Na Faki Mjaka Maelezo Zanzibar 19/01/2012
Ripoti ya Tume ya kuchunguza ajali ya kuzama kwa Meli ya Mv. Spice Islanders 1
imependekeza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Mustafa Aboud Jumbe pamoja
na wahusika wengine wachukuliwe hatua za kisheria na kinidhamu kutokana na uzembe
waliofanya na kusababisha kuzama kwa Meli hiyo
Akitoa mapendekezo ya Ripoti hiyo leo katika Ukumbi wa Wizara ya Habari Katibu wa
Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Katibu Mkuu Kiongozi Abdulhamid Yahya Mzee
amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeyakubali mapendekezo ya ripoti hiyo na
kusema itaiachia Mahaka na Jeshi la Polisi kutimiza wajibu wao
Dk.Abdulhamid amesema miongoni mwa watu ambao walibainika na makosa katika ajali
hiyo ni pamoja na Mkurugenzi wa Mamalaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar Haji Vuai
Ussi,Mkuu wa kituo cha usimamizi wa usalama wa vyombo vya baharini wa Shirika
la Bandari,Usawa Khamis Said na Kaimu Mdhibiti wa Bandari ya Malindi Sarboko
Makarani Sarboko.
Wengine ni pamoja na Wanahisa wa Kampuni inayomiliki meli hiyo Jaku Hashim Ayub
ambaye ni Mwakilishi na Mbuge wa Jimbo la Muyuni,Salim Said Mohammed, Makame
Hasnuu Makame na Yussuf Suleiman Issa.
Dk.Abdulhamid amesema wahusika wote waliotajwa katika ripoti hiyo ikiwa ni pamoja
na Captain wa Meli hiyo Said Abdallah Kinyanyite na wasaidizi wake,Afisa usafirishaji
wa Shirika la Bandari Hassan Mussa Mwinyi na Mkaguzi wa Meli wa Mamlaka ya
Usafisiri wa Baharini Juma Seif Juma watachukuliwa hatua za kisheria kulingana na
makosa yao
Mrajis wa meli Abdallah Mohammed Abdallah, Afisa Usalama wa Mamlaka ya Usafiri
wa Baharini Simai Nyange Simai, na wasimamizi wa watatu wa uingiaji wa abiria katika
meli hiyo Yussuf Suleiman Issa,Shaib Said Mohammed na Juma Abdallah Hussein nao
wachukuliwe hatua za kisheria na kinidhamu.
Wengine ni Afisa Mkuu wa Mv.Spice Abdalla Mohammed Ali,Mhandisi Mkuu wa
Meli hiyo Khamis Ahmada Hilika, Mabaharia wote wa Meli hiyo pamoja na Askari wa
Bandarini waliokuwepo zamu katika kupanga abiria siku ya tukio ambao ni Sajent Jumbe
Muhaji na Koplo Juma Abdulla.
Akizungumzia juu ya fidia kwa wahanga wa ajali hiyo Dk.Abdulhamid amesema jukumu
la kuwalipa wahanga hao liko mikononi mwa wamiliki wa meli hiyo kwa mujibu wa
sheria na kwamba vigezo vya kulipwa wahanga vitafuata utaratibu maalum uliowekwa
ambapo kwa waliofariki watalipwa si chini ya Sh Milioni Kumi
Kwa waliopata ulemavu watalipwa asilimia 75% ya Fedha watakazolipwa waliofariki
dunia ambapo waliokuwemo katika meli hiyo bila kupata ulemavu watapata asilimia 50%
ya kiwango hicho.
Kuhusu fedha za michango ya maafa ambazo zimetolewa na taasisi mbalimbali Dk.
Abdulhamid amesema fedha hizo zitagawiwa kwa wahusika chini ya utaratibu maalum
utakaowekwa na Mfuko wa Kamati ya maafa uliopo chini ya Afisi ya Makamu wa Pili
wa Rais
Aidha Dk.Abdulhamid alisema ripoti hiyo itawekwa wazi na kupatikana katika mitandao
na Maktaba kuu ili wananchi waweze kuisoma.
Ripoti ya Tume hiyo iliundwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein kufuatia kuzama kwa Meli ya Mv. Spice Islanders
1 tarehe 9/09/2011 katika Mkondo wa Nungwi kuelekea Pemba ambapo inasadikiwa
ilikuwa na abiria 2470 na tani kadhaa za mizigo
IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment
Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.