TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Chama Cha Mapinduzi kinatarajiwa kuadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa kwake mwanzoni mwa mwezi Februari na kufikia kilele chake tarehe 5 Februari, 2012.
Maadhimisho hayo ni kumbukumbu muhimu kwa Chama Cha Mapinduzi kufikisha miaka 35 ya uhai wake tangu vyama vya TANU na ASP vilipovunjwa na kuundwa Chama kipya chenye nguvu tarehe 5 Februari, 1977.
Sherehe hizo huadhimishwa kwa Chama na Jumuiya zake kufanya shughuli mbali mbali za kisiasa na kijamii. Aidha, Kitaifa Chama huteua Mkoa mwenyeji wa sherehe hizi ambazo huambatana na Matembezi ya Mshikamano.
SHEREHE ZA MWAKA 2012:
Tofauti na sherehe za miaka mingine, sherehe za mwaka huu zitabeba malengo yafuatayo:-
(1) Kuhamasisha wanachama wetu waadilifu na waaminifu kujitokeza kugombea kuanzia ngazi ya Shina mpaka Taifa.
(2) Kupiga vita wagombea wote wanaotoa na kupokea rushwa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Chama 2012.
(3) Kutoa elimu kuhusu mabadiliko ya Katiba ya nchi yanayokusudiwa kufanyika hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na kuhudhuria mikutano ya kutoa maoni bila kukosa wakiwa na msimamo wa kuilinda nchi yetu, amani yake na kupatikana kwa Katiba bora itakayokuwa na manufaa kwa watu wote.
KAULI MBIU:
Kwa kuwa mwaka huu ni wa Uchaguzi Mkuu wa Chama inapendekezwa Chama kiwe na Kauli mbiu mahsusi itakayotumika katika sherehe hizo. Kauli mbiu inayopendekezwa ni:-
“CCM Imara na Madhubuti inaanza na mimi; naimarisha Chama Changu kwa kuchagua viongozi bora na waadilifu.”
UZINDUZI WA SHEREHE:
Sherehe za mwaka huu zitazinduliwa kila Mkoa tarehe 30/01/2012, na zitafuatiwa na wiki ya shughuli za Jumuiya, ambazo kila Jumuiya itapanga ratiba ya mikutano ya ndani pamoja na shughuli za kijamii kama vile kupanda miti, kutembelea wagonjwa, kufanya usafi na kwa maeneo mengine ambayo zipo shughuli za ujenzi wa vyumba vya madarasa pamoja na nyumba za walimu n.k. katika shule za kata, Jumuiya zitashiriki kadri watakavyoona inafaa kulingana na shughuli zitakazokuwepo.
Aidha wajumbe wa kamati ya Siasa na Halmashauri kuu ya Mikoa waitumie wiki hiyo kufanya ziara katika matawi kuimarisha uhai wa Chama.
USHIRIKI WA VIONGOZI WAKUU KATIKA SHEREHE
Mwenyekiti wa Taifa wa CCM Dr. Jakaya Mrisho Kikwete atakuwa mgeni rasmi katika sherehe za kilele na matembezi ya mshikamano zitakazo fanyika kitaifa Jiji la Mwanza.
Aidha Makamu wa Mwenyekiti wa CCM Zanzibar naye atashiriki katika vikao vya ndani vya wanachama pamoja na mkutano ya hadhara katika Mkoa utakaoandaliwa kuhitimisha sherehe hizo za kilele kwa upande wa Zanzibar.
MATEMBEZI YA MSHIKAMANO NA SHEREHE ZA KILELE
Matembezi ya Mshikamano ya mwaka huu yatafanyika kila Mkoa na Walezi wa Mikoa wataongoza matembezi hayo. Aidha, katika Matembezi hayo Mwenyekiti wa CCM wa Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dr. Jakaya Mrisho Kikwete ndiye atakayedhaminiwa kwa Mikoa yote. Matembezi hayo yataanza asubuhi saa moja na baada ya hapo mikutano ya hadhara ya kuhitimisha sherehe hizo itafanyika.
Kila Tawi litafanya kilele chake tarehe 04/02/2012
Source:Sixtus Mapunda,
Assistant Secretary,
Department of Political Affairs & International Relations,
Chama Cha Mapinduzi (CCM),
P. O. Box 9151,
Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment
Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.