Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Tuesday, January 24, 2012

WAFANYABIASHARA YA POMBE WAPIGWA RISASI ZANZIBAR


Mfanyabiashara Alvind Asawla aliyepigwa risasi katika paji la uso ikatokea shingoni na kumwagiwa tindikali Zanzibar, akiwa na mkewe Bimal katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jumatano iliyopita. (Na Yusufu Badi).

WAFANYABIASHARA wawili mtu na mkewe, wamepigwa risasi na kumwagiwa tindikali huko Zanzibar kwa kuuza pombe.

Katika uvamizi huo uliofanyika Jumatano iliyopita mwanamke Bimal Alvind (36) alinusurika kupoteza ujauzito wake wa miezi minne baada ya kupigwa risasi ya tumbo na kumwagiwa tindikali.

Risasi hiyo ilitolewa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili bila kuathiri ujauzito huo lakini tindikali hiyo ilimjeruhi mwilini kuanzia usoni, kifuani kwenye matiti, mikono yote miwili na tumboni.

Mumewe, Alvind Asawla (42) alipigwa risasi kichwani kwenye paji la uso katikati ya macho iliyotokea nyuma chini ya shingo na sasa amepooza upande mmoja.

Akizungumza na gazeti hili nyumbani kwa ndugu yake Upanga wiki hii, Asawla alisema walivamiwa Jumatano iliyopita saa 10:30 jioni katika Mtaa wa Hurumzi Mji Mkongwe.
Alisema wakati wakivamiwa, yeye na mkewe aliyeishi naye kwa miaka 17 sasa na kujaliwa watoto wawili; Priyanka (14) na Nidh (12), walikuwa wakitoka katika biashara yao wakirudi nyumbani eneo la Kiponda.

Alisema ghafla watu wawili walimvamia mkewe na kummwagia tindikali na yeye alipokuwa akijaribu kumsaidia, watu hao walimmwagia tindikali usoni.

Kwa mujibu wa Asawla, wakati wakitaharuki kwa hali hiyo, ghafla alitokea mtu mwingine na kumpiga risasi katika paji la uso akadondoka chini huku damu zikimtoka.

Alisema alijaribu kujikongoja kwa nia ya kuendelea kumsaidia mkewe lakini mtu huyo wa tatu alimpiga risasi ya pili mgongoni na mkewe akapigwa risasi ya tumbo.

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.