Mahakama kuu nchini Kenya imetoa mapendekezo mawili ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu nchini humo.
Katika nafasi ya kwanza mahakama hiyo imependekeza kuwa uchaguzi huo unaweza kufanyika mwaka huu iwapo Rais Mwai Kibaki na Waziri Mkuu Raila Odinga wataafikiana kwa maandishi kuvunja serikali ya muungano wa kitaifa.Uchaguzi utatarajiwa kufanyika siku 60 baada ya hatua hiyo ya kuvunja serikali kukamilika.
Pendekezo la pili ni uchaguzi mkuu ufanyike mwezi Machi mwaka 2013, siku 60 baada ya kukamilika kwa muda wa bunge la kumi.
Bunge la sasa linakamilisha muhula wake tarehe 14 Januari, 2012.
Tofauti na ilivyokuwa chini ya katiba ya awali, Rais Mwai Kibaki sasa hana uwezo wa kuvunja bunge na kamati ya bunge ndio inayoendesha shughuli zake.
Majaji wa mahakama ya kikatiba Isaac Lenaola, David Majanja and Mumbi Ngugi, pia wameamuru kuwa tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) ndiyo itakayoamua siku hasa ya uchaguzi huo baada ya kuzingatia uamuzi huo.
Uamuzi huu umepongezwa na mwenyekiti wa tume ya utekelezwaji wa katiba (CIC), Charles Nyachae, ''sisi kama CIC tumekuwa tukisema wakati wote kwamba kama kuna jambo lolote katika katiba ambalo lina utata na linafaa kutatuliwa mahali pa kutatua hilo jambo ni mahakamani'' , Bwana Nyachae amesema.
Bwana Nyachae ameongeza kuwa ni jambo nzuri kwamba utata kuhusu tarehe ya uchaguzi hatimaye umetatuliwa.
Tarehe ya uchaguzi ujao nchini Kenya ni jambo ambalo lilikuwa likisubiriwa kwa hamu kuu na wakenya wengi.
Hii ni kwa sasa, huu ndiyo utakaokuwa uchaguzi wa kwanza tangu uchaguzi wa mwaka 2007 ambao ulighubikwa na visa vya machafuko ambavyo vilisababisha vifo vya zaidi ya watu 1200 na wengine zaidi ya nusu millioni kuachwa bila makao.
No comments:
Post a Comment
Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.