Katika hali ambayo inaonesha kuweza kuja kulitetemesha taifa kupita kiasi mtu anayejiita “Daudi Balali” ameanza kuzungumza kupitia mtandao wa Twitter akijaribu kuwaamsha Watanzania kuwa taarifa za kifo chake zilikuwa za uongo na kuwa huko aliko yu mzima salama salimini. Daudi Balali “huyo” alianza kuandika kwenye mtandao huo wa intaneti ambao umekuwa maarufu duniani kwa kuweza kutoa taarifa za watu mbali kwa haraka zaidi na kwa maneno machache zaidi.
Balali alianza kuandika mwezi Disemba tarehe 6 mwaka jana kwa maneno machache tu akisema kuwa “Its time to go home” yaani “Wakati wa kwenda nyumbani umefika”. Kwa maneno hayo machache mtu huyo ajiitaye Balali alianza pole pole kudokeza kuwa taarifa ambazo serikali ilizitoa kuwa “amefia” Marekani hazikuwa na ukweli wowote na kuwa ilikuwa ni sehemu ya njama za kimataifa za kumnyamazisha kufuatia kuibuliwa kwa wizi mkubwa katika Benki Kuu ya Tanzania wakati yeye alipokuwa Gavana wa Benki Kuu.
Daudi Balali alikuwa ni Gavana wa Benki Kuu baada ya kuletwa nchini na aliyekuwa Rais wa Tanzania Bw. Benjamin Mkapa kuwa Mshauri wa Rais pale Ikulu. Baada ya muda mfupi Ikulu Balali alipewa nafasi ya kusimamia taasisi kubwa kabisa ya fedha nchini ambayo ina wajibu wa kusimamia uchumi wa Tanzania yaani Benki Kuu. Ilikuwa ni chini ya Gavana Balali wizi wa aina mbalimbali ukihusisha magenge ya kimataifa ya mitandao ya kihalifu ambayo yalikuwa yanafanya kazi nchini kwa kushirikiana na wanasiasa, wataalamu na wana usalama mbalimbali.
Katika ya kashfa zote kubwa ambayo ilionekana kutishia usalama wa nchi na utawala ulio madarakani ni ile inayojulikana kama Kashfa ya EPA. Wakati wa Gavana Balali makampuni mbalimbali nchini yaliwasilisha Benki Kuu hati za kujitambulisha kuwa yamepewa haki ya kisheria ya kufuatilia madeni ya makampuni ya nje ambayo yalikuwa yanaidai Benki Kuu ya Tanzania kutokana na sababu mbalimbali za kiuchumi. Makampuni hayo ya Kitanzania yalipatiwa taarifa za ndani ya madeni hayo na watu kutoka ndani ya Benki na yakafanikiwa kukusanya baadhi ya wanasiasa na wafanyabiashara nchini ambao waliunda kwa haraka haraka makampuni feki ya kudai madeni hayo kwa “niaba” ya makampuni ya kigeni.
Katika hali ambayo ilishtua Kampuni ya Kimataifa ya Ukaguzi wa Fedha ya Deloitte and Touche ambayo iligundua kutokupatana kwa taarifa mbalimbali za makampuni hayo. Kampuni hiyo iliandika taarifa yake kwa Gavana kuelezea kutokupatana huko na kushangazwa ni jinsi gani watu wa Benki kuu walishindwa kuona tofauti hizo. Hata hivyo katika hali ya kushangaza kampuni ya Deloitte and Touche iliondolewa kufanya kazi hiyo.
Hata hivyo siri ilikuwa tayari wazi. Makampuni 22 yalijipeleka Benki Kuu na kuwasilisha vielelezo mbalimbali vya ulaghai na watu wa Benki Kuu wakiwa na akili timamu na wenye elimu ya juu kabisa wakawapatia kiasi cha dola milioni 133 kwa urahisi kabisa. Waliochukua fedha hizo wakazibadilisha huku wengine wakizihamisha nchini. Kampuni maarufu kati ya hizo 22 ni kampuni ya Kagoda Agriculture Limited ambayo peke yake ilichotewa zaidi ya dola milioni 40 kutoka Benki Kuu!
Kuibuliwa kwa kashfa hiyo ambako kulipigiwa kelele vikali na viongozi wa upinzani Tanzania kulielekea kutishia watawala ambao walijitahidi kutafuta namba ya kukabiliana kwani ukweli ulikuwa ni mgumu kuukana. Kwamba, kuna fedha zilichotwa Benki Kuu hakukuwa na shaka; kwamba makampuni yaliyochotewa fedha hizo yalikuwa ni feki hakukuwa na shaka; kwamba kulikuwa na njama ya hali ya juu kufanikisha hilo bila kushukiwa na vyombo vya usalama nalo halikuwa na shaka. Serikali ikajikuta iko kwenye matatizo.
Lakini kilichounganisha vitu vyote ilikuwa ni taarifa iliyotolewa na kundi lisilojulikana ambalo kwa mara ya kwanza liliwachorea Watanzania picha ya mtandao wa uhalifu wa kiuchumi (economic criminal ring) ambao unafanya kazi Tanzania. Taarifa hiyo ilionesha kuwa mtandao huo unahusisha wafanyabiashara kadhaa wa Kitanzania pamoja na watendaji wa ngazi za juu serikalini ambapo kinara alikuwa ni Gavana wa Benki Kuu Bw. Daud Balali. Taarifa hizo zilidakwa na wapinzani na Dr. Wilbrod Slaa wakati huo akiwa Mbunge wa Karatu alihoji juu ya taarifa hizo katika Bunge ambapo mwanzoni aliyekuwa Spika Bw. Samwel Sitta alijaribu kupuuzia kuwa ni taarifa za “mtandaoni”.
Hata hivyo, madhara yalikuwa yamekwisha fanyika. Pamoja na juhudi zote za serikali kujaribu kupuuzia na kuonesha kuwa siyo jambo kubwa ilikuwa vigumu kuwashawishi Watanzania kuwa madai ya wapinzani na Watanzania wengine yalikuwa ni ya “kisiasa” tu na ya “kutafuta umaarufu”. Hatimaye, Gavana Balali aliitwa Dodoma ambako alikutana na viongozi mbalimbali. Hiyo ilikuwa ni baada ya kufanya mkutano na waandishi wa habari ambapo alikanusha kabisa kuhusika na wizi huo na kudai kuwa kilichokuwa kinaelekezwa kwake ni njama za “wafanyabiashara” ambao hawakufurahia alivyokuwa anasimamia Benki Kuu.
Alipotoka Dodoma kwa ndege ya Serikali Balali “alitoweka” nchini. Siku chache baadaye taarifa zikatangazwa kuwa amepelekwa Marekani kwa matibabu japo siku ya kuondoka na namna alivyoondoka hakuna ambaye alikuwa tayari. Na huo ndio ulikuwa mwisho wa Balali kuonekana Tanzania. Taarifa zikaanza kutokea kila baada ya siku chache juu ya maendeleo ya “hali” yake huku nchi ya Marekani ikitoa ofa kwa serikali ya Tanzania kuwa kama wanamtaka Balali ingeweza kumsaidia kumleta nchini. Serikali haikuwaomba Marekani kufanya hivyo.
Kama wiki moja hivi kabla ya “kifo” chake taarifa za mpango wa geresha ya kifo zilivuja kutoka vyanzo vya ndani sana ambavyo vilidokeza kuwa Balali alikuwa atangazwe kuwa amekufa kwa “ule ugonjwa” na atazikwa huko huko “Marekani”. Na kweli siku chache baadaye taarifa kuwa Balali amefariki dunia zilitangazwa na kama ilivyokua kwenye mambo mengine taarifa hizo hazikukubaliana. Serikali ya Tanzania ilitangaza kuwa Gav. Balali ambaye alikuwa analipiwa matibabu na serikali alikuwa amefia kwenye “hospitali moja huko Boston” japo taarifa zilizotolewa kwenye “msiba” huko Washington DC zilidai kuwa amefariki katika hospitali ya Chuo Kikuu cha Georgetown ambako alisomea miaka kama arobaini iliyopita.
Katika hali ambayo ilitarajiwa (na kinyume na desturi ya misiba mingi ya Watanzania) mwili wa Balali haukuoneshwa kuagwa na hakuna mtu yeyote wa nje (asiye mwana familia) ambaye amewahi kuonesha aidha Balali akiwa mgonjwa hospitali au mwili wake ukiwa unaagwa. Na kinyume na kawaida nyingi za Watanzania wanaofariki nje ya nchi mwili wa Balali haukurudishwa nchini kwa mazishi. Taarifa nyingine ambazo zimekuja miaka karibu miwili tangu taarifa za kifo cha Balali zitolewe zimedokeza kuwa Balali aliruhusiwa kutoka hospitalini na kwa miezi mitatu alikuwa akiugulia nyumbani. Hizo nazo zilikinzana na taarifa za serikali kuwa Balali alikuwa ameugulia hospitali hadi mauti yalipomkuta.
Hivyo, kuibuka kwa “Balali” kunaelekea kuibua mjadala mwingine kabisa kama kweli alikufa kama ilivyotangazwa au alitoweshwa na kufichwa mahali akiahidi ukimya. Maandishi ya Balali wa mtandao wa “twitter” yanaonesha kuwa kama kweli ndiye Balali wa BoT basi huko aliko amechoshwa. Dalili ya hali ya kutokukubali (defiance) ya Balali wa twitter inatukumbusha jinsi alivyojitokeza hadharani kuzungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa juma la pili la mwezi Julai 2007 akikanusha vikali madai kuwa alihusika na wizi wa EPA.
Baadhi ya watu wanaamini kuwa ilikuwa ni maneno yake yale ya hadharani ambayo yaliwashtua wahusika mbalimbali kuwa Balali hakuwa tayari kubebeshwa zigo la Kagoda na kama wangemuachilia kwa hakika angemwaga ugali, kumwaga mboga, kuvunja masufuria na kuchoma jiko!
Maandishi ya Balali wa twitter yanaonesha kuwa ni mtu ambaye anaamini amedhulumiwa haki yake ya kusema ukweli na kuwa huko aliko anajuta kuondoka Tanzania katika mazingira ya alivyoondoka. Akiandika siku ile ya kwanza ya Disemba 6, 2011 Balali wa twitter anaandika “I didn’t die, I’m not dead” kwamba “sikufa, niko hai”. Baadaye aliandika “I miss home” na kuwa “the Big 6 and the Architect said I died” akimaanisha kwamba anatamani kurudi nyumbanio na kuwa Vigogo 6 pamoja na “Mtaalamu” ndio waliosema kuwa amekufa. Aliongeza pia kudai kuwa hakukuwa na jinsi yoyote ya yeye kwenda kinyume na weledi wa fani yake na kuisaliti nchi ambayo anaipenda kutoka moyoni.
Hata hivyo akidokeza kwa mbali kile kinachowezekana kuwa ni sababu ya yeye kutokea hadharani sasa Balali wa twitter anasema “they ripped me off” akimaanisha kwamba hao watu waliomsababishia kukubali kuondoka nchini wamemuingiza mjini. Akiwaita watu hao “wao” anasema wanauwezo wa kuchagua rais, kutafuta fedha na kuzitumia na kutangaza watu kuwa wamekufa. Balali wa twitter amedai kuwa kama atakufa sasa kabla ya lengo lake kutimia bado siri aliyo nayo itawafikia wananchi. Inasadikiwa kuwa wapo watu wachache sana ambao Balali huyo amewafuata na kuwapa sehemu ya taarifa aliyonayo kwa masharti kuwa wakae nazo na wazitoe tu kama atashindwa kufika nyumbani katika muda aliouweka.
Balali huyo amedai kuwa hao waliomsababishia atoweke nchini waliamini kuwa hana madhara yoyote kwao na kuwa wanajua kwamba yuko hai japo hawajui yuko mahali gani. Katika maandishi yake ametuhumu vyombo vya habari kuwa navyo vinatumika kiufisadi kuanzia ngazi ya chini hadi ngazi ya juu kabisa.
Balali huyo amedai kuwa ameandaa mpango wa kina ambao anaufuata wa kuweza kulipua mambo yote ambayo bado yamewakalia wananchi kama kivuli. Ameahidi kufunua gharama halisi ya Minara Miwili ya Benki Kuu, Jinsi Benki Kuu inavyofanya kazi, EPA, Magavana “halisi” wa Benki Kuu, Mkataba wa Rada na mambo mengine kem kem. “Nina mpango wangu kamili ambao ni lazima niufuate na hivyo sina haja ya kuharakishwa kufanya lolote; nitaamua mwenyewe nifanye nini na vipi” amedai Balali huyo wa twitter na hivyo kufanya wahusika mbalimbali kuanza kuwa na matumbo moto hasa kama itathibitka kuwa ni kweli anayezungumza ni Balali aliyewahi kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania.
Akionekana kuwa anatekeleza mpango wake Balali huyo wa twitter alianza kuhesabu siku zilizobakia hadi mpango wake huo kutimizwa. Tarehe 9 Disemba (Siku ya Uhuru) alitangaza kuwa zimebakia siku 308 hadi tukio fulani ambalo amelidhamiria litatokea. Haijulikani kama ni siku ambayo yeye mwenyewe atajitokeza hadharani au siku ambayo nyaraka mbalimbali zinazohusiana nay eye zitawekwa hadharani. Siku 308 tangu Disemba 9, 2011 ni tarehe 12 Oktoba, 2012.
Vyovyote vile ilivyo, wazo kwamba suala la Ballali halikufikia mwisho unaoeleweka linaacha uwezekano mkubwa wa watu wa aina mbalimbali kuweza kujitokeza na kufanya lolote wakijua tundu kubwa lililoachwa wazi na serikali baada ya kuonekana kushindwa kabisa kujua la kufanya juu ya Ballali. Lakini kinachotisha zaidi ni swali lisiloepukika “vipi kama ni kweli huyu ni Ballali”?
No comments:
Post a Comment
Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.