NAIBU Waziri wa Ujenzi anayeugua ugonjwa uliozusha utata mkubwa serikalini, Dk. Harrison Mwakyembe, ameandika waraka mahususi unaoeleza kile anachokiamini kuwa ni chanzo cha ugonjwa wake, Tanzania Daima Jumatano limebaini.
Waraka huo ambao gazeti hili limeuona mbali ya kueleza kile ambacho Mwakyembe mwenyewe anaamini kuwa ni chanzo cha ugonjwa wake, unaeleza pia jinsi alivyoanza kuugua, watu anaowashuku kuwa nyuma ya mpango huo, siku na tarehe aliyodhani kuwa ndiyo aliyowekewa sumu hiyo.
Kama hiyo haitoshi, Mwakyembe katika waraka wake huo pasipo kueleza chanzo halisi cha undani wa taarifa zake, anaeleza mbinu iliyotumika kumdhuru na mahala mpango huo wa kumdhuru ulipopangwa.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kwamba Dk. Mwakyembe ambaye kwa sasa yuko nchini India ameusambaza waraka huo kwa ndugu, jamaa na marafiki zake wa karibu.
Katika waraka huo, Dk. Mwakyembe anaeleza kwamba anaamini alipewa sumu hiyo akiwa ofisini kwake huku akitaja majina ya watu anaowatuhumu kuwa nyuma ya mpango huo ambao gazeti hili kwa sasa linahifadhi majina yao.
Kwa mujibu wa Dk. Mwakyembe, mara tu baada ya kuwekewa sumu hiyo alianza kuwashwa mwili kabla ya hali kuendelea kuzorota na kuwa mbaya.
Akionekana kujibu hoja za Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, mwanasiasa huyo katika waraka wake anaeleza kwamba hakuwekewa sumu hiyo kwenye chakula, bali kwenye sabuni na kitaulo cha kujifutia, ambacho huwekwa kwenye chumba maalumu ofisini kwake kwa ajili ya kusafisha mikono na huduma nyingine awapo ofisini.
Vyanzo vyetu vya habari kutoka kwa ndugu na marafiki wa karibu wa Dk. Mwakyembe vilisema kuwa, naibu waziri huyo ambaye pia ni Mbunge wa Kyela, amefikia hatua ya kuandika waraka huo kwa lengo la kutaka kuijulisha familia yake na taifa kile anachoamini anakabiliana nacho endapo atapoteza maisha kabla ya ukweli kamili kubainishwa.
Hata hivyo, kutokana na ukweli kwamba suala hilo la afya ya Dk. Mwakyembe liko katika hatua za uchunguzi, Tanzania Daima Jumatano haliwezi kuandika kwa undani kuhusu waraka huo kwa sasa.
Ukiacha hilo, Dk. Mwakyembe katika waraka huo ameelezea historia ya maisha yake kisiasa na mikasa iliyompata kiasi cha kujijengea maadui.
Ameeleza jinsi alivyonusurika kuuawa mara kadhaa na kwamba taarifa zote za mikasa yake aliziripoti polisi, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa na Jeshi hilo la Polisi.
Baadhi ya mikasa aliyoitaja kwenye waraka huo ni pamoja na tukio la kunusurika kuuawa kwenye ajali ya gari iliyotokea Mei 21, mwaka 2009. Ajali hiyo ilitokea eneo la Ihemi, kilomita 40 kutoka Iringa mjini akiwa safarini kutokea Mbeya kwenda Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa waraka huo, gari alilokuwa akisafiria aina ya Toyota Land Cruiser T 362 ACH, liliacha njia saa moja asubuhi baada ya kukanyaga shimo na tairi ya upande wa kulia kuchomoka na dereva wake, Joseph Msuya (30), kupoteza mwelekeo kabla ya gari hilo kutoka nje ya barabara upande wa kushoto na kuparamia mti kisha kupinduka.
Ajali hiyo ilitokea wakati dereva wa Dk. Mwakyembe akijaribu kulipita lori kabla ya kukanyaga shimo hilo.
Anasema katika ajali hiyo aliokolewa na wasamaria wema pamoja na trafiki wawili waliokuwa kwenye basi dogo waliokuwa wakisafiri kutoka Iringa kwenda Njombe.
Anasema katika waraka huo kuwa, baada ya ajali hiyo alilazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa kutokana na kuumia taya kisha alihamishiwa Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.
Kwa mujibu wa waraka huo, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema, aliunda tume iliyoongozwa na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani wakati huo, Kamanda James Kombe, kuchunguza chanzo cha ajali hiyo.
Matokeo yalionesha kwamba ilisababishwa na uzembe wa dereva wake, Msuya wakati Dk. Mwakyembe akiamini kwamba ajali hiyo ilipangwa.
Februari 9, mwaka 2011, Dk. Mwakyembe aliandika barua kwa Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Said Mwema, akimpa taarifa juu ya kuwapo kwa njama za kutaka kumuua yeye pamoja na viongozi wengine.
Wengine aliowataja katika barua hiyo ni pamoja na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, mfanyabiashara maarufu nchini, Reginald Mengi, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Mark Mwandosya, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela.
Katika orodha hiyo ya Mwakyembe kwa IGP, hadi sasa kiongozi mwingine ambaye anaumwa ni Profesa Mark Mwandosya.
Wizara tatu zakorogana
Katika hatua nyingine, mwendelezo wa mjadala kuhusu ugonjwa unaomsumbua Dk. Mwakyembe unaonekena kuzikoroga wizara tatu za serikali ya Rais Jakaya Kikwete.
Mkorogano huo unajitokeza katika Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Afya na ile ya Ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Duru za siasa zinahoji umakini wa serikali kutokana na kushindwa kwake kuwa na kauli ya pamoja iliyofanyiwa utafiti wa kutosha.
Kwa nyakati tofauti, Wizara ya Mambo ya Ndani, kupitia kwa Waziri wake, Shamsi Vuai Nahodha na baadaye kwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, imetoa taarifa iliyoibua mjadala.
Wakati Manumba akikaririwa akisema uchunguzi uliofanywa na Jeshi la Polisi ikiwa ni pamoja na kupata ripoti ya kitabibu kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, umebaini kwamba Dk. Mwakyembe hajalishwa sumu.
Siku mbili baada ya kauli hiyo ya Manumba, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda, alimshangaa Manumba alikopata ripoti hiyo.
Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Waziri wake mwenye dhamana, Samuel Sitta, anasisitiza Dk. Mwakyembe amelishwa sumu.
Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa mgogoro na ukinzani uliojitokeza katika wizara hizo tatu, umeziondolea imani kwa wananchi.
Ingawa taarifa za ndani kutoka Jeshi la Polisi zinaonyesha kuwa kulikuwa na mawasiliano kati ya Wizara ya Mambo ya Ndani na Wizara ya Afya kama ambavyo Manumba alisema.
Lakini pia taarifa hizo zinaeleza kuwa Manumba alikurupuka.
Ingawa kilichosababisha hasa ugonjwa wa Mwakyembe bado hakijabainika kutokana na kauli yake mwenyewe kuwa madaktari wanaomtibu katika Hospitali ya Apollo nchini India, bado wanahangaika kujua kitu kilichoko kwenye uboho (bone marrow) kinachochochea hali ya maradhi yake.
Chanzo: Tanzania daima
|
No comments:
Post a Comment
Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.