Send to a friend |
NI KUHUSU MCHAKATO WA KATIBA MPYA JUZI, KAMATI KUU YAJIFUNGIA KUJADILI, NCCR- MAGAUZU WATOA TAKMO LAO Fidelis Butahe MKUTANO kati ya Rais Jakaya Kikwete na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) uliofanyika juzi Ikulu, Dar es Salaam ulichukua saa nane kutokana na uzito wa hoja zilizokuwa zimetolewa na pande zote mbili. Novemba mwaka jana, Chadema ilikutana na Rais Kikwete kwa mara ya kwanza Ikulu na kumkabidhi kabrasha lililokuwa na mapendekezo mbalimbali kuhusu mchakato wa mabadiliko ya Katiba ambayo pamoja na mengine, kilitaka mchakato huo urejeshwe upya bungeni na kumtaka mkuu huyo wa nchi asitie saini Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambao ulipitishwa na Bunge. Hata hivyo, siku moja baada ya mazungumzo hayo, Rais alitia saini muswada huo na kuwa sheria. Vyanzo vya habari kutoka Ikulu, vililiambia gazeti hili jana kwamba Chadema ilipewa ratiba hiyo kuanzia saa 10:30 hadi saa 5:45 usiku ili kutoa wigo mpana wa majadiliano hayo yenye nia ya kupata Katiba kwa njia za amani na umoja. Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, katika chumba cha mazungumzo kulitawaliwa na majadiliano ya kina ambayo wakati mwingine, yaliambatana na utani wa hapa na pale kwa mfano, Katibu Mkuu wa Chadema Dk Willbrod Slaa alimwambia Rais: “Watu wanasema nakukwepa Rais.” Ilielezwa kwamba katika mazungumzo hayo, wajumbe wa pande zote mbili walijadili kwa uhuru mkubwa na mkuu huyo wa nchi namna ya kupata Katiba bora bila mikwaruzano. “Mazungumzo yalikuwa ni mazuri tu, pande zote mbili zilizungumza na kutoa hoja zake, kulikuwa na utani wa hapa na pale. Yale ambayo yalionekana kuwa magumu kidogo kila upande uliomba kuyachukua na kwenda kuyafanyia kazi zaidi kabla ya kufikia uamuzi wa mwisho.” Novemba 28 mwaka jana, Rais Kikwete alisaini muswada huo na kukamilisha safari ya kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011 baada ya Bunge kuwa limeupitisha. Tangu wakati huo Rais Kikwete amekuwa akitutana, kusikiliza na kuchukua maoni na mawazo ya wadau mbalimbali kutoka vyama vya siasa, asasi za kijamii na makundi mengine ya kijamii kuelekea mchakato wa kupata Katiba Mpya. Mchakato huo umekuwa ukipingwa na kwa hoja mbalimbali zikiwamo za kuundwa kwa tume ya kuratibu mchakato huo, hadidu za rejea, mamlaka ya uundaji wa tume na uteuzi wa wajumbe na wapi tume itapaswa kuwajibika. Kauli ya Ikulu Taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu na kusainiwa na Mwandishi wa Habari Msaidizi wa Rais, Premi Kibanga ilisema Rais Kikwete alisema licha ya nchi kuwa na Katiba ambayo imelilea vizuri taifa, inahitajika Katiba mpya inayokwenda na wakati. Alisema baada ya kumalizika kwa kikao na viongozi wa NCCR-Mageuzi, Rais Kikwete alikutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Chadema, ikiwa ni mwendelezo wa mazungumzo yao yaliyoanza mwishoni mwa Novemba, 2011 kuhusu Katiba Mpya. “Katika mazungumzo haya na vyama vya siasa, Rais amesisitiza kuwa lengo lake ni kuhakikisha kuwa hatimaye Watanzania wote watakiri kuwa Katiba Mpya ni yao wote na hatimaye ifikapo mwaka 2015 nchi iweze kufanya uchaguzi wake na Katiba Mpya,” alisema Kibanga. Chadema wajifungia Dar Kwa upande wa Chadema, jana Kamati Kuu (CC) chini ya Mwenyekiti wake Freeman Mbowe ilikuwa katika Hoteli ya Protea Dar es Salaam kujadili mkutano huo na Rais, Ikulu juzi. Katika kikao hicho, Kamati Maalumu ya Chadema kuhusu mchakato huo wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011, iliwasilisha taarifa yake. Taarifa ya chama hicho, iliyotolewa na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika ilisema uamuzi wa CC kuhusu mkutano na Rais Kikwete utatolewa baada ya kikao hicho kumalizika. Akizungumzia mkutano wa Ikulu, Mnyika alisema kamati hiyo maalumu ya Chadema iliyokutana na Rais Kikwete ikiongozwa na Mbowe, ilitaarifiwa hatua ambayo imefikiwa na Serikali katika kuanza kuiboresha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011, ili ikidhi mahitaji ya kuaminiana na muafaka wa kitaifa kwa mawasiliano na ushauri wa wadau mbalimbali. Kauli ya NCCR-Mageuzi NCCR-Mageuzi kwa upande wake, kilitoa taarifa kwa vyombo vya habari kikidai kwamba Rais Kikwete amekubali kuifanyia marekebisho sheria hiyo. Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia ambaye aliongoza na ujumbe wa watu sita kwenda Ikulu Dar es Salaam juzi, alisema jana kwamba baada ya kuwasilisha ajenda zao mbili kuhusu katiba na umeme, waliambiwa sheria hiyo itafanyiwa marekebisho katika kikao kijacho cha Bunge. Mbatia aliwaambia waandishi wa habari kwamba pamoja na sheria hiyo kurudishwa bungeni, pia walimwomba Rais Kikwete aifanyie marekebisho Ibara ya 98 ya Katiba ya sasa kwa kuwa inachangia kukwamisha mabadiliko ya Katiba. “Lengo la kuanzishwa kwa NCCR-Mageuzi ni Watanzania kuwa na Katiba yao na hata Rais wa Awamu ya Tatu (Benjamin Mkapa), tuliwahi kumweleza kwamba Katiba ni ya kudumu na lazima iundwe kwa maslahi ya wananchi na ndicho tulichomweleza Rais Kikwete,” alisema Mbatia. Alisema tangu wakati huo nchi imekuwa na katiba yenye mfumo wa chama kimoja, licha ya kuwa ilipitishwa sheria ya kuwa na vyama vingi. Mbatia alisisitiza kwamba, katika msafara wa chama hicho Ikulu, Mkuu wa Idara ya Katiba na Sheria wa chama hicho, Dk Sengondo Mvungi alitumia zaidi ya saa moja kumfafanulia Rais Kikwete na timu yake jinsi mchakato wa kuandika Katiba Mpya unavyotakiwa kuwa. Alisema walimweleza Rais Kikwete kwamba suala la Katiba ni la kisiasa, hivyo si vyema Tume itakayoundwa ikaachwa chini ya uangalizi wa wanasheria pekee. “Katika tume hii wanatakiwa kutumiwa wataalamu mbalimbali hata kama watakuwa wanasiasa… kinachotakiwa ni kuangalia uwezo wao,” alisema Mbatia. Katika kikao hicho cha Rais na NCCR-Mageuzi, viongozi wa Serikali waliokuwapo ni pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Emmanuel Nchimbi na ujumbe wa chama hicho uliwajumuisha pia Makamu Mwenyekiti wake, Zanzibar, Ambary Hamisi, Naibu Katibu Mkuu George Kahangwa, Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali, Mweka Hazina Taifa, Mariam Mwakingwe, na Mbunge wa Kasulu Vijijini, Zaituni Buyogela. Mwananchi.co.tz |
No comments:
Post a Comment
Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.