandishi huyo kwa kuwa sasa inawezekana atakuwa anapata ten percent ya manunuzi ya vitu vibovu katika halmashauri ya Urambo.

Na hata hati safi waliyoipata hadi kusherekea usiku kucha mwaka uliopita naamini ni ya kuchakachua kwani kwa mambo yanayofanyika Urambo haihitaji kuita wakaguzi toka nje ya nchi kuja kufanya ukaguzi mambo yako wazi zaidi hata mhasibu wa kawaida atagungundua madudu yaliyopo lakini cha ajabu Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa fedha za Serikali eti akatoa hati safi. Mimi naamini kabisa Mkaguzi na Mdhibiti wa fedha za Serikali alihongwa ili amsafishe Mkurugenzi wa Wilaya ya Urambo, lakini kwa usahihi Urambo haiwezekani kupata hati safi hata siku moja mpaka hapo mafisadi wote watakapoondolewa. Kama David Jairo amechangisha fedha kinyume cha utaratibu na akajilipa milioni nne kwa siku tatu na CAG alipotumwa kumkagua akasema hakuna matumizi mabaya ya fedha za Umma, atashindwa nini kumlinda Mkurugenzi wa Wilaya ya Urambo wakati wanatoka Mkoa mmoja? Nimesema hati safi waliyopata ni ya kuchakuchua kwani hali iliyopo sasa Tanzania hakuna kinachoshindikana imebaki kulindana tu.

Mimi sijaona halmashauri ikipata hati safi Mkurugenzi anafanya sherehe, anasherehekea nini ambacho siyo cha kawaida? Maana kupata hati safi ni wajibu wake na siyo jambo la hisani wala la kubahatisha mpaka apate mshituko kwa kuona kuwa pamoja na uovu alioufanya wa kuiba fedha za halmashauri, amefanikiwa kuingizwa kwenye kundi la waaminifu wakati yeye siyo mwaminifu na ndiyo maana ya kufanya sherehe hiyo. Kwanza sherehe hiyo aliifanya kwa bajeti gani ya watu kula na kunywa usiku kucha wakati baadhi ya wafanyakazi wakiomba hata nauli ya kwenda kusoma na kwenye matibabu hawapati? Ni wafanyakazi wangapi wa halmashauri ya Wilaya ya Urambo wamenyimwa fedha za kwenda kusoma lakini za kusherehekea wizi uliobarikiwa na CAG zikapatikana?

Mkurugenzi ni jeuri na anafanya mambo yake anavyotaka mwenyewe kwa kuwa anakingiwa kifua na Mheshimiwa Sitta, kiasi cha kuwatisha madiwani wanaohoji matumizi na safari zake. Kwa mfano diwani mmoja alihoji kwanini Mkurugenzi anatumia fedha nyingi kila mwezi kwenda KCMC kufanya uchunguzi wa afya yake wakati fedha hizo zingeweza kuokolewa kwa kumuhamishia Moshi mkurugenzi huyu ili awe karibu na matibabu? Mbona baadhi ya watumishi mbalimbali wakiwemo Walimu wenye matatizo huhamishiwa mahali popote ambapo huduma ya aina ya matibabu anayotakiwa kupata ipo? Sasa kwa Mkurugenzi huyu imeshindikana nini kufanya hivyo? Au analindwa na nani kwa kipi kizuri anachoifanyia Wilaya ya Urambo? Kwa kuona madiwani hawapati sapoti kutoka kwa wabunge wao sasa hivi wanashughulika na mambo yao tu na kuacha kila mtu afanye atakavyoweza kujinufaisha binafsi.

Kumekuwa na tabia iliyohalalishwa na Mkurugenzi katika halmashauri hii kwa wafanyakazi wa ngazi ya juu na ngazi ya kati, kukiuka kwa makusudi taratibu na miiko ya uongozi baada ya kuona kiongozi wao anayofanya. Idara ya elimu wapo watumishi watatu, wawili idara ya ukaguzi na mmoja ni Afisa elimu vifaa na takwimu.

Nitaanza na afisa elimu vifaa na takwimu ambaye ndiye kinara wa hujuma iliyowazi akishirikiana na Mkurugenzi wake kuhalalisha uovu huo, kwa muda wa miaka mitatu mfululizo amewaamuru walimu wote wa Wilaya hii kwamba kazi zote za uchapaji kuanzia mitihani na taarifa mbalimbali lazima zikachapwe kwake, mwalimu asiyepeleka kazi kwake atakiona cha moto kwa kutopitishiwa malipo yake hata kama ni ya halali na ni haki yake, kwa kuwa yeye ni mwenye saini ya akaunti ya Idara ya Elimu kwa hilo walimu hatuna ujanja na bado tunashangaa jambo hili linawezaje kufanyika wakati vyombo vyote vipo vilivyowekwa kudhibiti ukiukwaji wa kanuni za utumishi.

Mwaka juzi aliagiza shule zote zinunue flash disk zimpelekee kwa ajili ya kutunza na kutayarisha taarifa za MMEM,Walimu walitekeleza agizo hilo la kifisadi na wakamkabidhi hizo flashdisk ambazo baada ya kazi hazikurudishwa shuleni zikawa mali yake. Mwalimu aliyepeleka kuchapa taarifa ya MMEM sehemu nyingine ilikataliwa kwa kisingizio kuwa ina makosa, kazi hiyo ilikubalika kwake ikiwa imechapwa na mke wa afisa huyo kwa gharama kubwa isiyolingana na kazi yenyewe lakini kwa kuwa yeye ndiye mwenye kupitisha malipo hakuna aliyehoji, kwani yeye na Mkurugenzi wanashirikiana kuhujumu halmashauri ya Wilaya ya Urambo. Jambo hili lina ushahidi wa wazi lakini mamlaka zilizopo zimeshindwa kudhibiti kwani ukichunguza hundi zote zinazolipwa kwenye kampuni yake inayoitwa SAVENA SECRETARIAL amezisaini yeye mwenyewe sasa hili nalo linahitaji tume? Kwa uthibitisho mashahidi wa kwanza watakuwa ni benki kwani hundi hizo ziko benki.

Afisa elimu wake aliyehamia Igunga alikuwa akikataa kuzipitisha kwa maelezo kwamba haiwezekani kazi zote za uchapaji kwenye idara ya elimu wilaya nzima zifanywe na yeye ambaye ni kiongozi na mweka saini katika idara hiyo, lakini yeye kwa jeuri aliyopewa na Mkurugenzi aliamua kujisainia hundi hizo hatimaye afisa yule alihamia Igunga, akaja mwingine akajaribu kumuelewesha lakini huyu bwana ameshabinafsishiwa wilaya hii hakuelewa kitu, tena ikafika siku moja akamtukana Afisa elimu mbele ya walimu waliokuwa wamekuja kupata huduma ofisini kwao, hali hiyo ilimfanya afisa elimu huyo kujiuliza inakuwaje afisa huyu anakosa nidhamu kwa kiongozi wake, jibu alilopata ni kwamba huyu bwana anakula sahani moja na Mkurugenzi hivyo ni vigumu kumdhibiti kwa hiyo anaendelea kujifanyia atakavyo.

Afisa elimu wa pili naye anashindana na huyu mwenzake kwa kuvunja kanuni na maadili ya uongozi yeye baada ya kuhamia hapa alimkuta mwenzake akivunja taratibu hizo na yeye akaamua kufungua ofisi haraka haraka akaiita jina lake Manjoli Secretarial kukaanza mapambano na afisa elimu vifaa na takwimu ya kugombea wateja ambao ni Walimu wakuu wa shule kupeleka kazi za uchapaji wale waliopeleka kazi kwa afisa elimu ukaguzi hundi zao hazikupitishwa na afisa elimu vifaa na takwimu kwa visingizio mbalimbali.

Lakini kubwa likiwa ni kuwaonyesha jeuri kwamba kwanini wamepeleka kazi kwa mtu mwingine, na huyu afisa elimu ukaguzi alifikia mahali naye akaanza kuwatisha walimu kuwa atawaandikia ripoti mbaya ya ukaguzi ikiwa hawatapeleka kazi kwake na imefikia hata kipindi cha kupiga picha za wanafunzi wa darasa la saba anakwenda shule kwa shule kupiga picha kwa kuwalazimisha walimu wawaandae wanafunzi awapige picha muda wa kazi, lakini kama nilivyosema Urambo ni yatima hakuna anayeuliza inakuwaje muda wa kazi za serikali mtumishi wa serikali anafanya kazi zake binafsi pasipo kuhojiwa na ikifika mwisho wa mwezi ndiyo wakwanza kuchukua, hivi kwenye logi book anapofika kwenye hizo shule anasaini kweli?

Je, ni lini mkaguzi akaenda kukagua shule akiwa peke yake tena wilaya nzima? Katika hali kama hii Elimu lazima itashuka kwani viongozi hawaheshimiki na wanaowaongoza kwakuwa haiwezekani mtu ufanye naye biashara wakati huohuo umkague na kutoa taarifa sahihi ya mapungufu yake, lazima taarifa hiyo itakuwa na upendeleo kwa kuhofia kuvunja uhusiano wa kibiashara ambao ni uhusiano binafsi na ambao ni muhimu zaidi kuliko kazi ya serikali.

Afisa elimu wa tatu yeye pia ni mkaguzi na ni kabila moja na Mkurugenzi yeye amefika mahali vyombo vya ofisini anavitumia kufanyia biashara zake hapo hapo ofisini kwa kutumia kompyuta za ofisi na printa zake kwa kuchapa vitambulisho vya watumishi wanamlipa, kadi za harusi na mialiko mbalimbali wino ukiisha unanunuliwa kwa fedha za serikali wakati mtu kajifanyia kazi zake binafsi kwa kutumia vifaa vya serikali.

Haya yote yanafanyika viongozi wao wapo lakini wanapewa rushwa kuhalalisha uovu huu na mpaka ninapoandika barua hii kuna makundi mawili makubwa ya walimu wakuu wapo mashabiki wa SAVENA SERCRETARIAL na MANJOLI SECRETARIAL lakini wengi wakiwa kwa afisa elimu vifaa na takwimu ambaye anaweza kumwambia mwalimu aandike hundi pasipo kazi na manunuzi hewa akaipitisha na hivi sasa kuna mkakati wa kumchagua mtu mmoja atakayekuwa anauza vitabu wilaya nzima ili waweze kudhibiti fedha zote za vitabu kupitia kwa mtu huyo.

Ifahamike wazi kwamba ufisadi unaofanyika Urambo ni mbaya kama wa Richmond na Dowans ambao Mzee Sitta amejitoa mhanga kupambana nao kwa maneno bila vitendo, lakini vipi anashindwa kubaini ufisadi unaofanyika kwenye wilaya lilipo jimbo lake? Hapa kuna siri nzito haiingii akilini kuona mtu mwenye nguvu kama yeye anayeogopeka serikalini na mawaziri wenzake, anayeweza kupambana na mafisadi papa atashindwaje kupambana na hawa wezi walioishika halmashauri ya Urambo kama kampuni yao!! Hakuna hapo siyo bure wanafanya hayo kwa baraka za Sitta, Sitta ni wa Ki-mataifa siyo wa kushindwa kudhibiti viongozi wa ngazi za wilaya. Kinachofanyka Urambo utafikiri serikali hakuna wako wapi watu wa utawala bora au huu ndiyo utawala bora wa serikali ya Kikwete?

Kuthibitisha uwezo alionao Mheshimiwa Sitta wa kupambana na mtu yeyote asiyemtaka Wilayani kwake ni tukio la hivi karibuni kwenye kikao cha baraza la madiwani wa Wilaya ya Urambo Mheshimiwa Sitta alikuwepo na kulitokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya wajumbe wa kikao hicho juu ya utendaji kazi wa Afisa wa Takukuru-Urambo, kwa kuonyesha ubabe wake mbele ya kikao hicho aliamuru afisa huyo aitwe ili aje kujibu tuhuma zake alizotuhumiwa na wajumbe wale, palepale kwenye kikao, lakini Mwenyekiti wa halmashauri alimfahamisha Mheshimiwa Sitta kuwa kauli yake inaaminika kwa hiyo haina sababu za kumuweka kiti moto afande huyo wa Takukuru.

Baada ya kutoka nje ya ukumbi wa halmashauri kilichofanyika ni kwamba Dk. Hosea alipigiwa simu na Mheshimiwa Sitta na kuamuriwa amhamishe mtumishi huyo wa Takukuru, jambo ambalo Dk. Hosea alilitekeleza mara moja, naye siku hiyo hiyo akamuamuru afisa wake ahamie Wilaya ya Meatu wakati akiwa likizo, amemaliza likizo akaenda kituoni kwake. Sasa kwa uwezo huohuo alioutumia kwa afisa wa Takukuru ni vipi kashindwa kuwadhibiti Mkurugenzi na maafisa elimu wake mpaka wanaifanya Urambo kuwa Kampuni yao? Hali hii narudia tena kusema kuwa Mheshiwa Sitta anajua kinachoendelea.
Mwisho nasema kama ni kweli kama tunavyotangaziwa na Serikali yetu kila siku watanzania kuwa kuna vyombo vya kudhibiti viongozi wanapovunja taratibu. Naomba tena kama ni kweli TAKUKURU wanapambana na rushwa kama wanavyojinadi wachunguze yafuatayo kwa SEVENA SECRETARIAL na MANJOLI SECRETARIAL:-

  • Waende benki wangalie hundi zinazolipwa kwa SAVENA SECRETARIAL zinalipwa kwa kazi gani na zimesainiwa na nani.
  • Pili wachunguze malipo yaliyofanyika kwenye kampuni ya Jackson Nungu ambaye alikuwa akiuza vifaa vya ujenzi na amehamia Mwanza lakini utaona amelipwa hundi kwa ajili ya kuchapa mitihani wakati ofisini kwake hakuna hata sura ya kuwekwa photocopy mashine au compyuta na hata leseni yake ni ya kuuza vifaa vya ujenzi tu, na hundi hizi zilikuwa ni za SAVENA SECRETARIAL na nyingi kati hizo zimesainiwa na Sadoki Magesa ambaye ni mmiliki wa SAVENA SECRETARIAL na ndiye afisa elimu vifaa na takwimu.
  • Waende SAVENA SECRETARIAL watakuta kuna fomu za likizo, fomu za uhamisho na fomu za uhamisho wa wanafunzi ambazo walimu wanalazimika kuzinunua hapo, wakati wakinunua sehemu nyingine hazisainiwi na afisa huyu kwa nini? huu ndiyo utaratibu wa maofisa wa umma kutumia ofisi za umma kufanya biashara? Je, sekretaeti ya maadili ya viongozi ipo kweli au tunadanganyana tu?
  • Waende MANJOLI SECRETARIAL waangalie hundi ngapi zimelipwa kwenye akaunti yake na kwa kazi gani
  • Waangalie mahudhurio kazini mwezi wa pili mwishoni mpaka wa tatu alipangiwa na nani akafanye kazi gani katika tarafa za Kaliua na Ulyankulu na baada ya kufika kwenye shule hizo alisaini kwenye kitabu amefika hapo kufanya nini.
  • Waulize ni wafanyakazi wangapi wametengenezewa kadi na vitambulisho ofisini na walilipa shilingi ngapi kwa nani na risiti walizopewa kwa biashara hiyo zimeandikwaje? TRA wametoa TIN namba kwa halmashauri kufanya biashara ofisini? Afisa biashara ametoa leseni kwa halmashauri kufanya biashara? Je, ni utaratibu kumlipa mtu binafsi anayetumia vifaa vya ofisi ya umma kwa manufaa yake binafsi?

Mzee Sitta wawezaje kukitoa kibanzi kilichoko kwenye jicho la mwenzio (RICHMOND NA DOWANS) wakati boriti iliyoko kwenye jicho lako (URAMBO) hujalitoa? Tunaomba kama kweli hauhusiki katika haya ruhusu, vyombo vyote vya dola Polisi, Takukuru, na Tume ya maadili ya viongozi viyafanyie kazi mambo haya pasipo kuingiliwa na wewe, na ukweli utathibitika)

Mwalimu mwenye uchungu
S.L.P. 170
Urambo

Source: JF

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.