Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Tuesday, January 17, 2012

NAKUAGAJE REGIA?-zitto kabwe



Siku zote ninaamini katika sera za vizazi kufundana na kukabidhiana
majukumu. Katika maisha ya kijamii ninaumizwa sana na kupotea kwa
utamaduni wa wazazi kurithisha watoto wao masuala kama ufundi na hata
majukumu ya kitamaduni kwenye mila na desturi zetu. Ndio maana hivi
sasa kwenye vijiji vingi hapa nchini imekuwa nadra kupata mafundi
Seremala wa kurithi ama Waashi pia. Kwenye Siasa Kizazi kinaposhindwa
kuandaa kizazi kingine kuchukua jukumu la kuongoza kuna hatari kubwa
ya Taifa kukosa viongozi walioandaliwa vema na hivyo kuongoza
inavyopasa. Taifa huumia sana linapopoteza viongozi wanaoandaliwa
kubeba majukumu mazito ya kitaifa.
Dada Regia Estelatus Mtema, Mbunge wa Viti Maalumu, Waziri Kivuli wa
Kazi na Ajira na Mjumbe wa Kamati Kuu CHADEMA ni mmoja wa wanasiasa
vijana waliokuwa wanafundwa kuchukua majukumu zaidi ya Taifa letu.
Alikuwa anafundwa na Chama chake. Alikuwa anafundwa na Bunge (mafundo
kutoka kwa vyama vyote na hasa Spika Anna Simamba Makinda). Alikuwa
anafundwa na marafiki zake. Alikuwa anafundwa na Chama cha Walemavu
Tanzania (CHAWATA). Alifundwa na Shirika la FES. Dada Regia alikuwa
anafundika. Alikuwa ni Hazina kubwa kwa Taifa letu. Alikuwa na sifa za
peke yake kabisa kulinganisha na wanasiasa wengine na hasa wanasiasa
vijana. Nitaeleza.
Sijui ni kwa nini mama yangu Bi Hajjat Shida Salum amekuwa sasa
anapata habari kwanza kabla yangu (yeye ndiye aliyenipa habari za
msiba wa Mwenyekiti wa Mkoa wa Shinyanga na Rafiki yangu kipenzi
Shelembi).
Nikiwa nimepumzika sebuleni, nyumbani kwetu Tabata Bi Shida ghafla
ananiuliza, umeongea na dada yako? Ilikuwa kama saa sita mchana hivi,
yeye kasimama upenoni mwa ukuta ananiangalia macho makali. Nikashtuka
kidogo maana amekuwa mgonjwa mgonjwa toka amerejea toka Hijja miezi
kadhaa iliyopita. Najua akiniuliza hivyo ana maanisha nani (Mhonga
Said Ibrahim Ruhwanya), nikamjibu sijazungumza naye, kunani?
Akaniambia piga simu makao makuu nasikia kuna Mbunge wetu wa Viti
Maalumu amepata ajali. Mara moja nikashika simu kumpigia ndugu Msafiri
Mtemelwa. Alichoniambia sikuamini. Eti kwamba Regia amepata ajali na
amefariki muda mfupi uliopita. Nikamwita rafiki yangu Hatibu Mchange
anayeishi jirani yetu kumwambia aje ili anisindikize makao makuu ya
chama. Kisha nikamjulisha Bi Shida kuhusu msiba wa rafiki yake na
mwanae Regia. Nikamwacha akilia sana. Sikumpa pole wala kumtaka asilie
maana kwanza sikuamini kabisa kwamba ni kweli Regia ametutoka.
Nikasema mpaka nikamwone mwenyewe kwa macho yangu.
Siku nne kabla ya kifo chake Regia alikuja nyumbani kumsalimu mama
yetu (Bi Shida siku zote alimwona Regia kama mwanaye na yeye Regia
alimheshimu mama yangu kama mama yake mzazi kabisa). Wakati
namsindikiza akaniambia, ‘ naona umeshikia bango suala la ajira kwa
vijana. Nakuunga mkono na unipe ‘data’ za kutosha ili kupitia Wizara
yangu nilisukume suala hilo kwa nguvu zaidi’. Tukakubaliana.
Tukakumbatiana na kuagana. Yeye alikuwa ameambatana na kulwa wake
Remija. Kumbe ndio nilikuwa namuaga moja kwa moja dada yangu Regia
Estelatus Mtema, mwanasiasa kijana asiye na woga na jasiri haswa. Hii
ndio sifa yake kubwa kuliko wanasiasa wengi vijana. Ujasiri!
Regia hakuwa mwanasiasa wa asili ama kurithi. Aliamua kuingia kwenye
siasa kwa kwanza ushahiwishi wa ndugu David Kafulila ambaye walikutana
huko kwenye Programu ya Mafunzo kwa vijana (YLTP) inayoendeshwa na
Shirika la Friedrich Ebert Foundation (FES), mimi ni mwanzilishi wa
Programu hii katika YLTP 1. David akiwa mwakilishi wa CHADEMA na Regia
akiwa Mwakilishi wa CHAWATA katika YLTP 6. Regia alishawishika na
kuingia CHADEMA, chama kikamweka kitengo cha Vijana kama Afisa. Wakati
fulani kukatokea matatizo kati yake na Afisa mwenzake ndugu Ali Omar
Chitanda kuhusu namna ya kufanya kazi. Regia akiwa na hoja kwamba
chama kinajenga ushawishi kwa wasomi na hivyo vijana wasomi tu ndio
waendeshe kitengo kile. Wakawa hawawezi kufanya kazi na mwenzake
kabisa. Nikiwa Naibu Katibu Mkuu wa chama nikachukua maamuzi ya
kumhamisha Regia na kumpeleka kuwa Afisa wa Mafunzo chini ya Kurugenzi
ya Mafunzo na Oganaizesheni inayoongozwa na ndugu Benson Kigaila
Masalamakali. Regia kwa ujasiri akaniandikia ujumbe mfupi wa simu
‘uamuzi wako sio sahihi’. Sikumjibu bali nikamwita Ofisini siku ya
Pili yake. Nikamweleza namna ambavyo chama kinahitaji kada zote na
kwamba wasomi wa vyuo vikuu waje kwenye chama wakijua pia kuna maafisa
ambao si wasomi na wana mchango mkubwa katika harakati za
kidemokrasia. Nikampa mifano ya namna mtu Kama Samora Machel
alivyochaguliwa kiongozi wa FRELIMO ilhali kulikuwa na wasomi zaidi
yake kama Joachim Chisano au hata mkewe Graca Machel. Regia alinielewa
vizuri sana na mkutano ukaishia kutaniana kuhusu namna ya mitindo ya
uongozi. Regia hakuficha kama hakupenda jambo na wala hakuwa
anaangalia cheo cha mtu. Alisema anachokiamini na mengine yatabaki
mjadala wa baadaye.
Ujasiri wake wakati mwingine ulimletea shida kwa wakubwa zake lakini
hakuna hata mmoja aliyetilia shaka mapenzi yake kwa chama chetu.
Hakujali kuudhiwa na alikuwa tayari kukilinda chama muda wote. Huu ni
mfano wa pili wa Ujasiri wake kisiasa.
Wakati wa uchaguzi Mkuu wa nchi mwaka 2010 Regia alikwenda kugombea
Ubunge katika Wilaya ya nyumbani kwao Kilombero. Watu wengi hawakumpa
nafasi kubwa ya kushinda. Aliliandaa jimbo lake kwa mikutano ya mara
kwa mara. Alishinda kura za maoni katika mchakato wa ndani ya chama.
Katika kikao cha Kamati Kuu mmoja wa Wakurugenzi wa Chama akasema
tunaye mgombea mwingine mzuri sana, Mwanasheria. Regia akaombwa kukaa
pembeni. Akakubali. Kamati Kuu ikampitisha mtu ambaye hakwenda kwenye
kura za maoni na wala hatukuwa tunamjua maana tuliambiwa na mtu
tunayemwamini kwamba ni mgombea mzuri. Regia hakufurahishwa na uamuzi
ule lakini kwa heshima na utiifu wa hali ya juu akakubali kutogombea.
Siku za kurejesha fomu za kugombea zilipokuwa zinakwisha yule mgombea
akatoa nje. Hakuonekana, kwa sababu mbalimbali ambazo sisi tuliokuwa
mbali na Dar es Salaam na Morogoro hatuzijui. Chama hakikuwa na namna
isipokuwa kurudi kwa Regia kumwomba aokoe jahazi. Regia hakusita.
Akaendesha kampeni za uhakika akiwa hana mali wala jina kisiasa.
Akaaminiwa na watu wa Kilombero. Akapata kura nyingi sana ambazo hata
zilileta utata wa uhalali wa matokeo ya uchaguzi katika Jimbo lile.
Ujasiri na nidhamu ya namna hii ni nadra sana kwa wanasiasa sio tu
vijana hata waliobobea kwenye siasa. Huyu ndio Regia. Ndiye
tunamsindikiza kwenye nyumba yake ya milele. Regia mwenye upendo wa
dhati kwa watu aliowapenda. Regia aliyekuwa tayari kusaidia kwa hali
na mali wenzake wanapohitaji msaada. Hii ni sifa yake ya nyingine ya
kipekee.
Mara baada ya Uchaguzi Mkuu na yeye kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Viti
Maalumu, Spika alitugawa kwenye Kamati Wabunge wote. Kazi ya kwanza ya
Kamati hizi ilikuwa ni kuchagua wenyeviti na makamu wao. Regia alijua
mimi napenda kuendelea kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mashirika
ya Umma (uwekezaji umma). Hata hivyo alijua nina wakati mgumu sana
kutokana na mazingira ya kisiasa yaliyokuwapo wakati ule kati ya
Wabunge wa CCM na CHADEMA. Regia ni Mbunge pekee (ukiachana na wajumbe
wa kamati ya POAC kutoka CHADEMA) aliyezunguka nami usiku kucha na
kupiga simu kwa kila Mbunge mjumbe wa Kamati yangu kuniombea kura.
Mbunge mwenzangu na Rafiki yangu wa karibu kutoka Ludewa Deo
Filikunjombe atamkumbuka Regia kwa aina ya kampeni aliyopiga. Deo
aliniambia kwamba alipokea simu ya mwanamke anaongea Kipangwa (moja ya
Lugha ya watu wa Ludewa). Mwanamke yule mwenye sauti nyembamba na ya
kutulia alikuwa anamwombea kura Zitto kuwa mwneyekiti wa POAC. Deo
alifurahishwa na namna Regia alivyoweza kutumia lugha ya nyumbani kwao
kuniombea kura. Hata tulipopata taarifa kwamba Kamati ya Wabunge wa
CCM imeamua kwamba atakayepewa kura sio mimi, Regia alinitia moyo na
kuendelea na kampeni. Asubuhi ya siku ya kura alimpitia kila mjumbe wa
Kamati POAC aliyemwona na kumkumbusha kunipa kura hata kama CCM
imewakataza. Nilimcheka sana Regia kwa kumwambia wewe sio mzoefu hapa.
Hao wakishakaa ndio maamuzi hayo. Akaniambia hapana watabadilika.
Ghafla Waziri Mkuu akatangaza kikao kingine cha Wabunge wa CCM na huko
wakaelezwa kwamba kamchagueni Zitto. Ningekata tamaa bila kuendelea na
juhudi usiku kucha kama nilivyoshauriwa na regia kwa kweli
nisingeshinda nafasi ile. Regia alikuwa mtu wa kwanza kumjulisha
matokeo ya uchaguzi nilipopata kura 13 kati ya 15 zilizopigwa. Huyu
ndiye Regia ambaye alikuwa na uwezo wa kufanya kila mbinu ili mwenzake
apate msaada. Ni lazima watu watoe machozi. Ni lazima Wabunge watoe
machozi. Ni lazima wana CHADEMA wamlilie. Mimi sitawafuta machozi na
nimekataa kulia.
Kikao cha mwisho cha chama ambacho nilishiriki na Regia nilihudhuria
kwa muda mfupi sana. Wenzangu watakumbuka mengine katika kila kikao
kile. Mimi ninakumbuka moja tu ambalo ni moja ya sifa pekee aliyokuwa
nayo na wanayo wanasiasa wachache sana na hasa wanasiasa vijana (ambao
hupenda zaidi siasa za kuridhisha kwa kusema watu wapendacho). Regia
alikuwa na uwezo mkubwa wa kusema usichopenda kusikia. Alisema tu.
Katika kikao kile wajumbe na Wabunge walikuwa katika ‘emotion’ sana
kuhusiana na muswada wa mchakato wa kuandika Katiba. Mjadala ulikuwa
mkali sana. Mwenyekiti wetu akampa nafasi Regia aseme. ‘mimi nashauri
tuombe kuonana na Rais Kikwete’ yalikuwa ni maneno yake makali kupenya
kwenye ngome za masikio ya wengi na yalipokelewa kwa mguno mkubwa.
Mwenyekiti akaamrisha wajumbe na Wabunge watulie kwani Regia ana haki
ya kutoa maoni yake. Mimi niliondoka baada ya muda mfupi maana
nilikuwa ndio nimetoka nchini India kwa matibabu na nilikuwa na
masharti ya kupumzika muda mrefu. Ushauri wa Regia (pamoja na wajumbe
na viongozi wengine wa chama walioshauri ama waziwazi au kwa
chinichini) ndio uliofuatwa na sasa kumekuwa na mazungumzo ya mara kwa
mara ya viongozi kuhusu sheria ile ya mchakato wa kuandika Katiba.
Huyu ndio dada Regia. Maisha mafupi lakini mafunzo makubwa katuachia
vijana wenzake kwenye medani ya siasa.
Nakuagaje Regia?
Nilikataa kuamini kuwa umekufa. Nikasema mpaka nikuone.
Nilipofika Tumbi, nikasema hujafa na wala siingii ‘motury’ kukuona.
Sasa eti nakuandikia Tanzia . Kwa nini nikuage?
Halafu nakuagaje REGIA?
Ukikutana na Shelembi Magadula, mwambie kile kiti chake cha udiwani
tulikitunza, akija atakikuta. Ukikutana na Chacha Wangwe Mwambie bado
tunaendelea na harakati Nyamongo. Ukikutana na Amina mwambie asilie
tena vijana wengi wameingia Bungeni na sasa wanaelekea Ikulu.
Ukikutana na Bibi Titi mwambie sasa wanawake hata wanawake walemavu
wanaweza bila hata kuwezeshwa, wanajiwezesha.
Nakuagaje dada yangu mpenzi? Haya.
Mungu atupe subira.

Kabwe Zuberi Zitto, Mb
DSM, 16 Januari 2012.

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.