Regia alimkwepesha pacha wake na ajali
PACHAwa Mbunge wa Viti Maalum Chadema, Regia Mtema (32) aliyefariki juzi kwa ajali ya gari eneo la Ruvu mkoani Pwani, Remija Mtema (32) ameeleza alivyonusurika baada ya kushuka kwenye gari muda mfupi kabla ya ajali.
Akizungumza na gazeti hili jana, Remija ambaye ni kurwa, alisema Regia kabla ya ajali iliyosababisha kifo chake, alikuwa akitoa kauli za kutia moyo na za kutarajia kuonana tena.
“Tulitoka nyumbani kwake Mbezi-Makabe, Dar es Salaam kwenye saa tatu asubuhi, mimi nilikuwa nakwenda Iringa na tuliondoka na gari lake hilo lililopata ajali nyumbani hapo, wakanishusha Mbezi stendi nisubiri basi la Iringa .
“Wakati tunatoka nyumbani alikuwa anaongea kwa uchangamfu sana, kwanza juzi (Ijumaa)
tulizungumza na kupanga kwamba mimi niende Iringa kuomba ruhusa kazini, maana kuna wakati nikiwa huru namsaidia kazi kama Katibu wake, tulipanga nikipewa ruhusa nirudi nimsaidie kwenye Kamati na Bungeni,” alisema Remija.
Kwa mujibu wa Remija, walikubaliana hivyo na baada ya kupanga mambo yao usiku huo wa
Ijumaa, walicheza sana karata.
“Ni karata za kuagana maana mimi ndio nilikuwa nasafiri kesho yake kwenda Iringa, asubuhi ndio tukaondoka huku tunacheka, mimi nikashukia Mbezi, alikuwa ni zaidi ya pacha wangu, alikuwa rafiki yangu,” alisema Remija.
Remija ambaye ni Ofisa Tarafa wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, alisema aliposhuka Mbezi
kusubiri gari, walikaa nae na watu wengine kwenye gari kwa karibu saa moja wakimsubiri mama yao, Bernadeta aliyekuwa akitokea Tabata-Chang’ombe nyumbani kwao.
“Mama alipofika aliingia garini na wakaondoka, pacha akasisitiza nikipata usafiri niwaambie, ni
kama alitamani niendelee nao lakini haikuwa hivyo, baada ya muda wa nusu saa mama alipiga simu kuniuliza kama nimepata basi maana waliona basi la Upendo limewapita, nikamjibu bado, baada ya muda mfupi nikapata basi la Budget,”
“Nilipoingia kwenye basi saa tano asubuhi hivi, nikamtumia ujumbe Regia kuwa nimepata basi, lakini ujumbe haukujibiwa, nikajua labda kwa kuwa alikuwa anaendesha gari, nikaendelea kusoma gazeti na tulipofika Ruvu niliona watu lakini sikutilia maanani nikaendelea kusoma gazeti,” alisema Remija.
Alisema kabla hajafika Chalinze, alipigiwa simu na mama yake kuwa wamepata ajali na
wapo Hospitali ya Tumbi na kumuomba dereva ashuke kwa kuwa ndugu zake wamepata ajali
Ruvu.
“Dereva na kondakta waliniuliza aina ya gari, nikawaambia wakathibitisha waliiona. akasimamisha gari nikashuka na kuanza safari ya kurudi hadi Hospitali ya Tumbi, nikakuta kweli Regia amefariki,” alisema Remija.
Alisema pacha wake alikuwa jasiri ambaye akiamua jambo lake ni lazima alifanye, alikuwa na huruma asiyependa mtu aonewe na alimuamini Mungu kwa kila jambo kutokana na malezi ya kiimani waliyopata kwa baba na mama yao mlezi.
Kwa mujibu wa Remija, yeye na pacha mwenzake walizaliwa Hospitali ya Ocean Road, jijini Dar
es Salaam Aprili 21 mwaka 1980, alikuwa mpenzi na shabiki wa timu ya mpira wa miguu ya Simba kwa hapa nchini na kwa nje alikuwa akipenda kufuatilia Barcelona ilipocheza zaidi ya timu nyingine.
Baba wa marehemu, Estelatus Mtema aliliambia gazeti hili jana kuwa anamshukuru Mungu kwa
kila jambo na kuomba majeruhi akiwemo mkewe waliolazwa hospitali ya Taifa ya Muhimbili walikohamishiwa wakitokea Tumbi juzi jioni, wapone mapema.
Utaratibu wa maziko
Mtema alisema misa itafanyika leo saa tisa alasiri katika Kanisa Katoliki la Segerea pamoja na heshima za mwisho na kesho kutakuwa na heshima za mwisho katika ukumbi wa Karimjee.
Alisema bada ya hapo safari ya kulekea Ifarakara itaanza na maziko yatakuwa Jumatano huko
Ifarakara mjini nyumbani kwa wazazi wa marehemu.
Majeruhi Muhimbili
Mtoto wa binamu wa mama wa marehemu, Theresia Simon, ambaye ilidaiwa kuwa amefariki
kutokana na kujeruhiwa vibaya kichwani, anaendelea vizuri alikolazwa wodi namba 10 Kibasila.
Theresia katika mahojiano, alisema anamshukuru Mungu hali yake inaendelea vizuri na maumivu yamepungua.
Baadhi ya vyombo vya habari jana, viliripoti kuwa Theresia aliyejeruhiwa kichwani, alikufa hivyo kufanya idadi ya walioaga dunia kuwa wawili akiwemo Mbunge Mtema.
Shangazi yake, Consolata Mwandenga alisema pia kuwa alimpa uji jana na kula vizuri asubuhi na mchana hivyo hali yake ni njema. Pia mama wa marehemu, Bernadeta na watu wengine
wawili, wanaendelea vizuri na wote wamelazwa katika wodi hiyo.
Vikao vya dharura Chadema
Wakati huo huo Sekretarieti ya Chadema jana ilifanya kikao cha dharura chini ya Uenyekiti wa Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa kupanga utaratibu wa chama na viongozi wake wakuu, kushiriki kikamilifu kwenye maombolezo, heshima za mwisho na hatimaye maziko yaliyopangwa kufanyika Ifakara.
Shughuli hizo za mazishi ya heshima kwa Mbunge huyo, kwa mujibu wa taarifa za Chadema, zitaongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Freeman Mbowe.
Mbali na Sekretarieti, pia Kamati ya Uongozi ya Wabunge wa Chadema, ilifanya kikao cha
dharura, kwa kuzingatia uzito wa msiba uliotokea na kupitisha azimio kwamba wabunge wote wa Chadema washiriki kutoa heshima ya mwisho.
Kwa mujibu wa azimio hilo, wabunge wote wa chama hicho watasindikiza mwili wa Regia
hadi Ifakara na kushiriki maziko.
No comments:
Post a Comment
Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.