Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Wednesday, January 18, 2012


Na Mwandishi Wetu
PICHA zilizopigwa eneo la tukio kwa simu muda mfupi baada ya ajali iliyosababisha kifo cha Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Mkoa wa Morogoro, Regia Mtema, zinathibitisha mateso makubwa aliyoyapata shujaa huyo.
Risasi Mchanganyiko, linaweza kuwa gazeti pekee lenye picha hizo za kusikitisha zenye kukutoa machozi, zinazomuonesha shujaa Regia akiwa ametulia kwenye kiti baada ya kukata roho na nyingine zikionesha matukio tofauti wakati anaondolewa eneo la tukio.
Kwa ushuhuda wa gazeti hili, Regia ambaye alikuwa Waziri Kivuli wa Kazi na Ajira, aliumia kwa kiasi kikubwa kichwani, hivyo ilikuwa ni vigumu kunusurika kifo.
Gazeti hili limebaini kuwa Regia alitimiza nidhamu ya kufunga mkanda ndiyo maana mauti yalimkuta akiwa amekaa kwenye siti yake, upande wa dereva.
Mtiririko wa matukio hatua kwa hatua unaonesha kuwa baada ya Regia kuondolewa eneo la ajali, mwili wake ulipelekwa Hospitali Teule ya Mkoa wa Pwani, Tumbi na baadaye kuhamishiwa Hospitali ya Taifa    Muhimbili.
Regia ambaye alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alifikwa na mauti Jumamosi iliyopita (Januari 14, 2012) baada ya gari lake aina ya Toyota Land Cruiser VX lenye namba za usajili T 296 BSM, kupinduka mara saba eneo la Ruvu Darajani, Pwani.

USHUHUDA
Rogers Abdallah ambaye ni majeruhi wa ajali hiyo, alikaririwa na gazeti ndugu na hili, Ijumaa Wikienda akizungumza akiwa Hospitali ya Tumbi kuwa Regia ndiye aliyekuwa akiendesha gari hilo.
“Ilikuwa saa 5:15 asubuhi. Tulikuwa tunatokea nyumbani Mbezi Makabe tunakwenda Ruvu shambani. Tulipofika Ruvu darajani, alitaka kulipita lori lakini alipoanza kulipita, tukakutana uso kwa uso na lori lingine.
“Ili kulikwepa lori, ikabidi apindishe kulia kwa kulitoa gari nje ya barabara, bahati mbaya tairi la kushoto lilipasuka, hivyo gari kupinduka mara saba,” alisema Rogers.

PACHA WA REGIA
Maelezo ya pacha wa Regia, Remija Mtema (32) ambaye ni kurwa, yaliwaliza wengi kwani muda mfupi alikuwa na marehemu kabla ya kupanda gari kuelekea Iringa ambako ni diwani katika moja ya kata za Wilaya ya Iringa.
“Tulitoka nyumbani kwake Mbezi-Makabe, Dar kwenye saa tatu asubuhi, nilikuwa nakwenda Iringa na tuliondoka na gari lake hilo lililopata ajali, wakanishusha Mbezi stendi ili nisubiri basi la Iringa.
“Wakati tunatoka nyumbani alikuwa anaongea kwa uchangamfu sana, kwanza Ijumaa (siku moja kabla ya kifo) tulizungumza na kupanga kwamba mimi niende Iringa kuomba ruhusa kazini, maana kuna wakati nikiwa huru namsaidia kazi kama Katibu wake, tulipanga nikipewa ruhusa nirudi nimsaidie kwenye Kamati na Bungeni.
Hata pale stendi hakutaka kuondoka, alisubiri hadi nikapata gari ndiyo akaendelea na safari yake,” alisema Remija.
Kwa mujibu wa Remija, walikubaliana hivyo na baada ya kupanga mambo yao usiku huo wa Ijumaa, walicheza sana karata huku Regia akitoa kauli za kutia moyo wakitarajia kuonana tena, lakini haikuwezekana, jambo ambalo liliwaliza wengi alipokuwa akiwasimulia.

KUZIKWA LEO IFAKARA
Regia anatarajiwa kuzikwa leo nyumbani kwao Ifakara, Morogoro, ikiwa ni baada ya tukio kubwa la kumuaga kitaifa, lililochukua nafasi jana Jumanne kwenye Viwanja vya Karemjee, Dar.
Kabla ya kuagwa kitaifa juzi Jumatatu, marehemu Regia aliagwa na familia yake kwenye Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Tabata ambako ibada ya kumuombea marehemu ilifanyika.
Katika ajali hiyo, Regia na msaidizi wake wa kazi za nyumbani, Theresia Simon walipoteza maisha, wakati wengine sita walijeruhiwa.

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.