Ahoji wabunge wanakopata mamilioni kufadhili miradi majimboni
Aeleza wasiwasi wake kwa viongozi wa vyama vikubwa vya siasa
Wiki hii Raia Mwema imezungumza na mwanasiasa mkongwe nchini aliyepata kushika nyadhifa mbalimbali nchini Jaji Joseph Warioba kuhusu maoni yake juu ya mwenendo wa nchi katika mwaka uliokwisha wa 2011 na matarajio ya mwaka mpya wa 2012 katika nyanja za uchumi, siasa na maandalizi ya katiba mpya. Haya ndiyo yaliyojitokeza.
Raia Mwema: Mwaka 2011 umepita, sasa tumeingia mwaka 2012. Watu mitaani wanasema huko mambo ni magumu katika uchumi wao, na hakuna dalili kama 2012 itakuwa na nafuu yoyote kulinganisha na 2011. Wewe maoni yako ni nini?
Jaji Warioba: Tumemaliza mwaka 2011 vizuri tu, na hasa sherehe za miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika zimetuwezesha kufanya tathmini ya tulikotoka, tulipo na tunakokwenda. Tumeona mafanikio tuliyopata lakini pia tumeweza kuona matatizo yaliyotufika kama nchi tunapoekelea katika miaka 50 ijayo.Leo tupo mwaka 2012 na tumeanza ile safari ya miaka 50 ijayo. Kwangu mimi tumeianza safari hii katika hali ambayo inanitia wasiwasi kidogo katika maeneo mengi, lakini kama ulivyoniuliza, nianze na eneo la uchumi.
Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita tumejikita mno katika mambo ya siasa. Hatukuweza kutumia muda wa kutosha kutafakari masuala ya uchumi. Miaka mitatu na minne iliyopita, tumezungumzia sana mambo ya siasa, hasa mambo ya viongozi, mambo ya ufisadi. Sawa, ni muhimu tukazungumzia mambo haya, lakini utaona ni kama yanaishia kwenye maneno tu.
Tunavyoendelea hali inakuwa mbaya zaidi. Nafikiri katika mwaka huu tuweke mkazo zaidi katika suala la uchumi. Hali ya uchumi wetu si nzuri. Ukiangalia mazingira ya uchumi wa dunia yalivyobadilika, ni mazingira yanayoweza kutuathiri tukashindwa kutekeleza vyema mipango yetu ya uchumi.
Sasa hivi wakubwa wa dunia wana matatizo. Huko Ulaya matatizo ya nchi zilizomo katika umoja wa Ulaya ni makubwa. Hayo ni matatizo yao, lakini kwa njia moja au nyingine, yatakuja kutuathiri. Kuna pia hali ya wasiwasi katika maeneo muhimu yanayotuhusu.
Ukitazama kaskazini mwa Afrika na Mashariki ya Kati kuna matatizo ambayo kama hayakupatiwa majawabu, yatakuja kutuathiri. Kwa mfano, matatizo ya Iran, ya ugomvi wake na wakubwa. Sasa kuna vitisho vya kususia biashara ya mafuta ya Iran. Yenyewe inasema kama hilo litatokea itafunga mlango bahari wa Hormuz na ukichanganya hayo na matatizo ya Syria, bei za mafuta zitapanda.
Bei za mafuta zikipanda, sisi hatutamudu kuendesha uchumi wetu. Kwa hiyo mazingira hayo ya nje lazima tuyaangalie kwa vile yatatuletea matatizo.
Hayo ni ya nje. Ukiangalia mazingira ya ndani, mwaka 2011 haukuwa mwaka rahisi. Tulikuwa na matatizo mengi tu ya kiuchumi.
Tulikuwa na matatizo ya umeme na upungufu wa kiwango fulani wa chakula uliosababisha bei kupanda. Tulikuwa na matatizo ya thamani ya shilingi yetu kuteremka, na yote haya kwa jumla yakaleta mfumuko wa bei.
Matatizo haya, pamoja na ya mafuta, bado tunayo, ukiacha kwamba bei ya mafuta ni ya juu, utaratibu wa kusimamia bei ya mafuta unatia wasiwasi na hisia kwamba wakati wowote tunaweza kuamka tukakuta vituo havina mafuta.
Na hili si geni, tumeliona, na wala si dogo. Kuna haja ya kuliangalia. Ukiona bei ya mafuta ni kubwa katika dunia, hapa italeta tabu katika kupanga bei na usambazaji wake.
Ni kweli kwamba pamoja na kwamba mvua za vuli zimekuwa nyingi hata zikaathiri shughuli za kilimo katika baadhi ya maeneo, lakini kwa ujumla hali inaonyesha kwamba hapatakuwa na upungufu wa chakula.
Kama upungufu wa chakula utapungua, na kama wasemavyo wataalamu kwamba mfumuko wa bei kwa kiasi kikubwa unasababishwa na upungufu wa chakula, unaweza kusema labda mfumuko utapungua ingawa hakuna hakika sana.
Ukiacha hayo, umeme bado ni tatizo kubwa. Ni kweli sasa hivi tumeweza kupata mitambo ya kufua umeme na mgao ama umekwisha au umepungua, lakini hiyo haimalizi tatizo la umeme. Ukosefu wa umeme unaleta madhara makubwa kwenye shughuli za uchumi.
Sasa tuna umeme, lakini umeme huu ni umeme wa wafanyabiashara waliotoka nje walioweka mitambo yao hapa. Ili wafanye biashara nzuri watataka wapate faida. Kama watapata faida kwa kuiuzia TANESCO umeme, itakuwa ni vigumu kwa TANESCO kuendelea kuuza umeme kwa bei ya sasa.
Tayari bei ya umeme imepanda ikiashiria kuwa sasa tutakabiliana na madhara yatakayofanana na ya wakati ambao hatukuwa na umeme.
Wakati hatuna umeme, uzalishaji ulizorota, gharama za uzalishaji zikapanda, na bei za bidhaa za msingi kwa matumizi ya mwananchi nazo zikapanda. Sasa tunao umeme, lakini bei yake imepanda na gharama za uzalishaji nazo zitapanda, hiyo italeta mfumuko wa bei. Haya ni mambo ambayo tumeyaona na ndivyo hali ilivyo sasa.
Raia Mwema: Lakini mwishoni mwa mwaka jana, akihutubia Taifa, Rais Jakaya Kikwete alisema uchumi utakua, na hata Gavana wa Benki Kuu (BOT), Profesa Beno Ndulu, maoni yake ni kama ya Rais Kikwete?
Jaji Warioba: Ndiyo niliona kwenye hotuba ya Rais na matamshi ya Gavana kwamba uchumi utakua kwa kati ya asilimia sita na asilimia saba. Hizi ni tarakimu tu zinatajwa. Uchumi unakua katika maeneo gani ambayo yatapunguza matatizo ya wananchi? Uchumi unaweza kukua kwenye madini, kwenye utalii, kwenye miundombinu na sijui upande wa viwanda itakuwaje. Lakini yale maeneo yanayogusa wananchi sioni. Ni kwamba unachukua uchumi umekua katika maeneo hayo kisha unagawanya kwa watu waliopo. Katika hali hiyo wanaofaidika na kukua huko ni wachache sana.
Mwaka huu tunaweza tukawa na bahati, kwamba chakula kikapatikana kwa wingi. Kwa hiyo bei ya chakula itapungua. Lakini hivi bei ikipungua wanaofaidika ni wananchi wote?
Kwa mkulima, tunaposema bei ya chakula imepungua, ni kwamba hata yeye anapouza mazao yake anayauza kwa bei ya chini. Anakuwa amepata mavuno mengi lakini kwa kuwa bei ziko chini hatakuwa amejiongezea kipato.
Kukua kwa uchumi lazima kukuonyeshe mabadiliko katika maisha ya watu wa kawaida. Hii ni macro. Tunachukua macro na tunatazama uchumi wetu kwa maana ya fedha. Lakini ukichukua social development index utakuta mwananchi wa kawaida bado atakuwa na hali ngumu.
Umeme umepanda, tuchukue mifano midogo, unakwenda kijijini, tuchukue kijiji chenye umeme, wana mashine ya kusaga pale ya kutumia umeme. Umepandisha bei ya umeme, yule mwenye mashine atapandisha bei ya kusaga. Sasa huyu mkulima ambaye amelina na kupata ziada, mahindi yake anauza kwa bei ya chini, lakini akitaka kusaga, anasaga kwa bei ya juu. Kwangu hii litaleta matatizo makubwa, tulitazame kwa maana ya wananchi wa kawaida. Bado tumo katika hali ambayo ni muhimu tuangalie namna ya kuendesha uchumi wetu.
Tuna mpango wa miaka mitano ulipitishwa mwaka jana. Mimi naona kama wakati mwingine tunaendesha uchumi wetu bila kuangalia msingi mkubwa ni nini. Sawa, tuna mpango wa miaka mitano, huo unaugawanya katika mipango ya mwaka mmoja mmoja. Na mwaka mmoja mmoja huo unapitishwa kama bajeti. Kwa hiyo zile sera za mwaka mmoja zinajikita katika bajeti.
Ninachosema ni kwamba hapa tuna mpango wa miaka mitano, tuna Mkukuta, tuna Millennium Development Goals, tuna Vision 2025 na mingine. Ungetaraji sasa kwamba tunapanga mambo vizuri na tunakuwa na nidhamu ya kutekeleza mipango.
Naona katika utekelezaji wakati mwingine tunakwenda nje kabisa ya tulivyopanga. Kuna lugha siku hizi inazungumzwa, eti kutekeleza ahadi za Rais; nilifikiri mipango yetu ya uchumi inategemea jinsi tulivyopitisha bajeti.
Raia Mwema: Si utekelezaji wa ahadi za Rais tu, kuna pia utekelezaji wa ilani ya chama kilichoshinda uchaguzi wa Oktoba mwaka jana, chama tawala?
Jaji Warioba: Hiyo ilani mimi nachukulia kwamba imetafsiriwa kwenye mpango wa mwaka na bajeti imepita. Kwa hiyo bajeti ikipita, tunachotekeleza ni malengo ya bajeti ile. Sasa wanaposema ahadi za Rais, sijui kama kuna tofauti kati ya mpango wa Serikali, ambao ndio msingi wa kupitisha bajeti, na ahadi za Rais.Nadhani sasa umefika wakati tuondoe kiza. Tunapokuwa na mipango ya maendeleo, tuijue vizuri mipango hiyo ili tuitekeleze. Nchi hii kwa muda mrefu imekubali hoja ya kupanga ni kuchagua. Ukishakuchagua kwa mwaka huo, uwe na nidhamu. Isije katikati hapa ikatoka ahadi nyingine. Kwa sababu, hiyo inawakwaza wasimamizi katika kusimamia.
Ili kulikabili hili la uchumi nadhani mwaka huu tuseme kwamba hali ni hii, hatuwezi kufanya yote. Tutafanya haya, yakija mengine tuwe na nidhamu, tuweze kusema haya hayakuwa kwenye mpango.
Lakini la muhimu zaidi, nadhani tusitoe ahadi kwa wananchi kwamba hali ni nzuri. Ni muhimu kuwaambia wananchi kwamba mazingira ya mwaka 2012 ni magumu na kila mtu ajiandae. Aone anachoweza kufanya. Isije ikatokea hii ya kwamba uchumi unakua, kwa asilimia sita hadi saba, tukakaa tukasema hali ni nzuri. La, hali si nzuri.
Na mimi nafikiri wananchi na viongozi, mawazo yetu yaende kwenye kuimarisha uchumi. Kuna magomvi mengi sana yanazungumziwa, na hasa hili la ufisadi. Sasa ni kama fasheni kuzungumzia kila kitu kuwa ni ufisadi. Pengine ni vizuri kwamba tunakazania kusimamia matumizi. Tuhakikishe kwamba tulichonacho kinatumika vizuri.
Lakini hiyo peke yake haitoshi. Ni lazima tuweke mkazo mkubwa zaidi kwenye uzalishaji. Tusibaki tunagombana tu kwa hiki kidogo tulichonacho. Umeona Kigamboni. Ongezeko la shilingi 100 tu limefanywa ni suala kubwa ajabu. Kama ni posho za Bunge basi linakuwa ni suala kubwa kabisa.
Nasema haya ni matatizo, lakini je, tumezipitia sera husika? Tuchukue, kwa mfano, posho za wabunge. Hivi tatizo ni posho za wabunge tu au tatizo ni sera tulizonazo? Je, ni wabunge tu wanaopata posho ya vikao? Au wapo wengine wanaopata posho ya vikao chini ya sera hiihii?
Mtu anafanya kazi, analipwa mshahara kwa kazi ambayo ameajiriwa. Kama kuna shughuli ambazo zinamtoa pale anapofanyia kazi, anakwenda kwingine ambako inabidi kuwe na matumizi fulani, anastahili kupata posho. Nadhani huo ndio msingi wa posho ya kujikimu. Hilo halina matatizo.
Lakini posho ya kikao, mantiki yake ni nini? Tuchukue mbunge. Hivi mbunge kazi yake ni nini? Chukua Katiba. Katiba inafafanunua kazi za wabunge. Inasema katika kifungu cha 63 kwamba kwa madhumuni ya utekelezaji wa madaraka yake Bunge laweza kumuuliza waziri yeyote, swali lolote kuhusu mambo ya umma katika Jamhuri ya Muungano ambayo yako katika wajibu wake.
Pili, kujadili utekelezaji wa kila wizara wakati wa mkutano wa Bunge wa kila mwaka wa bajeti; tatu, kujadili na kuidhinisha mpango wowote wa muda mrefu au muda mfupi, unaokusudiwa kutekelezwa katika Jamhuri ya Muungano.
Nne, kutunga sheria, pale ambapo utekelezaji unahitaji kuwapo sheria; tano, kujadili na kuridhia mikataba yote inayohusu Jamhuri ya Muungano na ambayo kwa masharti yake inahitaji kuridhiwa.
Hizi ndizo kazi za wabunge. Na kazi hizi zinafanywa Dodoma. Kwamba kazi hizi unazifanya ndani ya Bunge. Kwa hiyo wanalipwa mshahara kwa kufanya kazi hizi wakiwa Dodoma. Wakiwa nje ya Dodoma wana marupurupu mengine. Mbunge akiwa kwenye jimbo ana posho ya jimbo. Ana posho ya mafuta na mambo mengine.
Akija Dodoma kwa kuwa ametoka jimboni, ana posho ya kujikimu. Mimi ningeelewa kama wangesema kwamba ama posho ya jimbo haitoshi, waeleze, au posho ya kujikimu haitoshi kwa kuwa Dodoma imekuwa ghali, ili waongezewe. Lakini kujiongezea posho ya kufanya kazi ya ajira yako, mimi hii siielewi. Lakini hii haiko bungeni tu, iko katika maeneo ya mihimili mingine. Kwa hiyo, hili ni suala la sera. Kulipwa posho ya kikao kwa kazi ambayo unalipwa mshahara msingi wake ni nini? Kwangu mimi hoja si kiwango, bali sera. Msingi wake ni nini?
Nimemsikia mbunge mmoja akisema kwamba posho hii inasaidia wananchi. Kwamba akirudi jimboni wanakuja wengi, wengine wanahitahji fedha za matibabu, za masomo ya watoto wao, na mambo kama hayo.
Ni kweli katika jamii yetu ukiwa katika nafasi, hata kama si mbunge, utakuwa na ndugu ambao wana matatizo. Na popote pale, hata mtu wa chini kabisa, huwa wanatoa msaada. Lakini hukuajiriwa ili utoe msaada. Kwanza utatoa kwa watu wangapi? Unataka kusema jimbo zima ni ombaomba, kwa hiyo ni lazima upewe fedha za kuwapa ombaomba wa jimboni kwako.
Mimi hii siielewi, na hii ya fedha ni kama viongozi wetu wanataka wabadilike wawe wafadhili. Tumezungumza sana mambo haya ya ufisadi. Lakini ukiangalia kwa ndani, hawa waliomo madarakani, wanazungumza kama siasa hivi. Kama kuna hatua zimechukuliwa utaona zaidi ni matendo ya serikali iliyopita. Ya sasa huoni kama hatua zimechukuliwa.
Kwa nini nasema hivi? Kuna mambo yanatokea unajiuliza maswali mengi. Mbunge anatoa shilingi milioni 50 au milioni 70 kusaidia jimbo lake. Haulizwi zimetoka wapi hizo. Hawa wamepata wapi fedha zote hizo? Naona kama imefika mahali kama awamu hizi za utawala zitakuwa za kusutana. Iliyopo itasuta iliyopita, nayo ikitoka inasutwa na itakayokuja.
Mbele ya safari watu watahoji, hawa walikuwa wanapata wapi mamilioni haya ya fedha? Ama wamekuwa ombaomba au wanatumia fedha kupata nafasi zao. Maoni yangu ni kwamba tuangalie sera zinasemaje kuliko kuhangaika na matukio.
Niseme tu kwa jumla kwamba mwaka huu hali ya uchumi itakuwa mbaya. Wananchi wajiandae. Wajue hivyo, tuonyeshe maeneo, tuwe na mipango ambayo itataja kila mtu wajibu wake nini.
Lakini pia tusifurahi sana kwamba linapotea jambo basi tunakuwa wa kukosoa tu. Wakati tunakosoa tuwe pia tunasema nini kifanyike. Uchumi mbaya utatugusa wote. Viongozi wasipambepambe hali hii kuonyesha kana kwamba hali ni nzuri na wananchi wasitarajie kwamba Serikali itafanya kila kitu.
Raia Mwema: Idadi kubwa ya Watanzania ni wakulima, ukitaka kuwaondoa hawa katika uchumi duni ni kushughulikia kilimo chao, unaziona jitihada za kweli za kuinua uchumi wa wakulima hawa?
Jaji Warioba: Kama tunataka kuondoa umasikini katika nchi hii kilimo ndiyo msingi. Katika kilimo ndiko mahali pa kuweka mkazo mkubwa. Na huko nyuma, kwa sera na kwa matamko wakati wote, tulisema kilimo ndio uti wa mgongo. Hatukweza kufanikiwa kuwa na sera ambayo ingeinua kilimo cha mkulima mdogo mdogo. Tulijaribu wakati fulani na matunda yake yakaonekana. Tuna Big Four, sijui kama watu wanakumbuka Big Four: Iringa, Mbeya, Rukwa na Ruvuma ilikujaje.
Ni kwa kuinua kilimo kule, na kwa kuwa tuliona huko ndiko kwenye uwezekano wa kuwa na ghala la chakula, hatua makusudi zilichukuliwa na zikainua kilimo.
Nini hasa kilichofanywa? Tulisema tuhakikishe mkulima anapata mahitaji yake kwa bei anayoweza. Kukawa na mpango mkulima apate zana na pembejeo kwa bei anayoiweza. Na anapopata ziada kwa mazao yake auze kwa bei nzuri. Wakati ule Serikali ilikuwa inatoa ruzuku.
Nakumbuka wakati fulani mahindi Ruvuma yalikuwa yananunuliwa kwa shilingi tatu, sembe mjini Dar es Salaam ilikuwa inauzwa kwa shilingi mbili na senti hamsini. Ni kwamba ruzuku ilikuwa imetolewa ili bei ya mkulima iwe nzuri.
Sasa wakati ule ulikuwa ni wa uchumi kusimamiwa na dola, sasa tumebadili sera, uchumi ni wa soko huria na hilo lina matatizo yake kwa mkulima mdogo mdogo.
Gharama za uzalishaji ni kubwa, anapouza mazao yake bei inakuwa chini na hivyo hawezi kufidia gharama zake za kuzalisha. Serikali imejitahidi, kuna vocha za pembejeo. Lakini hii ni sehemu ndogo sana na mara kadhaa inaleta matatizo ya rushwa.
Ni ngumu, na imekuwa ngumu wakati wote. Tusikate tamaa, lazima tutie mkazo kwenye kilimo. Ifike mahali mkulima apate zana na pembejeo kwa gharama anayoiweza, na anapouza mazao yake auze kwa bei inayorudisha gharama zake. Ikafanyika hiyo akapata faida ndipo atakapoboresha maisha yake.
Raia Mwema: Mwaka jana ulikwisha na mwaka huu umeanza tukishuhudia ugomvi ndani ya vyama vya siasa, vikubwa kwa vidogo. Kama si Chama cha Mapinduzi (CCM) basi itakuwa ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tanzania Labour Party (TLP), NCCR Mageuzi au Chama cha Wananchi (CUF). Ni nini hiki kinachoendelea ndani ya siasa zetu?
Jaji Warioba: Tunayo matatizo ya kiuchumi, lakini hayo yanakuwa makubwa zaidi kutokana na matatizo ya uongozi wa kisiasa. Vyama vyetu, tangu mwaka 1992, wakati ule kulikuwa na matumaini, na hata tulipokwenda kwenye uchaguzi wa mwaka 1995 tulikuwa tunaelekea katika upinzani wa kweli.Wakati ule Rais alipata asilimia kama 60 hivi ya kura zote huku upinzani ukipata kama asilimia 40 hivi. Hiyo ilikuwa inatia matumaini. Lakini baada ya hapo kukawa na migogoro mingi katika vyama hivi. Naukumbuka wa NCCR Mageuzi. Kufika mwaka 2000, wakati wa uchaguzi mwingine, Rais alishinda kwa kura kama asilimia 80 hivi.
Kwa hiyo umetoka kwenye ushindi wa asilimia 60 umepanda hadi asilimia 80 na upinzani umeshuka kutoka asilimia 40 kuja kwenye asilimia 20 hivi. Na sasa matatizo haya yanaendelea.
Mwaka juzi, lakini kabla ya hapo, ni kama tulikuwa tunarejea kwenye mfumo wa chama kimoja. Mwaka 2010 ni kama upinzani ulianza kupanda tena na kujenga matumaini kwamba tunaweza kujenga mfumo wa kweli wa vyama vingi.
Mwaka 2005, Rais alipata asilimia 80 hivi. Mwaka 2010 upinzani ulipanda kwa kiwango cha kura kama za mwaka 1995. Kwa hiyo ukichukua ya mwaka 2010 ni kama tunajenga mfumo mzuri zaidi wa vyama vingi. Na kwa kweli ni kama upinzani umepanua zaidi uwanja wa mawazo na sera, kwa maana hiyo unaona kama hatupaswi kufikiria kurudi kwenye chama kimoja. Tuimarishe mfumo wa vyama vingi.
Lakini kuimarisha mfumo wa vyama vingi maana yake ni kuimarisha vyama vya siasa. Sasa dalili zinaonyesha kwamba vyama hivi vinasambaratika. Tuna vyama 18, vyenye wabunge ni sita. Vingine vilivyobaki ni kama wananchi hawavijui. Wakati mwingine vimekuwa kama ni vyama mtu, ukitaja chama unataja mtu. Lakini hata hivi ambavyo vinaonyesha nguvu kidogo navyo vinasambaratika.
Na tatizo lake ni nini? Si tofauti za itikadi, si tofauti za sera. Ni madaraka. Kwamba wakubwa wakihitilafiana, jibu ni kufukuzana. Tumeliona hilo kwenye TLP, tumeliona hilo kwenye NCCR, si mara ya kwanza, tanaliona pia kwenye CUF.
Baadhi ya vyama ni kwamba vinarudi nyuma. Kwanza havikuwa na nguvu sana, sasa migawanyiko hii inavifanya vidhoofike zaidi. Hata vikubwa, pamoja na CHADEMA. Pale kuna magomvi, madiwani wamekuwa na msimamo uliotofautiana na wakubwa, wamewatimua. Adhabu ni kutimua.
Lakini matokeo yake ni nini, na haya si matokeo ambayo hayahusu wanachama tu, bali pia wananchi. Mmekwenda kwenye uchaguzi, mmeweka mgombea, mkaomba wananchi huyo ndiye awe mwakilishi wenu. Akiishakuupata, anakuwa mwakilishi wa chama. Na chama kinapofikiria kuchukua hatua, hakifikirii kuwa ni mwakilishi wa wananchi.
Asili ya yote haya ni kugombea madaraka. Na utaona hadi kufika 2015 kama mwenendo ni huu kutakuwa na mgawanyiko zaidi. Maana mtu akisema anataka uongozi mnamfukuza, labda mfike mahali ndani ya chama mzuie watu kujitokeza. Iwe kama ilivyokuwa wakati wa chama kimoja.
Nina wasiwasi mkubwa na vyama hivi vikubwa. Kwa mfano, CUF imeunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar. Hilo ni jambo ambalo ni zuri. Limeleta amani na utulivu Zanzibar. Lakini jambo zuri wakati mwingine lina matatizo yake. CUF chama ambacho kabla ya uchaguzi wa 2010 kilikuwa na nguvu, sasa hakijitokezi kama chama cha upinzani.
Kwa Zanzibar CUF ni chama tawala. Kwa hiyo kule huwezi kukuta siasa hizi za kawaida za vyama wakati huu. Kwamba kuna chama tawala na chama cha upinzani. Lakini hiki ni chama cha nchi nzima. Zanzibar kuna CCM na CUF zinashirikiana, lakini Bara kuna CCM na CUF zinapingana. Hali hii ni ngumu.
Ni kawaida, kwamba katika mfumo huu ambao CUF ni mwenza wa CCM Zanzibar, nguvu zake zitapungua. Kwa hiyo CUF ina tatizo hilo. Isipokuwa makini itajivuruga.
Raia Mwema: Lakini mbona mazingira ya Zanzibar ni kama ya Zimbabwe na huko Morgan Tsvangirai bado anamtikisa vilivyo mzee Robert Mugabe?
Jaji Warioba: Zimbabwe ni mseto pia. Lakini huko utaona kwamba wanasuguana bado hata ndani ya serikali. Wanasema wako pamoja katika kuendesha nchi lakini unauona waziwazi upinzani hata ndani ya serikali. Zanzibar wamekubaliana na huwezi kupinga kwamba makubaliano hayo yameleta utulivu na amani. Lakini tukumbuke Zanzibar ndiyo katika eneo hili imekuwa yenye demokrasia hasa, hata kabla ya uhuru.
Zanzibar wana historia nzuri ya upinzani na wamezoea. Kwa hiyo mbele ya safari kutakuwa na watu watakaoona kwamba upinzani haupo na wao wanahitaji kuwa wapinzani, watatoka. Wakifanya hivyo CUF itadhoofika.
CHADEMA nako hali wanayokwenda nayo si nzuri, wanayo matatizo. Wamefukuza watu na jambo hilo si dogo. Wasipoangalia hawatakuwa tofauti na vyama vingine hivi.
CCM ina matatizo ya kipekee, inawezekana ni makubwa zaidi kuliko vyama vingine. Kwanza inaonekana ina tatizo la bango hili la ufisadi. Inaonekana kama ndiko kuna ufisadi. Kwa hiyo inajitahidi kulindoa bango hilo.
Jitihada za kujivua bango zimeleta mgawanyiko zaidi ndani, tangu chini hadi juu. Wapo wana CCM wanaojiona kuwa wao ni wapambanaji na wengine ambao siyo. Lakini tatizo kubwa ni kwamba wameshindwa kufanya uamuzi katika wakati muafaka.
Imechukua muda mrefu. Na inapochukua muda mrefu uhasama na mgawanyiko unakua zaidi. Wangechukua uamuzi likaisha, chama kingejijenga. Wamewekeana muda ukapita, wakaweka muda mwingine ukapita, hapajatokea lolote.
Hatari ninayoiona, mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi wa CCM. Tatizo hili lisipoamliwa au uamuzi usipotolewa kabla ya uchaguzi, uchaguzi huu utakuwa wa mgawanyiko. CCM inaweza kusambaratika. Kila kundi litataka watu wake ndio wachaguliwe. Huku atapita wa kundi hili na kule atapita wa kundi jingine. Mgawanyiko wa ndani ya CCM utakuwa wa kitaasisi. Ikifika 2015 watakuwa wamegawanyika zaidi.
Matatizo ya CCM sasa hivi yanahatarisha uhai wa CCM yenyewe. Lazima ifike mahali CCM itoe uamuzi. Vinginevyo chama kitabomoka. Maamuzi yafanywe mapema kabla ya uchaguzi.
Lakini matatizo haya ya CCM si ya CCM peke yake. Yatasambaa. Sera zilikuwa zinaandaliwa na chama kupitia Halmashauri Kuu na Kamati Kuu. Utekelezaji ulikuwa unafanywa kwa kiwango kikubwa na jumuiya zake. Hasa jumuiya ya vijana na ya kina mama. Jumuiya ya vijana nayo imesambaratika, ina matatizo kama ambayo yako kwenye chama.
Lakini si hivyo tu. Jumuiya ya vijana inaonekana kama inapingana na chama chenyewe. Sasa jumuiya ya vijana badala ya kuwa mtekelezaji inaonekana kama mshindani. Kwa upande mwingine, hatusikii mara nyingi kuhusu UWT. Ni kama haipo. Unaweza usijue UWT iko wapi.
Kwa hiyo sasa tuna jumuiya ambazo kwa upande mmoja ni sehemu ya chama na kwa upande mwingine zinapingana na chama. Nazo ni sehemu ya makundi ndani ya chama.
Ukitafakari mgawanyiko huu si wa itikadi wala hoja. Ni wa maslahi. Mnakuwa na matatizo tangu 2010, lakini wakati wote wa mazungumzo ajenda ni urais wa 2015. Lakini hapa mna ilani ambayo ndiyo mliyotumia kuomba ridhaa ya wananchi mkaahidi kwamba kwa miaka mitano kazi yenu ni kutekeleza ilani hiyo. Sasa hatusikii utekelezaji wa ilani bali mazungumzo ya madaraka na urais wa mwaka 2015.
CCM ni chama kikongwe na kikubwa. Ni chama ambacho kimeongoza serikali kwa muda mrefu. Hali ya uchumi siyo nzuri na maisha ni magumu kwa wananchi wengi, hasa vijana ambao hawana ajira. Katika hali hiyo kuna watu wanataka mabadiliko bila hata kufikiria sera. Kuna watu wanataka regime change. CCM isifanye makosa ya kudharau kundi hili kwani kuna dalili ni kundi linalozidi kukua.
Chanzo: Raiamwema
No comments:
Post a Comment
Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.