Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Tuesday, January 24, 2012

LIBYA DAMU UPYA









Luqman maloto na vyanzo  vya kimataifa
YALIYONENWA kuhusu damu kuendelea kumwagika Libya yameanza kudhihirika kwa vitendo, amani ya nchi hiyo ni msamiati mgumu kutokana na machafuko yaliyoibuka wiki iliyopita ambayo almanusra yasababishe vifo vya viongozi wakuu wapya wa nchi hiyo.
Mwenyekiti wa Baraza la Mpito la Taifa (NTC), Mustafa Abdul Jalil ambaye ni kiongozi mkuu wa nchi hiyo kwa sasa na makamu wake, Abdul Hafiz Ghoga, walinusurika kuuawa Jumamosi iliyopita.
Jalil, aliponea chupuchupu baada ya walinzi wake kumtoroshea mlango wa nyuma, kuwakwepa waandamanaji waliovamia Makao Makuu ya NTC, Benghazi na kuvunja ofisi hizo za serikali ya muda.
Baada ya Jalil kuokolewa na walinzi wake, waandamanaji hao wakiwa na hasira, walilivamia gari lake na kulivunjavunja kabla ya kuliacha nyang’anyang’a.
Kwa upande wa Ghoga, alizingirwa na wanafunzi wa vyuo vikuu mjini Benghazi lakini aliokolewa kabla hawajamdhuru.
Jalil ndiye aliyekuwa na wakati mgumu zaidi, kwani alitupiwa vitu mbalimbali ambavyo hata hivyo, havikumjeruhi.

MADAI YA WAANDAMANAJI
Waandamanaji nchini Libya, wamegawanyika kwenye makundi matatu na kila upande una sababu zake ambazo unataka zisikilizwe na kufanyiwa kazi.
Makundi yote, yanaungana kwenye pointi moja kuwa ni lazima uongozi wa NTC ung’oke kwa sababu umeshindwa kutekeleza mahitaji yao.

KUNDI LA KWANZA
Ni wananchi wanaotaka uwazi kuhusu rasilimali za Libya. Wanadai kuwa aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi, aliacha fedha na mali nyingi kwa ajili ya Walibya lakini zinatumika bila mpangilio wala maelezo.
Wanadai kuwa maisha yamekuwa magumu, wakati enzi za Gaddafi kulikuwa na hali nzuri. Vilevile wanailaumu NTC kwa kuunda sheria ya uchaguzi bila kuwashirikisha wananchi.

KUNDI LA PILI
Ni wapiganaji walioshiriki kumng’oa Gaddafi. Wanadai kuwa NTC imewatenga katika muundo wa serikali ya mpito na hata fedha walizopewa kama mgawo, hazitoshelezi mahitaji yao na hazilingani na nguvu waliyotumia.
Wapiganaji hao ambao wengi wao walivamia ofisi za NTC wakiwa na majeraha yaliyotokana na vita, wanaishutumu NTC kwa kushirikisha baadhi ya watumishi wa umma waliokuwepo tangu enzi za Gaddafi.

KUNDI LA TATU
Ni wanaharakati wa Islamic Brotherhood ambao wanadai Libya ni nchi ya Kiislam, kwa hiyo ni lazima iongozwe kwa sharia, hivyo wanataka NTC ing’oke kupisha muundo wa serikali utakaofuata misingi ya Uislam.

NI LAANA YA GADDAFI?
Kabla ya Benghazi, wananchi wa Jiji la Sirte walikuwa wa kwanza kulalamikia kuwa maisha ya Libya yamekuwa mabovu tangu kupinduliwa na hatimaye kuuawa kwa Gaddafi.
Wananchi hao walilalamika kuwa Gaddafi aliwasaidia kujenga nyumba lakini NTC walibomoa, kadhalika alilinda maisha yao ila baraza hilo la mpito liliua raia wakati wa vita wakisaidiwa na Jeshi la Kujihami la Nchi za Magharibi (Nato).

Wananchi wa Sirte walitoa msimamo kuwa Libya haitakalika mpaka damu ya Gaddafi ifidiwe, pia kaburi alilozikwa liwekwe wazi ili kila raia wa Libya ajue mahali lilipo.
Leo ni siku ya 96 tangu Gaddafi alipokamatwa na kuuawa Oktoba 20, 2011. Kabla hajafa aliwauliza wapiganaji wa NTC: “Je, mnaujua ukweli katika uongo?”
Kulikuwa na mpiganaji aliyekuwa mstari wa mbele kumsulubu, akamuuliza: “Kama wewe, nimekukosea nini?”

Awali, ilionywa na wachambuzi wa siasa za kimataifa kuwa kupinduliwa kwa Gaddafi haiwezi kuwa suluhu ya amani Libya, badala yake inaweza kuchochea machafuko ya muda mrefu.
Inaelezwa kuwa kumekuwa na machafuko ya chini kwa chini ambayo yamekuwa yakiwaachia majeraha wananchi, wakiwemo wanawake na watoto.
PICHA ZOTE NA AFP


Chanzo: Global Publishers

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.