Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Saturday, January 21, 2012

Wabunge mtegoni

Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Dk. Edward Hoseah

TAKUKURU yawavaa kuhusu posho
Ripoti yafikishwa mezani Ikulu
WAKATI Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, akipendekeza kuundwa kwa kamati maalumu ya kitaifa kuratibu viwango na malipo ya posho kwa viongozi na watumishi wa umma, Raia Mwema limeelezwa kuwa, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imewasilisha ripoti ya uchunguzi wake kuhusu utata na uhalali wa malipo ya viwango vipya vya posho kwa wabunge.
Ingawa haijawekwa bayana kama TAKUKURU walifanya uchunguzi huo kwa maelekezo ya Ikulu, lakini taarifa za uhakika zinaeleza kuwa hatua hiyo ilichukuliwa baada ya Spika Anne Makinda, kusisitiza posho mpya zilikwishakulipwa kwa wabunge kinyume cha kauli ya Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila, aliyekuwa akiweka bayana kuwa hakuna malipo yaliyokwishakufanyika.
Hata hivyo, wakati mvutano kati ya viongozi hao ukiendelea, Raia Mwema limefanya utafiti wake na kuchapisha habari katika moja ya matoleo yake ikieleza kuwa Rais Jakaya Kikwete, aligoma kuidhinisha viwango hivyo vya posho mpya na hivyo, hakuna kilichoongezeka kwa mujibu wa taratibu, kanuni na sheria husika.
Vyanzo vya uhakika vya gazeti hili serikalini vinaeleza kuwa tayari TAKUKURU imekwishakukamilisha kuchunguza kama kuna malipo yoyote yaliyokwishakufanyika kwa wabunge, ikiwahoji baadhi yao.
“TAKUKURU wamechunguza uhalali wa ongezeko la posho za wabunge na tayari wamemaliza na kuwasilisha taarifa kwa bwana mkubwa (Rais).
“Kilichosababisha wachunguze ongezeko hilo la posho kwa wabunge ni kauli mbili tofauti za viongozi wa Bunge, Katibu alisema suala hilo (posho mpya) bado linafanyiwa kazi lakini Spika akasema lilishapitishwa na wabunge wanalipwa,” kilisema chanzo chetu cha serikalini.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Dk. Edward Hoseah, hakuwa tayari kufafanua kuhusu suala hilo akiliambia gazeti hili ya kuwa asingeweza kulizungumzia kwa vile hakuwa ofisini.
Hata alipotafutwa Mkurugenzi wa Uchunguzi wa taasisi hiyo, Alex Mfungo, naye hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo akidai si msemaji wa taasisi hiyo.
Lakini gazeti hili limedokezwa kuwa ripoti ya uchunguzi huo wa TAKUKURU imeeleza kwa kina udhaifu wa kiutendaji katika Bunge pamoja na kuainisha mapendekezo juu ya hatua zaidi za kuchukua.
Katibu wa Bunge, Dk. Kashilillah hakuwa tayari kuthibitisha taarifa hizo za kiuchunguzi dhidi ya Bunge kutokana na kile alichoeleza kuwa ni kubanwa na shughuli nyingine, ikiwamo msiba wa Mbunge wa Viti Maalumu (CHADEMA), Regia Mtema.
Hata hivyo chanzo kingine cha habari katika ofisi ya Bunge kimelieleza gazeti hili; “Katibu wa Bunge amekasirishwa sana na kitendo cha bosi wake kuhakikishia umma kuwa ongezeko la posho hizo lilifuata taratibu zote, kama ingekuwa hivyo yeye Katibu ndiye angekuwa wa kwanza kujua, ila hapa kuna tatizo.”
Inaelezwa kuwa ni mkanganyiko huo wa kauli kati ya viongozi hao wakuu wa Bunge ndiyo umeifanya Serikali kuwa katika wakati mgumu zaidi kueleweka kwa wananchi na taarifa zaidi zikieleza kwamba, tayari kuna njia ya kidiplomasia imeandaliwa kumaliza suala hilo katika Bunge lijalo mwezi huu.
Taarifa hizo za kutafuta njia muafaka la kupata mwarobaini wa tatizo hilo la nyongeza ya posho zinawekwa bayana wakati tayari Naibu Spika Ndugai, akipendekeza iundwe tume maalumu.
Akizungumza katika moja ya vipindi vinavyorushwa na Televisheni ya ITV, Jumatatu wiki hii, Ndugai alisema tatizo la msingi ni uwezo mdogo kiuchumi na si kiwango cha posho wanacholipwa wabunge ambacho hata hivyo, ni kidogo mno ikilinganishwa na baadhi ya maofisa wengine serikalini.
Kwa mujibu wa Ndugai, viwango vya posho kwa wabunge ni vidogo ikilinganishwa na kwa mfano, maofisa waandamizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa (TANAPA).
“Kama mapendekezo ya kuundwa kwa tume maalumu yatakubaliwa tutakuwa tumepata ufumbuzi wa tatizo hili. Tume hii itakuwa na kazi ya kuratibu na kupanga nani alipwe posho kiasi gani, kuanzia jeshini, Mahakama na kwingine kuliko utaratibu wa sasa ambao baadhi hujipangia wenyewe,” alisema Ndugai.
Joto la viwango vipya posho liliibuliwa mara baada ya kukamilika kwa mkutano wa Bunge wa Novemba, mwaka jana.
Iliripotiwa kuwa kuna ongezeko la posho ya kukaa kitako kutoka Sh. 70,000 kwa mbunge kwa siku hadi Sh. 200,000 na Spika alithibitisha ongezeko hilo na kwamba tayari wahusika walianza kulipwa.
Hata hivyo, uthibitisho huo wa Spika ulitanguliwa na kauli ya Katibu wa Bunge, Dk. Kashilillah, aliyesema hakuna mbunge aliyelipwa posho mpya.
Baadaye gazeti hili liliripoti kuwapo kwa mapendekezo ya ongezeko la posho kwa viwango na kwamba mapendekezo hayo yamekwama mezani kwa Rais Jakaya Kikwete ambaye kwa mujibu wa sheria anapaswa kutia saini kuidhinisha matumizi hayo mapya ambayo yangefanya bajeti ya wabunge kufikia Sh bilioni 28 kwa mwaka.
Uchunguzi zaidi wa Raia Mwema umebaini kuwa baadhi ya maofisa katika mihimili mingine ukiondoa Bunge wamekuwa wakilipwa posho kati ya Sh. 300,000 hadi 600,000 kwa siku. Baadhi ya taasisi hizo ni Mahakama, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), baadhi ya mashirika ya umma katika Sekta ya Utalii na hata Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Mwezi uliopita Rais Jakaya Kikwete, aliwaonya maofisa wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), kuacha kulipana posho kubwa kwenda Ulaya kwa maelezo ya kutangaza sekta ya utalii, kinyume cha hali halisi.

Chanzo: Raiamwema

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.