Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Tuesday, January 10, 2012

Tendwa aishukia CUF

 Send to a friend
Monday, 09 January 2012 21:32
0digg
Msajiri wa Vyama vya siasa nchini, John Tendwa
ASEMA ADHABU YA KUIADHARAU MAHAKAMA NI KUFUTWA, MTATIRO ASEMA ADHABU IKO PALEPALE
 Waandishi wetu  MSAJILI wa Vyama vya siasa nchini, John Tendwa amekionya Chama cha Wananchi (CUF), kwa kuendesha kikao kilichowajadili na kuwafukuza Hamad Rashid Mohamed na wenzake wakati kimepewa amri na Mahakama Kuu ya kutofanya hivyo huku akikitaka kirejee na kutii amri hiyo.Kauli ya Tendwa imekuja siku moja baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Werema kusema kitendo hicho cha CUF kuendesha kikao hicho ni ukiukwaji wa Katiba ya nchi.  “Sijaiona amri ya mahakama (court order) inayowazuia CUF kuendelea na mkutano wao, lakini ninasema kuwa kuna uhalali wa kuwapo kwa tukio hilo? Ushauri wangu ni kwamba CUF warudi kutekeleza amri ya mahakama,” alisema Dar es Salaam jana na kuongeza:
“Mahakama ni mhimili wa Serikali wenye mamlaka kamili ya Katiba ya nchi. Mahakama imefanya uamuzi unaopaswa kuheshimiwa.”  Alitaja baadhi ya makosa ambayo chama kinaweza kupoteza sifa ya kuwa chama cha siasa kuwa ni pamoja na kukiuka Katiba ya nchi, kuwa na siasa za upande mmoja na kufanya siasa zinazochochea vurugu.

Barua kutoka CUF
 Kuhusu barua kutoka CUF, Tendwa alisema ofisi yake haijapata barua yoyote ya chama hicho inayoeleza kuhusu uamuzi wa kumfukuza uanachama Hamad Rashid na wenzake.  “Mimi sijaona barua kutoka CUF inayohusu kufukuzwa uanachama kwa Hamad na hata ingekuwa imepelekwa Ofisi za Bunge ningefahamishwa,” alisema Tendwa.

 Tendwa alisema sababu zinazotolewa na CUF kuwa Hamad Rashid alikuwa akifanya mikutano kinyume na taratibu za chama, hazina mashiko kwa kuwa hakuna kosa kwa mbunge kufanya mkutano wa hadhara na wananchi.  “Hakuna kosa kwa mbunge aliyechaguliwa na wananchi kufanya mkutano mahali popote katika nchi na kutoa msaada, si lazima kuomba ruhusa kwa yeyote wakati akitekeleza jukumu hilo,” alisema Tendwa.  Aonya vyama

Tendwa alivionya vyama vya siasa kutatua migogoro kwa njia ya mazungumzo badala ya kufukuzana uanachama akisema
mfumo huo ndiyo unaoweza kujenga vyama hivyo na kuvipatia uwezo wa kukubaliwa na wananchi na kupewa dhamana ya kuongoza nchi.

“Mfano, leo hii  CUF wanachama wake wanarudisha kadi kwa tukio la Hamad… huku ni kukidhoofisha chama,” alisema Tendwa.  Hamad: Sijapewa barua   Kwa upande wake, Hamad Rashid alisema bado hajapewa barua ya kufukuzwa uanachama lakini akasema kwamba viongozi wa CUF wamepeleka barua ya kutomtambua katika Ofisi ya Bunge.

Alisema hadi jana alikuwa hajapokea barua yoyote inayoonyesha kufukuzwa uanachama, jambo alilodai ni kinyume cha kanuni na taratibu za kumvua mtu uanachama.  “Mpaka sasa sijapokea barua ya kunivua uanachama lakini, nimesikia kwenye vyombo vya habari kuwa viongozi wa CUF wamepeleka barua ya kutonitambua kwa Spika wa Bunge,” alisema Hamad.

  Alisema kutokana na viongozi hao kutofuata taratibu,  amepanga kumwandikia barua Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah ili kumweleza kuwa hajapokea barua ya kufukuzwa rasmi ndani ya chama na kwamba uamuzi wa kutokuwa mwanachama wa CUF hautambui.  Alisema leo anatarajia kwenda Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam kupeleka hati ya kiapo pamoja na kuhoji hatua zitakazochukuliwa dhidi ya Baraza Kuu la CUF, kwa kukaidi amri ya mahakama ya kuitaka kuahirisha mkutano wa Januari 4, mwaka huu Visiwani Zanzibar.

Alisema ataifikisha hati hiyo ya kiapo kinachoonyesha kuwa walipeleka barua ya kupinga kikao hicho mahakamani hapo akiwa pamoja na wanachama wengine watatu.  “Lengo la kwenda mahakamani ni kuhoji mahakama ni hatua gani zitachukuliwa kwa viongozi wa Baraza Kuu la CUF waliovunja amri ya mahakama ya kutakiwa kusitisha mkutano,” alisema Hamad Rashid.

Alisema pamoja na kuhoji juu ya kuvunjwa kwa amri hiyo, atataka kujua msimamo wa Mahakama kuhusu uamuzi batili uliotolewa ndani ya kikao hicho.

CUF wajibu  Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu CUF (Bara), Julius Mtatiro alisema chama hicho kina heshimu kauli ya Jaji Werema na kwamba kama kingepata hati halisi (origional) ya mahakama kisingeweza kuendelea na mkutano uliowavua uanachama Hamad  Rashid na wenzake.

 “Hamad alikuwa na nakala ya hati ya mahakama na jambo lile lilikuwa la kisheria, CUF tusingeweza kukubaliana na hati kivuli, tunatambua hati halisi ya mahakama tu,” alisema Mtatiro.  Alisema siku moja baada ya kurejea Dar es Salaam wakitokea Zanzibar, walielezwa na walinzi wa chama hicho kuwa kuna barua ililetwa katika ofisi za chama hicho, Buguruni ikiwa na anuani ya makao makuu ya chama hicho ambayo yako Zanzibar.

Bila kufafanua kama barua hiyo huenda ndiyo ilikuwa ya Mahakama Kuu aua la alisema: “Walinzi walimjibu yule mtu kuwa Makao Makuu ya CUF ni Zanzibar siyo Dar es Salaam, na ile barua ilikuwa na anuani ya Zanzibar.”  Alisema mpaka jana walikuwa hawajapata barua yoyote ya mahakama inayozuia uamuzi waliochukua na kwamba hata kama wakiipata haitaathiri chochote kuhusu uamuzi huo.

“Hata kama mahakama ikileta barua leo(jana) haitaweza kuathiri uamuzi wa kuwavua uanachama Hamad na wenzake,” alisisitiza Mtatiro.  Alisema hadi jana, chama hicho kilikuwa hakijawapa barua ya kuwavua uanachama Hamad Rashid na wenzake kwa kuwa baada ya uamuzi, ni lazima kikao kingine kifanyike ili kujiridhisha juu ya uamuzi uliochukuliwa.

   Alichosema Werema Juzi, Jaji Werema alisema: “Sina hakika kama amri hiyo ipo, lakini kama kweli kuna 'court injuction' iliyotolewa na Mahakama kuzuia Hamad Rashid na wenzake wasijadiliwe na Baraza la Uongozi na kuwafukuza, basi CUF imevunja Katiba.

Tena hakiishii kuvunja katiba tu, kosa hilo linakwenda mbali zaidi na kukifanya chama hicho kikose uhalali wa kuendelea ku-exist (kuwepo).”  Alisema katika mifumo ya utawala duniani, kuna chombo cha mwisho cha uamuzi ambacho kimsingi, kinapaswa kuheshimiwa na vyombo vingine vyote bila kuhojiwa na kwa hapa nchini, Mahakama ndiyo yenye mamlaka hiyo.

Pamoja na Hamad Rashid, wengine waliovuliwa uanachama na kikao hicho cha Baraza Kuu ni Wajumbe wa Baraza hilo na maeneo wanayotoka yakiwa kwenye mabano ni Doyo Hassan Doyo (Tanga), Shoka Hamis  Khamis Juma (Pemba) na Juma Saanane (Unguja). 
Habari hii imeandaliwa na Fidelis Butahe, Geofrey Ngang’oro na Aziza Masoud.

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.