Kwa wale waliokuwa wakimfahamu Marehemu Kagashe, watakubali kuwa alikuwa mmoja wa waandishi makini, waliokuwa wakiamini kuwa jamii ya Watanzania inaweza kufanya mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, kufikia ustawi na maendeleo yanayohitajika, hivyo kwa kutumia vyema taaluma yake, akiongozwa na maadili ya tasnia ya habari, alishirikiana na Watanzania wenzake katika kuelimisha, kuhabarisha, kuhamasisha na kuburudisha umma, katika masuala mbalimbali, kupitia kalamu yake .
Kurugenzi ya Habari na Uenezi ya CHADEMA itamkumbuka Marehemu Kagashe kuwa mmoja wa wanafunzi wa mwanzo kabisa kusomea Shahada ya Uandishi wa Habari, katika Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), mara tu baada ya chuo hicho kuanzisha programu ya masomo hayo, kupitia iliyokuwa Taasisi ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (IJMC), ambayo sasa inatambulika kama Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC), chini ya chuo hicho.
Kurugenzi hii pia itakumbuka namna ambavyo Marehemu Kagashe alikuwa mmoja wa vijana wa mwanzo kabisa kutoka vyuo vikuu mbalimbali nchini, waliopelekwa na Kampuni ya Mwananchi Communications nchini Kenya, kupata mafunzo ya kuwaivisha zaidi katika taaluma ya uandishi, ikiwa ni matunda ya programu ya kusaka watu makini na wenye uwezo wanaohitimu masomo yao vyuoni na wako tayari kutumikia taaaluma hiyo nyeti, programu ambayo imekuwa ikifanywa na kampuni hiyo kwa muda mrefu sasa.
Bila shaka mambo haya ndiyo yalimsaidia na kumjenga Marehemu Kagashe kuwa mmoja wa wapambanaji mahiri katika kutumia taaluma yake kuutumikia umma wa Watanzania.
Tunatoa pole kwa ndugu, jamaa, marafiki na wafanyakazi wenzake Marehemu Kagashe na kuwaombea kwa Mungu awape moyo wa subira katika wakati huu mgumu wa majonzi kwa kuondokewa na mpendwa wao, halikadhalika Gazeti la The Citizen na Kampuni ya Mwananchi Communications kwa kumpoteza mmoja wa wafanyakazi wake makini, waliyemuandaa kuwatumikia.
Kurugenzi ya Habari na Uenezi CHADEMA iko pamoja na Watanzania wote walioguswa na msiba huu.
Mungu ailaze mahali pema peponi roho ya Marehemu Beatus Kagashe, Amina.
Imetolewa na;
Tumaini Makene
Afisa Habari CHADEMA
Januari 22, 2012
No comments:
Post a Comment
Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.