SIKU moja baada ya wanachama wa CCM, Jimbo la Arumeru Mashariki kumpendekeza Sioi Sumari kuwa mgombea wake katika uchaguzi mdogo ujao, baadhi ya wanachama wa Umoja wa Vijana (UVCCM) wilayani humo, wamepinga uteuzi huo wakidai kuwa uchaguzi uligubikwa na mizengwe.

Juzi, mkutano Mkuu wa Jimbo hilo ulimchagua Sioi, mtoto wa aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, marehemu Jeremiah Sumari kwa kura 361 akifuatiwa na William Sarakikya aliyepata kura 259, Elishilia Kaaya (176), Elirehema Kaaya (205), Anthony Musari (22) na Moses Urio (11).

Lakini jana, baadhi ya wajumbe hao wa UVCCM wakiongozwa na Mjumbe wa Baraza la Umoja Mkoani wa Arusha, Kennedy Mpumilwa walidai kwamba uchaguzi huo ni batili kwa kuwa ulitawaliwa na misingi ya rushwa.

Mpumilwa alidai kwamba uchaguzi huo ulijaa rushwa kila kona. Hata hivyo, hakuweka bayana kama walihongwa ili wamchague nani kati ya wagombea hao sita.

Alidai kwamba kigogo mmoja wa UVCCM ngazi ya mkoa aliyeongozana na kada mmoja wa jumuiya hiyo, walikuwa ndani ya gari karibu na eneo la uchaguzi wakigawa rushwa kwa wajumbe.

“Huu uchaguzi haufai kabisa baadhi ya wajumbe walihongwa. Ilikuwa ikitolewa 150,000 kwa kila mjumbe atakayekubali. Sasa hii CCM gani kama uteuzi tu hadi ufuate rushwa,” alidai Mpumilwa.

Alisema kwa jinsi mchakato wa uchaguzi huo ulivyofanyika, ni dhahiri chama hicho kimeingia katika mpasuko mkubwa ambao kama usipoangaliwa kwa makini, unaweza kukiathiri.

Mpumilwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi na Fedha wa UVCCM Wilaya ya Arumeru, alisema baadhi ya wanachama wa umoja huo wilayani humo wamechukizwa na mambo yaliyojitokeza katika uchaguzi huo huku wengine wakitishia kuhamia upinzani wakati wowote.

“Nakwambia vijana wamechukizwa kabisa na kilichofanyika katika mchakato wa uchaguzi, sasa wengine wametishia kwenda upinzani wakati wowote,” alieleza Mpumilwa.

Aliutaka uongozi wa CCM taifa kuingilia kati suala hilo na kulipa uzito akidai kwamba lisipoangaliwa huenda likazua mpasuko mkubwa ndani ya CCM wilayani humo na kusababisha kulipoteza jimbo hilo wakati wa uchaguzi.

Hata hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi ya wa CCM Mkoa wa Arusha, Loota Sanare alisema hadi jana hakuna mgombea yoyote kati ya hao sita ambaye alikuwa amepinga matokeo ya uchaguzi huo.

Alisema ushindi wa Sumari katika uchaguzi wa ngazi ya jimbo, siyo mwisho wa uteuzi na kwamba kuna vikao vya kamati ya siasa ya Wilaya ya Arumeru na baadaye vikao vya mkoa na Kamati Kuu (CC) ya CCM Taifa, ambayo ndiyo itakayomtangaza mgombea.
“Tumezipokea hisia za wana-CCM, Sioi ameongoza ni nafasi nzuri kwake lakini siyo mwisho wa uteuzi wake. Bado kuna mchakato mrefu mbele yake,” alisema Sanare.


Vigogo watimua mbio

Katika hatua nyingine, kushindwa kwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec) wa Mkoa wa Arusha, Elishilia Kaaya katika kura hizo za maoni juzi, kuliibua huzuni kubwa kwa vigogo wa chama hicho huku baadhi yao wakiondoka ukumbini kabla ya matokeo.

Kaaya ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), alikuwa anaungwa mkono na kundi la viongozi wa juu wa CCM na Serikali ambao wamejipambanua kuwa wanapambana na vitendo vya ufisadi. Mjumbe huyo wa Nec alishika nafasi ya nne baada ya kupata kura 176, nyuma ya Sumari, Sarakikya na Elirehema Kaaya.

Dalili za kubwagwa kwa kigogo huyo, zilianza kuonekana mapema nje ya ukumbi ambako baadhi ya madiwani na wana-CCM vijana, walikuwa wakiendesha kampeni nzito ya kutaka mgombea kijana ambaye ataweza kupambana na mgombea machachari wa Chadema, Joshua Nasari endapo atapitishwa na chama chake.

Pia, katika ukumbi wa kupigia kura, mara baada ya wagombea wote sita kujieleza, Sumari alikuwa akishangiliwa zaidi na kundi la vijana hali ambayo iliwasukuma baadhi ya vigogo kuanza kuondoka mapema ukumbini.

Gazeti la Mwananchi.